Boniface Meena
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limesema lina mpango wa kuvunya nyumba maeneo muhimu na kujenga majengo mengi zaidi ya ghorofa, zikiwa ni jitihada za kupunguza tatizo la makazi.
Maeneo ambayo yatahusika na ubomoaji huo ni Upanga na Ubungo jijini Dar es Salaam, lakini wapangaji kwenye nyumba hizo watatafutiwa maeneo mengine kabla ya uvunjaji.
Kutokana na mpango huo, NHC imeonya wananchi kununua nyumba za shirika hilo bila kufuata taratibu.
Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Umma na Huduma za Jamii, Susan Omari, alisema nyumba zitakazojengwa, zitauzwa kwa wananchi.
"Mipango ya ujenzi wa mradi huu tayari umeshakamilika na utaanza rasmi mwakani. Wananchi wote watafahamishwa wakati shirika litakapoanza utekelezaji miradi hii ili wale watakaotaka kununua wafuate taratibu zitakazowekwa za ununuzi," alisema Omari.
Alisema NHC itauza nyumba kwenye maeneo machache, ambayo gharama zake haziongezi tija na hazina manufaa kwa shirika.
"Wananchi watafahamishwa kwa kutumia vyombo vya habari kuhusu maeneo ambako nyumba zitauzwa kwa muda muafaka, ambao utawezesha wale wanaotaka kununua nyumba hizo kujiandaa," alisema.
Omari alisema shirika hilo linaendelea kukusanya madeni na wale ambao hawajalipa hadi sasa, watambue kuwa ifikapo Februari 28, mwakani wataondolewa.
Alisema kuna wapangaji ambao ni sugu, hasa mashirika ya umma na wizara ambazo madeni ya pango yamekuwa makubwa.
"Tunafahamu kuwa kila mwaka wa fedha taasisi zote za umma zinaweka kipengele cha kodi ya pango kwenye bajeti zao, lakini cha kusikitisha ni kwamba hayalipi kodi kwa wakati," alisema.
Alisema shirika limetoa notisi kwa wadaiwa wote, zikiwamo taasisi za umma na hatua mahususi zitachukuliwa iwapo watashindwa kulipa kwa wakati.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment