ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 21, 2010

SEMHANDO NDIYE ALIYENUNUA SANDA YA DK. REMMY

Abou Ally Semhando (kulia) akiwa na Dk. Remmy Ongala (kushoto) enzi za ujana wao.
Brighton Masalu na Musa Mateja
Usiku wa kuamkia Jumamosi, Desemba 18, 2010  ulikuwa wa majonzi kwa wapenzi wa burudani Bongo, hususan wadau wa muziki wa dansi baada ya taarifa za kifo cha aliyekuwa mpiga ‘drum’ na Meneja wa Bendi ya African Stars International ‘Twanga Pepeta’, Abou Ally Semhando (57), (pichani kushoto) ikiwa ni saa 34 tangu mazishi ya mkongwe Ramazan Ongala ‘Dk. Remmy’ yafanyike.

Kifo cha Semhando kilichosababishwa na ajali ya kugongwa na gari wakati akiendesha pikipiki eneo la Tangi Bovu, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kimekuja wakati ambao bado Watanzania walikuwa wakiomboleza kifo cha Dk. Remmy. Mwisho wa enzi za wakongwe hawa wawili ni wa kusisimua, na kuna maswali mengi ambayo bado hayana majibu.

KIFO CHA SEMHANDO KILIVYOTOKEA
Saa 8:20 usiku, Semhando alikuwa anaendesha pikipiki akitokea Africana, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam alipopata ajali ya kugongwa na gari dogo aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili T855 BLQ, eneo la Tangi Bovu, Dar na kupoteza maisha. Mwili wake uliondolewa eneo la tukio dakika 90 baadaye na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ulikohifadhiwa.
Abou Ally Semhando enzi za uhai wake.
UHUSIANO NA KIFO CHA DK. REMMY
Semhando, kabla hajapatwa na mauti alishiriki kikamilifu katika mazishi ya Dk. Remmy ambapo inaelezwa kuwa ndiye aliyetoa fedha za kununulia sanda iliyotumika kuuhifadhi mwili wa marehemu kabla ya mazishi. Akiwa msibani hapo, Semhando alionekana kuguswa sana na kifo cha Dk. Remmy ambapo muda mwingi alikuwa mwenye majonzi na masikitiko.

Hata wakati wa kuupeleka mwili wa marehemu Dk. Remmy makaburini, Semhando ndiye aliyekuwa mbele ya msafara wa waombolezaji na pikipiki yake.
Enzi za uhai wao, Semhando na Dk. Remmy walifanya kazi pamoja katika Bendi ya Matimila, iliyokuwa na makao makuu yake mjini Songea, inaelezwa kuwa hiyo ndiyo sababu kubwa iliyowaweka karibu wakongwe hao.

ALIJITABIRIA KIFO CHAKE
Watu wa karibu na marehemu Semhando, wanasema kuwa siku za mwisho za uhai wake alikuwa ni kama mtu anayetambua nini kilikuwa  mbele yake kwani alifanya mambo mengi ambayo hapo awali hakuwahi kuyafanya. Inaelezwa kwamba Semhando aliomba likizo ndefu isiyo na malipo kwa uongozi wa
Twanga Pepeta, kitu ambacho hakuwahi kukifanya hapo awali.
Dk. Remmy enzi za uhai wake.
Siku ya tukio, wakiwa ukumbini Africana, Semhando aliimba wimbo mmoja tu wa Mwana Dar es Salaam na kwenda kukaa pembeni kwa madai kuwa hakuwa anajisikia vizuri. Hata muda wa kuondoka, aliwahi kabla ya shoo haijaisha na kuagana na wanamuziki wenzake wa bendi hiyo. Muda mfupi baadaye ndipo alipokumbwa na mauti.

Marehemu ameacha mjane na watoto 12. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amen.

CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS

No comments: