Tibaijuka ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Sitta ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kadhalika taarifa hiyo ya utafiti wa EIU imesema mpasuko ndani ya CCM utaendelea kuongezeka licha ya Rais Jakaya Kikwete na chama chake hicho, kuendelea kutawala siasa za Tanzania.
Iwapo utabiri wa jarida hilo ni sahihi, mabadiliko ya Baraza la Mawaziri katika Awamu ya Pili ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, yatakuwa yamechelewa ikilinganishwa na yale yaliyofanyika katika baraza lake aliloliunda baada ya kuingia madarakani mwezi Desemba mwaka 2005.
Rais Kikwete aliunda Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza Januari 2006, lakini baada ya miezi saba tu (Agosti 2006), alifanya mabadiliko makubwa yakifuatiwa na mabadiliko mengine ya Februari 2008 wakati Baraza la Mawaziri lilipovunjwa na Aprili mwaka huo alifanya mabadiliko madogo kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge aliyehusishwa na kashfa ya rada.
Lakini katika taarifa ya utafiti wake huo iliyotolewa Desemba, 2010, jarida hilo limetabiri kuwa katika mabadiliko hayo, mawziri Tibaijuka na Sitta “wanaweza kuteuliwa katika nafasi za juu zaidi” kulingana na uwezo wao wa kiutendaji na ushirikiano wao mzuri na manaibu wao.
Katika baraza lake jipya alilolitangaza Novemba 24, mwaka huu, Rais Kikwete alisema ameridhishwa na utendaji wa baraza aliloliunda mwaka 2008 na kwamba hakuona haja ya kufanya mabadiliko makubwa.
Na katika baraza hilo jipya, Rais Kikwete alionyesha dhana ya uendelevu wa Serikali yake baada ya baadhi ya mawaziri akiwamo Mustafa Mkulo (Fedha na Uchumi), Bernard Membe (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Hussein Mwinyi (Ulinzi) na William Ngeleja (Nishati na Madini) kuendelea na wizara zao.
“Yote haya yanaashiria kwamba, japokuwa uteuzi wa baraza jipya haukuwavutia wengi, inaonyesha kama kuna haja ya kulifanyia mabadiliko ndani ya miezi 18 hadi 24 ili kuimarisha Serikali, kuna uwezekano wa kutokea mambo muhimu,” ilisema sehemu ya jarida hilo.
Kikwete aliwataka mawaziri wake, kujiwekea malengo na ratiba ya kutekeleza majukumu muhimu na mazito ambayo ataona yanahitaji kupewa kipaumbele katika mwaka ujao wa bajeti.
Kadhalika jarida hilo linahusisha moja kwa moja uteuzi wa baraza la sasa la mawaziri na jitihada za Rais Kikwete kujaribu kumaliza mpasuko wa kisiasa ndani ya CCM, huku likidai kwamba kuna uwezekano wa mpasuko huo kuongezeka.
Kwa mujibu wa jarida hilo, jambo kubwa linalotazamwa hivi sasa ni kama uamuzi wa Kikwete wa kuunda Serikali yenye mwelekeo wa kuyaridhisha makundi yote ndani ya CCM utamsaidia kukikwamua chama chake katika mvutano uliopo ndani yake.
“Ni wazi kwamba katika uteuzi wake wa Baraza la Mawaziri lililotangazwa mwishoni mwa mwezi Novemba, Kikwete aliwateua aina ya watu wanaoelekea kuwa ‘watiifu kwake’ na wanaoweza kuyasoma na kutekeleza mawazo yake, hivyo mabadiliko yanaweza kutokea,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza: “Wazo kuu katika uteuzi huu linaweza kuwa ni kutekeleza mkakati mkubwa wa vita dhidi ya rushwa katika idara mbalimbali za chama”. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vita ya rushwa ndani ya CCM vinaweza kuhusishwa zaidi na wapiga kura, lakini, hatua hiyo pia inawaweka roho juu wahusika katika uchaguzi ndani ya CCM utakaofanyika kati ya 2011 na 2012.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa kuingizwa kwa Sitta katika Baraza la Mawaziri akiwa na sifa za kuwa kiongozi wa vita dhidi ya rushwa, ni ishara nyingine kwamba Kikwete alikuwa akijaribu kuweka uwiano baina ya pande zinazovutana ndani ya CCM.
Aidha, jarida hilo lilisema kuwa, kuna hoja ya msingi kwamba licha ya Chadema kuwa na nia ya kuiangusha CCM, “Ni vema Chadema kikashauriwa kukubali matokeo kwa moyo mkunjufu, lakini kitumie nafasi yake madhubuti bungeni, ili kujenga hoja za kampeni yake ya kudai katiba mpya taratibu.”
“Ikiwa Chadema itafanikiwa kufanya hivyo, kitaweza kujenga mazingira mazuri ya kuingia katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015 kwa mafanikio zaidi.”
Jarida hilo lilisema kwa kuwa Rais aliyepo madarakani anamalizia awamu yake ya pili kikatiba na anafikria zaidi katika kuunganisha na kurekebisha hali ya kisiasa ndani ya chama chake.
“Kwa kuifanya nafasi ya rais kuwa ngumu, ni wazi kwamba CCM itacheza mchezo mbaya wa kisiasa dhidi ya Chadema ndani ya miezi 12 hadi18 ijayo, jambo ambalo ni hatari kwa chama hicho pinzani,” lilionya jarida hilo.
Kwa mujibu wa jarida hilo, historia inaweza ikawa onyo tosha kwa Chadema, kwa kuangalia vyama vingine vya upinzani ambavyo viliwahi kuvuma katika chaguzi zilizopita nchini Tanzania.
“Ni vigumu kwa chama kupata ushindi ikiwa kitasimama peke yake katika uchaguzi kutokana na CCM kuendelea kushika madaraka, leo hakuna hata chama kimoja kilichoweza kudumu katika nguvu na lengo lake.”
Pamoja na mambo mengine, jarida hilo limechambua masuala mbalimbali ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na mfumko wa bei, hali ya uchumi wa taifa, sera za kiuchumi, uhusiano wa kimataifa, namna uchaguzi ulivyofanyika na hali ya kisiasa nchini Tanzania.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment