Friday, December 24, 2010

Mume akataa maiti ya mkewe

UMATI wa wanakijiji wa Kijiji cha Borenga, Kata ya Kisaka wilayani Serengeti, Mara, jana ulishuhudia jambo adimu kutokea katika jamii, baada ya Mzee Maro Hagare kukataa kuupokea mwili wa mke wake, Rhobi Maro (58) akidai kuupokea na kuuhifadhi ndani ya nyumba yake ni sawa na kujitia mkosi.
 

Mzee Hagare anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 65, alisisitiza msimamo wake huo kwa kuanza ujenzi wa nyumba huku maiti ikiwa kwenye gari, akisema ni bora mwili wa mkewe huyo uhifadhiwe humo kuliko kuupokea na kuuhifadhi katika moja ya nyumba zake mbili wanazoishi wake zake wawili. 

Uamuzi huo uliibua mzozo mkali baina ya mzee huyo na wanandugu wa marehemu, lakini Mzee Hagare alitia `pamba’ masikio yake, huku akitafuta mafundi na kuanza ujenzi wa nyumba ya vyumba vinne inayojengwa kwa tofali za kuchoma. 

Hadi tunakwenda mitamboni, ujenzi wa nyumba hiyo ulikuwa umefikia `kozi’ ya 11, lakini tayari mwili ulikuwa umehifadhiwa ndani ya jengo hilo hilo huku mafundi wakiendelea na ujenzi. 

Hali ya mzozo ulianza mchana baada ya kuwasili kwa mwili wa marehemu aliyefariki siku nne zilizopita mkoani Morogoro na baadaye mwili wake kurudishwa kijijini Borenga kwa ajili ya mazishi. 

Mara baada ya mwili kufikishwa kwa mume wa marehemu, Mzee Hagare huku akivua shati lake mbele ya waombolezaji, alisema hayuko tayari kuipokea maiti ya mkewe huyo kwa madai kuwa hakuna nyumba ya kuilaza maiti hiyo kwa madai kuwa nyumba alizonazo ni za wake wawili tu. 

“Nimesema mwili huu haushuki hapa, mpelekeni huko alikotaka kuzikwa yeye mwenyewe na niko tayari kufanywa lolote, ama ninaendelea na ujenzi wa nyumba hii ya matofali ili maiti yake iingie hapa mara baada ya nyumba kumalizika kujengwa,” alisema mzee huyo huku maiti ikiwa kwenye gari aina ya Toyota Double Coaster lenye namba za usajili T 937 BFR lililousafirisha mwili wa marehemu kutoka Morogoro. 

Wakati akiyasema hayo ujenzi wa nyumba ya vyumba viwili vya awali ulikuwa unaendelea na maiti iliendelea kukaa kwenye gari na haikuweza kushushwa kwa madai kuwa hakustahili kuipokea nyumbani kwake. 

“Nimesema mumshushe mpelekeni kule kwenye pori la miti alikoomba yeye mwenyewe azikwe, lakini mimi nasema siwezi kumpokea hata mngenifanyaje,” alisema kwa hasira mzee huyo huku akionekana kujiandaa kwa chochote kitakachokuwa tayari. 

Kwa mujibu wa taratibu na mila za kabila la Wangoreme, ili maiti ya mke wa mume huyo izikwe sharti maiti hiyo ilazwe ndani ya nyumba ya mumewe kama uthibitisho wa yeye kumkubali mkewe huyo, lakini kilichotokea hapa kilikuwa ni tofauti kutokana na kile kinachoelezwa kutokuwapo kwa maelewano kwa muda mrefu baina ya mzee huyo na marehemu mkewe aliyekuwa amekwenda kwa mwanawe Morogoro. 

Mara baada ya kauli hiyo ya Hagare aliyoitoa kuwa hayuko tayari kuipokea maiti ya mkewe huyo, wadogo wa kiume wa marehemu Mwita Maro na Duncan Ikonyo walisema kuwa kama yeye (mume) anaona ni shida kuuchukua mwili wa mkewe na kuuzika ni bora wakabidhiwe wao ili waende kuuzika. 

“Tunachosema kama yeye anaona kuwa dada yetu hamtaki, aturuhusu sisi tumchukue tukamzike maana sehemu ya kumzika hatujakosa, bado tunampenda katika roho, tunaomba tupe mwili wa dada yetu, tupe mwili wa dada yetu yeye hajatushinda na tutamzika,” alisema Duncan Maro kwa masikitiko. 

Ndipo baadaye mume wa marehemu Maro Hagare alisema kuwa yeye hayuko tayari kuukubali upuuzi wowote atakaoelezwa na mtu yeyote yule na kwamba msimamo wake ni uleule wa kukamilisha ujenzi wa nyumba. 

“Nasema siko tayari kuukubali upuuzi wowote utakaoletwa kwangu hapa, nimesema sitaki maiti hii ishushwe kwangu, subirini nyumba yake ikamilike kujengwa ndipo niishushe, la sivyo muipeleke kule kwenye miti alikoomba yeye mwenyewe enzi ya uhai wake azikwe,” aliongeza. 

Mara baada ya maneno yake hayo, dada wa marehemu Mariam Chacha na Nyamahemba Omary huku wakilia kwa uchungu walimfuata Mzee huyo na kumueleza kuwa wako tayari kuuliwa nao ili mradi maiti ya marehemu dada yao ishushwe kutoka kwenye gari ili iweze kuzikwa. 

“Tuko tayari utuue tunasema tuue, tuuuuuuue…, unamkataa dada yetu kwa sababu tu sasa ni marehemu, hivi wewe ni nani katika kijiji hiki, tunasema tuue,” alisema Mariamu kwa uchungu na kuongeza; 

“Unamuona sasa hivi amekuwa ni kinyago na kwamba hastahili sasa kuitwa mke, nasema hivi leo mpaka kitaeleweka,” alisema Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kobesisi Yohana James alisema kuwa binafsi ameushuhudia mgogoro huo na kusema kuwa ni mgogoro wa aina yake wa vijana na baba yao kulumbana ni wapi pa kuzikwa marehemu huyo, lakini alisema kuwa ni imani yake kuwa ufumbuzi wa jambo hilo lingepatikana si baada ya muda mrefu. 

“Nimeshuhudia mgogoro huu ambao hapa kwetu ni wa kihistoria, na ni wapi azikwe familia bado haijakubaliana ila wamekubaliana kuushusha mwili huo wa marehemu kutoka kwenye gari na kuulaza katika banda la nyumba inayojengwa sasa ili taratibu za mazishi ziandaliwe kwa kesho, na sina uhakika kama mwili huo utazikwa maana naona mgogoro huu ni mkubwa,” alisema James. 

Alisema kuwa, kwa historia ya mkasa huo, serikali yake itaendelea kuwashauri wazazi na vijana wafikie muafaka ili waweze kumzika marehemu huyo ambaye hadi jana alikuwa amefikisha siku nne kabla hajazikwa. 

“Bado tunaendelea kuwasihi wazazi wa pande zote mbili wafikie uamuzi muafaka wa kufanya mazishi, maana endapo mgogoro ukiendelea unaweza ukaleta maafa kwa pande zote mbili, na niwaombe ndugu jamaa wa marehemu waache ushabiki bali watafute muafaka wa jambo hili ili maiti iweze kuzikwa,” aliongeza James. 

Aidha Mwenyekiti huyo wa mtaa alitumia fursa hiyo kuwaomba wawe na subira wasubiri maafikiano ya pande zote ili kuwezesha mwili wa marehemu uweze kuzikwa kwa amani na utulivu. 

Hadi gazeti hili linaondoka eneo la mazishi, hakukua na mwafaka, zaidi yam zee mfiwa kuendelea kusimamia ujenzi, huku mvua kubwa ikinyesha na kuwafanya waombolezaji kuondoka msibani na kwenda kujihifadhi katika nyumba za majirani. 

Wakati waombolezaji wakitawanyika, Mzee Hagare alibaki na jeneza la marehemu katika moja ya vyumba vya nyumba inayoendelea kujengwa. 

Marehemu aliacha mume na watoto wanane, wa kiume watatu na wa kike watano.


                                            CHANZO:HABARI LEO

2 comments:

  1. Huyu mzee ni katili sana..inabidi atubu kwa kweli yaani amefanya unyama huu wakati ajui kesho litampata lipi na uwenda akakimbilia upande huo wa marehemu kuomba msaada...amenisikitisha sana.na kwanini asichukuliwe hatua,sasa hiyo mvua ilivyokuwa inanyesha si huyo maiti kanyeshewa jamani,japo huo ni mwili tu lkn unahitaji heshima yake ya mwisho hapa duniani,kwa kweli inauma sana,poleni sana ndugu wa marehemu pamoja na watoto,Mungu awatie nguvu na awafariji katika kipindi hiki kigumu.Ameeeeeen!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. Duniani kweli kuna mambo. Huyo bwana anastahili adhabu kali ya kijiji au kutengwakabisa. lazima atubu kwa familia ya mkewe kuukosea mwili wa marehemu heshima mbele ya ndugu zake; jamani pamoja na marehemeu kumzalia watoto nane jamani...kweli huyo baba naamini ni kichaa sio mtu wa kawaida. mwenyezi mungu awatie nguvu ndugu na watoto wa marehemu na mwenyezi mungu aipumzishe roho ya marehemu mahala pema peponi. amen

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake