Phinias Bashaya, Missenyi
SERIKALI mkoani Kagera imewataka Watanzania kuwa macho na ugonjwa wa kutisha uliozikumba nchi jirani za Uganda na Sudan unaofanana dalili zake kama ule wa Ebola.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Issa Njiku mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na baraza jipya la madiwani na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kuwa macho na wageni wanaopitia kwenye mipaka ya wilaya hiyo.
Dalili za ugonjwa wa ebola ni pamoja na kuumwa kichwa, kutapika damu, kuharisha na kukojoa damu huku mwili ukiishiwa nguvu na hatimaye kusababisha kifo cha haraka.
Njiku alisema kuanzia sasa serikali itakuwa ikiwakagua watu wanaoingia mpakani na nchi jirani ili kuwabaini watakaoingia nchini kutoka nchi jirani wakiwa na dalili za ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Njiku tayari wamepata taarifa za kuenea kwa ugonjwa huo Sudan ya Kati na Uganda Kaskazini na kuwa kutokana na mwingiliano mkubwa wa raia wa nchi hizo na wenyeji wa Missenyi, ugonjwa huo unaweza kulipuka wakati wowote.
Pia alisema dalili za ugonjwa huo zinafanana na ebola kwani mgonjwa anakubwa na kuumwa kichwa, kuutapika damu, huharisha na kukojoa damu huku mwili ukiishiwa na nguvu na kuagiza kila atakayebainika kuwa na ugonjwa huo atazuiwa mpakani.
"Tumefuatilia hadi nchi jirani ya Uganda, ugonjwa huo dalili zake ni kama zile za Ebola, tutatoa matangazo maeneo yote ya mpakani na kila atakayebainika kuwa na dalili hizo atazuiwa"alifafanua Njiku
Aidha mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dk Zabron Masatu alisema walifuatilia taarifa za ugonjwa huo unaofananishwa na Ebola hadi nchini Uganda ambako waliambiwa kwamba watu 94 waligua ugonjwa huo na 31 kati yao walifariki dunia.
Kwa mujibu wa mganga huyo, bado wataalamu wa nchi hiyo hawajapata dawa wala kinga ya ugonjwa na kusema wameanza kuchukua tahadhali kutokana na kuwepo mwingiliano mkubwa wa wananchi kati ya nchi hizo.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya mtandao wa intaneti, ugonjwa wa Ebola ni tishio kutokana na kusambaa kwa njia ya hewa na kugusana ambapo mgonjwa hufariki baada ya muda mfupi.
Ugonjwa wa ebola uligundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1976 katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo tangu wakati huo hakuna matokeo ya utafiti yanayoonyesha wataalamu kupata chanzo wala kinga ya ugonjwa huo.
Jina Ebola lina asili ya mto Ebola uliopo nchini humo na nchi ya pili kukumbwa na ugonjwa huo ilikuwa Sudan Magharibi ambapo watu 397 walifariki kati ya 602 waliogungulika kuwa na virus vya ugonjwa huo.
Pia mwaka 2000 nchi jirani ya Uganda ilikumbwa na Ebola huku wataalamu wakieleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa nchi zilizo na nyani wengi barani Afrika kuendelea kulipukiwa na ugonjwa huo kutokana na kubainika kuwa wanyama hao ndiyo chanzo cha virus vya Ebola.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake