Thursday, December 16, 2010

Mlianzana kwa ‘I love you’, vipi muachane kwa matusi?

UTAKUMBUKA wiki iliyopita niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘NI SAHIHI KUANZISHA UHUSIANO NA ALIYEKUWA MPENZI WA RAFIKI YAKO?’ Makala hii imeonekana kuwagusa watu wengi sana na hata pale nilipotoa fursa kwa watu kuchangia juu ya mada hii, nilipokea ‘sms’ na simu nyingi sana kutoka kwa wasomaji wangu.


Asilimia kubwa ya waliochangia juu ya mada hiyo walieleza kuwa, hakuna tatizo endapo mtu ataanzisha uhusiano na aliyekuwa mpenzi wa rafiki yake. Hata hivyo, walichokisema ni kwamba, hilo halitakuwa na shida endapo tu kutakuwa na uthibitisho kwamba, uhusiano wa rafiki yako na mpenzi wake ulishakufa na ameonesha wazi kutokuwa na mapenzi naye tena.

Wakasema kuwa, hata kama kutakuwa na mazingira fulani ya rafiki yako kutaka kujenga uadui na wewe kwasababu ya kumchukua aliyekuwa mpenzi wake, hilo wala lisikuumize endapo tu utabaini una mapenzi ya dhati naye na dhamira yako si kumchezea bali kuingia naye katika maisha ya ndoa.

Kwa maelezo hayo nihitimishe makala hiyo ya wiki iliyopita kwa kusema kwamba, hakuna tatizo lolote kwako kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa mpenzi wa rafiki yako endapo utazingatia yale ambayo nimeyaeleza hapo mwanzo. 

Baada ya kusema hayo sasa nirudi kwenye mada yangu ambayo nimekuandalia kwa wiki hii. Nazungumzia suala la wapenzi kuachana kwa staili ya kutukanana na nyodo. Katika maisha yetu ya kila siku tumekuwa tukishuhudia wapenzi waliotokea kupendana sana wakiachana tena wakati mwingine katika mazingira yasiyofaa.

Unakuta wawili ambao huko nyuma walikuwa wakipendana na kufikia hatua ya watu kuwaonea gere, leo hii kwa sababu tu mwisho wa kupendana kwao umefika, wanaachana kwa shari kana kwamba walichokuwa wakifanya walikuwa wakiigiza tu, jambo ambalo kwa kweli halileti picha nzuri.

Hebu jaribu kukumbuka mambo mazuri mliyokuwa mnafanyiana enzi mnaanza uhusiano wenu, kumbuka maneno matamu mliyokuwa mnatamkiana mlipokuwa faragha, kumbuka ahadi nzuri mlizokuwa mkipeana huko nyuma, sasa iweje leo muachane kwa kurushiana maneno machafu?

Sawa, penzi lenu limefika mwisho na hamuoni sababu ya kuendelea kuwa pamoja lakini sasa, unadhani ni busara kuachana kishari? Mtafaidika nini sasa kwa kuachana kwa staili hiyo? Mimi nadhani kuachana kupo lakini mnapohisi penzi lenu limefika mwisho, bora muachane kwa amani.

Hicho ndicho nilichotaka kukueleza kwa siku ya leo lakini naomba niseme jambo moja kwamba, ili kuepuka kuja kuachana na mpenzi wako kishari ni vema ukamsoma mapema mwenendo wake na pale utakapobaini hana mapenzi ya kweli kwako, chukua uamuzi wa kumuacha mapema ili
kuepuka kuja kuumia. 

Wataalamu wa masuala ya mapenzi na uhusiano wanaeleza kuwa, unapokuwa katika uhusiano na mtu uliyetokea kumpenda, usimkabidhi moyo wako wote kwanza. Chukua muda wa kuchunguza ili kubaini kama na yeye pia anakupenda kwa dhati kabla ya kumzimia moja kwa moja.

Endapo utaona moyo wako unasita kuwa na mtu huyo na kuhisi hana penzi la kweli, ni vizuri bila kujali jinsi utakavyoumia ukamuacha haraka kabla ya yeye hajakuacha.

Kumuacha kwako kutakufanya uwe na amani moyoni mwako kwani utakuwa umejiandaa kumkosa mwenyewe kuliko yeye kuja kukuacha ghafla tena kwa nyodo au kukutukana.

Kimsingi hutakiwi kulilea penzi lisilokuwa na mwelekeo, usikubali kulizwa, unapoona nyendo za mpenzi wako hazikuridhishi, chukua uamuzi wa haraka wa kumuacha kwa amani huku ukiamini kwamba utampata mwingine.

Unapobaini kwamba huyo uliyenaye hana mapenzi ya dhati na wewe, jiandae kumkosa mapema na ikiwezekana uanze wewe kuusitisha uhusiano wenu kwa njia ambayo ni ya amani. 

Kuna njia mbalimbali ambazo zinashauriwa kutumiwa wakati wa wapenzi kuachana lakini leo nataka kuzungumzia njia moja ambayo ni ile ya kumtumia mpenzi wako ujumbe wa maneno. Maneno haya ni lazima yawe yameandikwa kiubunifu zaidi na kueleza hisia zako wakati wa kutimiza azma yako hiyo.

Yapo maneno ambayo ukimuandikia mpenzi wako wakati unamuacha hakika yatamuumiza sana na ataamini wewe kwa upande wako ulikuwa na mapenzi ya dhati kwake lakini yeye ndiye amekuwa tapeli. Maneno hayo yatamfanya asikusahau katika maisha yake hata kama hamtakuwa pamoja.

Mwambie maneno haya: “Nahisi sina nafasi kwenye moyo wako mpenzi, nilikupenda sana nikiamini tungeweza kuwa pamoja mpaka mwisho wa maisha yetu lakini haya unayonifanyia sasa, inaonesha huna mapenzi ya dhati kwangu.

“Naumia kukukosa lakini nahisi sina jinsi, nimevumilia mengi, nilijitahidi kukuonesha upendo wangu wa dhati lakini ulidiriki kulipiga teke penzi langu. Naona bora nikuache uendelee na maisha yako, naamini Mungu hakupanga tufike mbali, nakushukuru kwa kila jema ulilonifanyia na nakutakia maisha mema.”

Haya ni maneno makali sana ambayo unaweza kumtumia mpenzi wako wakati unamuacha. Hii itakufanya uonekane mwenye busara na kwamba upendo wako kwake haukuwa wa kinafiki wala wa kujifanyisha bali ulikuwa ukitoka moyoni.

Hiyo ndiyo njia nzuri ya kumuacha mpenzi wako badala ya kutumia maneno ya kumtukana na kumkashifu, huwezi kujua Mungu kakuepusha na nini na amekupangia nini baada ya kuachana na huyo uliyekuwa naye.

Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa makala nyingine motomoto.uyy

1 comment:

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake