Wachezaji wa timu ya soka ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' wakishangilia ubingwa wa kombe wa Chalenji baada ya kuifunga Ivory Coast bao 1-0 katika mchezo wa fainali kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. (Picha
na Fadhili Akida).
TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars jana ilimaliza ukame wa kukaa miaka 16 bila kupata Kombe la Chalenji baada ya kutwaa ubingwa huo kwa kuifunga Ivory Coast kwa bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mara ya mwisho Kilimanjaro Stars ilitwaa Kombe hilo mwaka 1994 ikiwa chini ya Kocha Sylersaid Mziray (marehemu) akisaidiwa na Sunday Kayuni ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Kabla ya hapo Stars iliwahi kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza mwaka 1974.
Aliyelirudisha Kombe hilo kwenye ardhi ya Tanzania baada ya miaka 16 ni nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa aliyefunga bao kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 41.
Penati hiyo ilitolewa na mwamuzi Bamlak Tessama wa Ethiopia baada ya mchezaji N’goran Kouassi wa Ivory Coast kuunawa mpira eneo la hatari.
Nsajigwa alipiga penati hiyo kwa ustadi, akipiga shuti lililokwenda upande wa kushoto mwa nyavu za wapinzani huku kipa wa Ivory Coast, Sangare Badra Ali akienda kulia.
Hata hivyo katika kipindi cha pili timu zilishambuliana kwa zamu na kuna wakati Stars ilionekana kuelemewa kwani ilikuwa ikiruhusu mashambulizi ya mara kwa mara katika lango lake, kitu ambacho hata kocha wa Kili Stars Jan Poulsen alikiri na kuongeza kwamba pamoja na ushindi lakini wapinzani wao walionesha soka safi na kuwazidi kiwango.
Michuano ya mwaka huu imemalizika kwa neema kubwa kwani mbali na kutwaa ubingwa, Nsajigwa amepata tuzo ya mchezaji bora wa michuano hii iliyotumia takriban wiki mbili huku Juma Kaseja akipata tuzo ya kipa bora baada ya kuruhusu kufungwa bao moja ambalo lilikuwa katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Zambia ambapo Stars ilifungwa bao 1-0.
Mfungaji bora wa michuano hiyo ni Felix Sunzu wa Zambia aliyefunga mabao matano na timu yenye nidhamu ni Somalia.
Kwa ushindi huo, Kilimanjaro Stars imepata dola za Marekani 30,000 huku Ivory Coast ikipata Dola za Marekani 20,000 na Uganda iliyoshika nafasi ya tatu ikipata dola 10,000.
Uganda iliyotwaa ubingwa mara mbili mfululizo mwaka juzi na mwaka jana ilitema Kombe baada ya kufungwa na Kilimanjaro Stars katika mechi ya nusu fainali kwa mikwaju ya penati 4-3, na hivyo ‘kuangukia’ nafasi ya tatu baada ya jana kuifunga Ethiopia mabao 4-3.
Kilimanjaro Stars jana si tu iliweka historia ya kutwaa ubingwa huo baada ya miaka 15, lakini pia imeweka historia kwa uongozi wa soka nchini TFF kutwaa taji la kwanza tangu kuingia madarakani takriban miaka mitano iliyopita.
Aidha, Kocha Poulsen raia wa Denmark amekuwa mwenye bahati kwa kutwaa ubingwa miezi minne tu tangu kuiongoza timu, hali inayowapa matumaini Watanzania kwamba huenda mambo mazuri yanakuja siku za usoni.
Poulsen alichukua nafasi ya Mbrazili Marcio Maximo Agosti mwaka huu aliyeiongoza Tanzania kwa miaka mitatu na kwa kipindi chote alichokuwa nchini hajaipatia Kilimanjaro Stars ubingwa.
Mwaka jana ilishika nafasi ya nne chini yake baada ya kufungwa na Zambia kwenye Uwanja wa Nyayo Nairobi, Kenya.
Kilimanjaro Stars: Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Idrissa Rajab/Kigi Makasi/Ramadhani Shamte, Kelvin Yondani, Jabir Aziz, Shaaban Nditi, John Bocco/ Henri Joseph, Nurdin Bakari, Stefano Mwasika, Salum Machaku na Juma Nyosso.
CHANZO:HABARI LEO |
No comments:
Post a Comment