Thursday, December 16, 2010
Kwaheri rafiki Dk. Remmy
Na Rhobi Chacha
MWANAMZIKI mkongwe aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii, Ramazani Mtoro Ongala ‘Dk. Remmy’ (pichani) anatarajiwa kuagwa na kuzikwa leo katika makaburi ya Sinza, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili juzi nyumbani kwa marehemu, Sinza kwa Remmy, mjomba wake, mzee Kitu Nzingu Makassy alisema taratibu za mazishi zinaendelea ambapo gwiji huyo atazikwa katika makaburi ya Sinza.
“Tumeamua kumzika Sinza, kwa kuwa enzi za uhai wake alikuwa akiamini kuwa yeye ni mnyonge na makaburi hayo ni ya wanyonge tena yapo karibu na nyumbani kwake,” alisema.
Aliongeza kusema kwamba, mazishi yamechelewa kufanyika kutokana na kuwasubiri watoto wa marehemu ambao wapo London, Uingereza na Dubai, Arabuni pamoja na ndugu wengine kutoka Kivu, Kongo (DRC).
Naye mke wa marehemu ambaye ni Mwingereza, Tony Ongala alipohojiwa na mwandishi wetu alishindwa kuficha hisia za majonzi juu ya msiba huo.
“Nusu ya maisha yangu nimeishi na yeye, sasa ameondoka, nitaishije,” alisema kauli iliyowafanya baadhi ya wanawake waliokuwa pamoja naye kutokwa na machozi.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Mr.11’ au Sugu akimzungumzia Dk. Remmy alisema, tunu ya taifa imepotea kwa sababu aliitangaza nchi kimataifa.
“Nilishangaa kuona taifa lilichelewa sana kumpa hati ya kusafiria, alipewa akiwa na umri mkubwa lakini angepewa mapema angefanya makubwa kwa sababu alikuwa akihudhuria matamasha makubwa waliyokuwa wakishiriki wanamuziki wenye majina duniani.”
Naye rafiki wa karibu wa marehemu, Cosmas Chidumule alisema Dk. Remmy alikuwa mtu wa ajabu kwa sababu alikuwa msanii mbunifu.
“Siku moja aliwahi kupanda juu ya mnazi pale Magomeni akiwa na microphone (kipaza sauti) akawa anaimba, ulikuwa ni ubunifu mkubwa,” alisema Chidumule.
Dk. Remmy, aliingia nchini Tanzania mwaka 1978. Kwa mujibu wa maelezo yake aliletwa hapa nchini na mwanamuziki mwingine maarufu mwenye asili ya Kikongo, Mzee Makassy ambaye kama ilivyokuwa kwa Dk Remmy, ameacha muziki wa dansi na kuwa Mlokole anayeimba nyimbo za dini za Kikristo pekee.
Dk. Remmy hakuwa na siri, kwani alitoboa kuwa aliishia darasa la tano baada ya wazazi wake kufariki dunia akiwa na umri wa miaka nane (8) tu na mama yeke naye akafariki miaka sita baadaye wakati akiwa na umri wa miaka 14, na hapo ndipo aliposhindwa kuendelea na shule.
Alisema baada ya hapo alichukuliwa na baba yake mdogo, ambapo aliishi maisha ya kunyanyaswa ambayo hatimaye yalimfanya akimbilie mitaani na kuwa ombaomba.
“Baba yangu mdogo alikuwa akiniacha nyumbani, akirudi akikuta paka amekula mboga naambiwa ni mimi. Siku nyingine naenda kuchunga, ngedere wanakula mahindi, naambiwa ni mimi,” aliwahi kusema Dk. Remmy, matukio ambayo aliyatungia nyimbo.
Nyimbo nyingi alizoimba mwanamuziki huyo zinanukuu Maandiko Matakatifu yaani Biblia.
Dk. Remmy ameacha mke na watoto watano ambao ni Kally, Jesca, Aziza, Shema na Thomas pamoja na wajukuu wanne.
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake