Hassan Mohamed
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, amezitaka kampuni binafsi zinazotoa huduma ya zimamoto, kutoa huduma kwanza kabla ya gharama, ili kunusuru maisha ya watu na mali zao.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika makao makuu ya Idara ya Majanga na Moto, jijini Dar es Salaam jana, Nahodha alisema kitendo cha kampuni hizo kukataa kutoa huduma, ili kwanza zilipwe gharama, kinazorotesha utoaji wa huduma kwa wakati.
"Nimepata malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa kampuni hizi zinataka kufanyika kwa maelewano ya gharama kabla ya kuzima moto. Hivi kwa nini kwanza kazi isifanywe ili kuokoa maisha ya watu na mali zao na baadaye maelewano kuhusu gharama,"alihoji Nahodha.
Waziri huyo pia aliitaka idara hiyo, kupitia upya usajili wa kampuni hizo ili kujua uwezo wao katika kukabiliana na matukio ya moto.
Kuhusu gharama za huduma, waziri Nahodha aliagiza zipitiwe upya ili kuwawezesha wananchi wa vipato vya chini, kupata huduma bila usumbufu, kama ilivyo sasa.
"Sisemi kampuni hizo zisitoze pesa, lakini zisitumie shida za wananchi kupata faida,"alisisitiza Nahodha.
Pia aliitaka idara, kuhakikisha kuwa inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa ili kujenga uwezo utakaowashawishi wananchi, kulipa gharama za huduma za zimamoto na kuwa na imani na huduma zitolewazo.
Aliongeza kuwa elimu kuhusu matumizi ya vifaa vya kupambana na majanga ya moto, lazima ipewe kipaumbele.
"Vifaa vya kuzimia moto vinaweza kuwepo lakini moto unapozuka watu hukimbia, wananchi wapewe elimu ya kuvitumia vifaa hivi ili waweze kudhibiti moto kabla haujawa mkubwa," aliagiza Nahodha.
Katika hatua nyingine, Nahodha aliitaka idara hiyo, kumuajiri kijana aliyejitoa muhanga kwa kutumbukia kwenye bwawa la maji machafu jijini Dar es Salaam na kuokoa maisha ya mtoto aliyekuwa akizama wakati wafanyakazi wa idara hiyo wakishindwa kutoa msaada.
"Nafahamu kuwa kuna taratibu za kutoa ajira, lakini yule kijana anapaswa kupewa zawadi kwa kipaji na ujasiri wake na zawadi inayomfaa ni kumuajiri ili aweze kuonyesha kipaji chake," alisema Nahodha.
Mapema, Kamishna wa Idara ya Majanga na Moto, Ragatus Kipali, alitaja changamoto zinazoikabili kuwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, kutotekelezwa kwa mafunzo na udhaifu wa miundombinu.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment