SINA shaka kwamba wasomaji wangu ni wazima wa afya njema na mnaendelea kulisoma gazeti hili la Risasi Jumatano kila linapoingia mtaani hususani katika ukurasa huu wa Uwanja wa Huba.
Kabla sijaendelea mbele na mada yetu ambayo inafikia hitimisho lake leo, napenda kuwakumbusha kuhusu kile kitabu changu cha Joseph Shaluwa … Let’s Talk About Love, kuwa kipo katika hatua za mwisho kabisa kabla ya kuingia mitaani. Ni kitabu kilichokusanya mada mbalimbali za mapenzi pamoja na Love Messages nzuri zenye ujumbe murua kwa ajili ya kurutubisha mapenzi yenu.
Swadakta! Nazungumzia juu ya kupendana, ndiyo, wiki iliyopita niligusia kuhusu maisha yako na mpenzi wako kama unampenda au anakupenda, nadhani jibu ulilipata kwa kujua kama unampenda kwa dhati au yeye naye anakupenda kwa asilimia mia kwa mia.
Leo nataka kuzungumzia ujumla wenu kwa pamoja, je, mnapendana? Maana kuna wengine kazi yao ni kutendana na kisha wanasema kwamba wanapenda.
Unaweza kuwakuta wapenzi hawaishi ugomvi kila siku, kiasi kwamba wewe ukamuonea huruma mmojawapo anayenyanyasika katika penzi hilo, ukatamani wewe uwe mwenza wa huyo anayeteseka ili umnusuru na mateso, unaweza ukawa unakosea kwa kuwa hiyo inaweza kuwa ndiyo staili yao ya mapenzi.
Hakuna mtu anayependa shida katika mapenzi na siku zote mapenzi si vita wala ugomvi, bali ni amani iliyoshushwa kutoka kwa Manani, hivyo kama wewe utamchukua mpenzi huyo ili umpe raha, siku mbili tu utashindwa kumvumilia utaamua kumuacha ukiwa unalia na kujijutia kwa uamuzi wako.
Kwake bila kupigana hukuna mapenzi! Ameshazoea staili ya mapenzi na ana mtu mmoja tu anayeweza kuishi naye ni yule tu ambaye kila siku anagombana naye na kisha kuelewana hata kama atajitokeza mwingine mwenye kumpiga hataweza kudumu naye.
Hao wawili wanaopigana kila siku wanapenda? Kuna wengine wameishi kwa amani wakiwa hawajawahi kugombana na wala kujibishana katika uhusiano wao kuanzia kujuana, uchumba hadi ndoa, lakini wanapogombana siku moja tu kila mtu anakwenda kivyake kwa kuapizana na kisha kutalikiana na ndoa yao kuingia matatani.
Wewe na mpenzi wako mko kwenye fungu gani? Mlipitia hatua zipi hadi kuwa wapenzi na je, mapenzi yenu yapo katika mfumo gani? Kwa kawaida kwa wanawake huwa inawawia vigumu sana katika kuchagua mpenzi anayemtaka kuwa mwenzi katika maisha.
Nasema hivyo kwa kuwa wanawake wengi wanaonekana kuwa ni watu wa kuchaguliwa na wanaume kuwa wapenzi wao, mwanaume anaamua kuwa anampenda binti fulani anaanza kumfukizia na kila akipigwa kibuti hakati tamaa, anaongeza kasi na kisha msichana anasalimu amri.
Je, msichana huyo alikuwa na penzi la dhati? Wakati mwingine utakuta binti huyo alikuwa na chaguo lake lingine lakini baada ya kuona kwamba jamaa haeleweki anaamua kuangushia penzi pale anapoamini kwamba anapendwa kwa kuwa anasumbuliwa na mtu aliyeonesha tangu awali kuwa hamtaki, au ndiyo tunaamini kile kinachosemwa kwamba ‘no means yes’?
Wapenzi wa aina hii wakiingia katika ndoa watakuwa wanapendana kwa dhati? Napenda kutoa angalizo kuhusiana mapenzi kuwa hayana ‘formula’ kama ilivyo kwa mpira wa miguu, huwezi kumpenda mtu kwa kuwa tu anakupenda, kama ambavyo unaweza kupenda pale usipopendwa
Kuna penzi ambalo ni nadra sana kutokea, yaani mwanaume na mwanamke wanapendana kwa kukutanishwa na hisia za mahaba mara ya kwanza tu baada ya kuonana na kisha kila mmoja ‘akamdondokea’ mwenzake, nadhani wengi wetu tungependa kukutana na wapenzi wetu katika staili hii.
Hata hivyo, nataka kuweka jambo moja muhimu zaidi kwa wapenzi, kabla ya kuingia kwenye uhusiano ambao baadaye unaweza kuzaa ndoa. Lazima mapenzi unayompenda mwenzako naye awe amekupenda kama wewe.
Kama mtakumbuka, wiki iliyopita wakati naanza kuandika makala haya nilisema kwamba, mapenzi ni hisia za watu wawili, ambazo zinafanana kutoka kwa kila mmoja kwenda kwa mwenzake. Umeona eeh?!
Pamoja na yote hayo, lazima ieleweke wazi kwamba msingi mkuu wa penzi ni kupendana. Mkishapendana, mengine yote yanaweza kuwa ya ziada tu.
KUGOMBANA NI MAPENZI?
Naamini kuna baadhi ya wasomaji watakuwa wamenielewa tofauti niliposema kwamba kuna wengine wanapenda kuwa katika uhusiano wa ugomvi. Sikuwa na maana mbaya. Nilieleza kama staili ya kuendesha uhusiano.
Kimsingi kugombana si mapenzi, lakini ni sehemu ya mapenzi, maana hakuna mapenzi yasiyo na matatizo. Kikubwa kwenu ni uvumilivu na kuchukuliana matatizo ninyi kwa ninyi. Katu usiweke mapenzi yenu nje ya nyumba yenu, kila kitu kiwe siri yenu, maana ninyi ndiyo ambao mnajua thamani ya penzi lenu.
MPO MARAFIKI?
Ni imani yangu kuwa katika safari ya wiki jana mpaka leo, kuna kitu umevuna. Hebu jiulize, huyo mpenzi wako uliyenaye, unampenda? Anakupenda? Mnapendana?...tulia ujiulize kwa utulivu na upate jibu yakinifu lisilo na unafiki.
Kama jibu litakuwa ndiyo, basi hatua inayofuata ya uchumba na baadaye ndoa inaweza kufuata. Sikiliza rafiki yangu…hata wewe ambaye bado huna mpenzi, lakini unatarajia kumpata, kama ni kweli unataka kuingia kwenye uhusiano wenye ‘akili’, lazima maswali yako ya msingi yawe hayo hapo juu: ”UNAMPENDA, ANAKUPENDA, MNAPENDANA? Hii iwe ngao yako siku zote.
Niseme nini tena? Nimechoka bwana…hadi wiki ijayo.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti la Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love vilivyopo mitaani. Mtembelee kwenye mtandao wake: www.shaluwanew.blogspot.com
Mbona picha zako zote ni za wazungu tu!!?
ReplyDelete