Rhobi Chacha na Musa Mateja
Mazishi ya galacha wa muziki wa dansi nchini, hayati Ramazani Mtoro Ongala ‘Dk. Remmy’ ni ya kihistoria, Ijumaa lina tathmini ya jumla.
Mtikisiko wa Jiji la Dar es Salaam, ukimya wa eneo la Sinza, vituo vya redio kupiga nyimbo zake mfululizo na mengineyo kuhusu kifo cha Dk. Remmy ni historia inayohitimisha enzi ya muasisi huyo wa mtindo wa Bongo Beats.
Dk. Remmy, alizikwa jana majira ya saa 10:00 alasiri, Sinza Makaburini, Dar kwa heshima kubwa.
Awali, shughuli ya kuuaga mwili wake ilifanyika kwenye Viwanja vya Biafra, Kinondoni, jijini.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Waziri wa Habari Vijana na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika pamoja na wasanii mbalimbali.
Katika kuufanya msiba huo kuwa wa aina yake, baadhi ya wanamuziki walirekodi nyimbo za kuomboleza kifo chake, ikiwa ni ishara ya kumuenzi.
Baadhi ya nyimbo hizo, zimekuwa zikichezwa nyumbani kwa marehemu, Sinza, Kwaremi, Dar palipo na msiba wa nyota huyo wa wimbo wa ‘Kifo’.
Watu waliofika msibani kwa Dk. Remmy, walipata fursa ya kusikiliza nyimbo za Injili hususan zile zilizoimbwa na marehemu lakini zaidi kulikuwa na sebene lililoporomoshwa.
Katika baa nyingi hasa zile zilizopo kando ya Barabara ya Shekilango, Dar, wateja wake wengi walitumia muda wao kumjadili Remmy, ushujaa wake kwenye muziki mpaka kifo kilipomchukua.
Tathmini ya jumla ya Ijumaa, ina jibu lililonyooka kuwa nyimbo za Dk. Remmy na mtindo wake wa maisha, uliwaingia wengi hasa wale waliokua miaka ya 1980 na mwanzoni mwaka 1990.
Gazeti hili limebaini kuwa ujumbe unaopatikana kwenye nyimbo za Dk. Remmy, ni kichocheo cha Watanzania wengi kumbeba mwimbaji huyo wa wimbo ‘Kwa Yesu Kuna Furaha’ kama kioo chao.
Ijumaa lilifanya mahojiano na wakazi mbalimbali wa Sinza ambao maoni yao yapo kama ifuatavyo;
“Remmy alikuwa anajua anachokifanya, mfano wimbo wa Kifo, hauwezi kuchuja, kizazi na kizazi kitaendelea kuusikiliza na kupata burudani na ujumbe.
“Kuna wimbo wa Mambo kwa Soksi, alivyoutoa ilionekana uhuni, hadi ukapigwa marufuku redioni, lakini leo hii zipo asasi nyingi za kupambana na Ukimwi zinahamasisha matumizi ya kondomu.
“Hapo ni wazi utaona Dk. Remmy aliona mbali, lile lilikuwa jembe bwana!” Alisema Issa Salum, mkazi wa Tandale, Dar aliyekuwepo msibani.
Salum aliongeza: “Dk. hakuwa na ubaguzi, ndiyo maana umeona watu wengi wamejitokeza kumzika, si Wakongo wala Watanzania, kiukweli alikuwa kipenzi cha wengi.”
Katika hatua nyingine, wadau mbalimbali walisikika wakisema kwamba ili kumuenzi, makaburi ya Sinza, ambapo ndipo alipozikwa yabadilishwe jina na kuitwa Makuburi ya Dk. Remmy.
“Tena eneo lote la Sinza Makaburini liitwe Kwa Remmy, hii itakuwa njia mojawapo ya kumuenzi,” alisema mdau mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Tuesday Hamisi mkazi wa Kinondoni Moscow, Dar.
Dk. Remmy alifariki dunia Desemba 13, 2010 (Jumatatu) saa nane usiku katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam, kwa maradhi ya kisukari na figo.
Aliingia nchini akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (iliyokuwa ikiitwa Zaire) mwaka 1978 na kujiunga na Bendi ya Orchestra Makassy, baadaye Orchestra Matimila (Wana Talakaka) aliyoigeuza na kuiita Super Matimila.
Alitunga nyimbo nyingi zilizompa umaarufu mkubwa, miongoni mwa hizo ni Siku ya Kifo, Mariam Wangu, Muziki Asili Yake Wapi, Kilio cha Samaki, Hamisa, Kifo, Mambo kwa Soksi, Kwa Yesu Kuna Furaha (baada ya kuokoka) na nyingine nyingi.
Ameacha mjane Toni Ongala raia wa Uingereza na watoto kadhaa wakiwemo Kalimangonga ‘Kally’ Ongala msakata kabumbu katika Timu ya Azam FC na Jessica Ongala ambaye aliwahi kuwa mnenguaji kabla ya kutimkia Uarabuni.
Mungu ailaze roho ya Dk. Remmy Ongala mahali pema peponi, Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. – Amen.
No comments:
Post a Comment