ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 31, 2010

2010 umekuachia funzo gani katika mapenzi? - 3

LEO ni Desemba 31, 2010, saa chache kabla ya kuhitimisha mwaka huu na kuanza mwaka mpya wa 2011. Tumuombe Mungu atujalie tuweze kuuona mwaka mpya.

 Yes, leo tunamalizia uchambuzi wa mada yetu ambayo inatoa tathmini ya kile tulichojifunza kwa mwaka mzima unaomalizikia katika sayari ya mapenzi.


Kabla ya kuingia kwenye mada yenyewe, wiki iliyopita niliahidi kuchapisha baadhi ya meseji za wasomaji ambao wanaeleza waliyojifunza katika uhusiano na mapenzi ndani ya mwaka huu. Kutokana na nafasi yangu kuwa finyu, nitachapa meseji kumi tu!

MSOMAJI WA KWANZA: Kaka Shaluwa kilichonipata mwaka 2010 ni kuachana na mpenzi wangu ambaye nimezaa naye mtoto mmoja. Yaani sikutegemea kama tungekuja kuachana tena bila sababu ya msingi. Aliniumiza sana mpaka nikawa nashindwa kula na kulala.
Timilai Shemalamba, Tanga

MSOMAJI WA PILI: Mwaka huu haukuwa mzuri kwangu, nilitarajia kufunga ndoa na mwanaume mmoja kutoka Kenya, alinivisha pete ya uchumba lakini kumbe alikuwa muongo. Nikasema simtaki tena, lakini mwisho nikajikuta sina ujanja, nikaendelea naye ingawa ni mume wa mtu. Sina uhuru naye kabisa. Nahitaji wangu.
Noreen.

MSOMAJI WA TATU: Hi Joseph. Mimi ni mfuatiliaji mzuri wa mada zako na simulizi zako, tangu nikiwa South Africa (kupitia mtandao) lakini sasa nimerudi hapa nyumbani. Nimeumizwa sana mwaka huu, lakini niliposoma hii mada, nahisi kupumua. Sina shaka nitaanza vyema 2011.
(Hajataja jina lake)

MSOMAJI WA NNE:  Nimeguswa sana na kipengele cha pili cha kutafuta amani iliyopotea. Siyo siri nilifanya kosa, ahsante kwa kunifungua. Merry Christmas and Happy New Year my brother.
Rich, Shinyanga.

MSOMAJI WA TANO: Dah! Umenipa raha sana, ukweli nimefarijika sana kwani nilimpenda mtu asiyenipenda so nikaamua kuachana naye coz hakuwa na mapenzi ya dhati kwangu lakini nilikuwa bado naumia kwa uamuzi niliouchukua, lakini baada ya kusoma mada yako, nimefarijika sana.
Vicky, Iringa.

MSOMAJI WA SITA: 2010 ulikuwa mgumu sana kwangu, nilikuwa na mpenzi niliyempenda sana, lakini akawa na mwanaume mwingine wakati akiwa na mimi. Kuna wakati tena akaniaga anakwenda kijijini kwao, kumbe kaenda kwa mwanaume wake, yakanishinda na kuamua kuachana naye.
Naamini mwaka ujao nitampata mwingine mwenye mapenzi ya kweli.
Maico Jacob, Dodoma.

MSOMAJI WA SABA: Mwaka huu kwangu haukuwa mzuri, nimekuwa wa kutendwa kila siku. Kuna jamaa nimezaa naye na anajulikana hadi nyumbani kwetu, lakini ghafla amebadilika, kuna siku nilimpigia simu hakupokea, baadaye akanitumia meseji akasema eti ameoa, nisimsumbue.
Naumia sana nikiona watu wengine wakipenda kwa dhati wakati mimi sina mpenzi.
Woi, Arusha.

MSOMAJI WA NANE: Nimeumia sana baada ya kufiwa na mwenzi wangu, lakini makala yako imenitia moyo na kunifariji sana. Ahsante sana na Mungu akubariki kaka yangu.
Dada (hakutaka jina lake liandikwe), Bukoba.

MSOMAJI WA TISA: Nimefurahi sana kufunga ndoa na mke wangu, baada ya misukosuko mingi. Kwangu 2010 umekuwa wa kihistoria sana.
Idd Sunzako, Mwanza.

MSOMAJI WA KUMI: Nimeishia kutendwa na wanaume kwa mwaka mzima. Kwa mwaka huu nimekuwa na wanaume watano, wote wamenitenda, hivi ninavyoandika ujumbe huu, nimetoka kuachana na boyfriend wangu baada ya kumfumania. Sina hamu na mapenzi kabisa. Najipa muda zaidi wa kujipanga!
Suzan, Lindi.

Hayo ndiyo baadhi ya mambo yaliyowatokea rafiki zetu kwa mwaka huu. Ni wengi sana wametuma, lakini nimelazimika kutoa chache kutokana na ufinyu wa nafasi.

UMEJIFUNZA NINI?
Asilimia kubwa ya walioeleza yaliyowakuta wamepata maumivu. Ni ukweli kwamba mapenzi yanaumiza sana, lakini hiyo haimaanishi ndiyo mwisho wa maisha ya kimapenzi. Bado yapo na lazima uingie, maana huwezi kuishi peke yako.

Kikubwa kwako ni kujifunza kupitia makosa na kuchukua hatua ya kuanza maisha mapya ukiwa na fikra tofauti zaidi. Achana na utumwa wa mawazo wa kuamini hakuna mwingine zaidi ya aliyepita au kuondoka duniani. Usilie sana, maana ukweli ni kwamba, hakuna wa kukufuta machozi zaidi ya wewe mwenyewe!

FUNGUA UKURASA MPYA
Badilisha staili yako ya maisha mwaka 2011, fikiri upya, fanya kila kitu kwa umakini. Acha kuwa na papara ya kuoa/kuolewa. Si kweli kila mwanaume/mwanamke utakayekutana naye ndiye utakayefunga naye ndoa.

Tuliza kichwa chako, lakini kubwa kuliko yote, huwezi kufanya haya yote kwa nguvu zako. Marafiki zangu, tumshirikishe Mungu katika kutafuta wenzi sahihi wa maisha yetu. Ukimwomba, atakupa tu!

Hongereni mliopata wenzi na kufunga nao ndoa, lakini poleni sana mlioteswa, kuumizwa na kuondokewa. Haupo peke yako...kubaliana na kilichotokea, halafu funga mkanda na uanze mwaka mpya ukiwa mpya kabisa. Bila shaka umebadilika? Siyo?! Nawapenda sana rafiki zangu.
Happy New Year!!!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love vilivyopo mitaani. Mtembelee kwenye mtandao wake;  www.shaluwanew.blogspot.com

No comments: