
KAMA ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu ya mahaba ili kujuzana mambo mawili matatu kuhusiana na matatizo tunayokutana nayo ndani ya uhusiano wetu.
Kumekuwa na utitiri wa matukio ya watu kuumizwa na wapenzi wao. Wengi wamejikuta wakiumia bila msaada wowote toka kwa muhusika.
Hii itakuwa mada ya mwisho katika mwaka 2010, katika mwaka huu kuna mengi umeyafanya, yapo yaliyofanikiwa na yapo ‘yaliyofeli’.
Lakini hii haikupi kiburi au kukuvunja moyo kutokana na maisha yetu kama biashara yenye faida na hasara. Nina imani kila mtu anapenda faida hata katika mapenzi vilevile.
Naandika mada hii kutokana na matukio mengi ya mwaka 2010 ambayo naweza kuyasema yalikuwa yana maumivu kuliko furaha kwa wapenzi wengi.
Kuna matukio mengi yameonyesha kuna usaliti ndani ya ndoa kufikia hatua ya watu kujiona hawana thamani na mwisho wa siku huchukua uamuzi mbaya wa kuua au kujiua wao wenyewe.
Lakini hebu tuangalie tatizo nini?
Tukiangalia neno mapenzi linasimama kama upendo wa watu wawili waliokubaliana kupendana, kuoneana huruma, kuheshimiana na kuvumiliana. Kama vitu hivi vitakosekana, basi elewa hakuna mapenzi zaidi ya kupotezeana muda.
Kila tatizo nililotakiwa kutoa ushauri lilionyesha kabisa kuna penzi la upande mmoja ambalo huwa linatesa upande mwingine bila mtenda kuathirika na lolote. Kama mpenzi wako haonyeshi ushirikiano zaidi ya wewe kuonekana unalazimisha, usipoanza wewe kwake kimya lazima penzi lenu linawalakini.
Au mwenzako anapofanya mambo ambayo kwako unayaona kabisa si ya kufanywa na mpenzi wako bila kukuonea huruma, tambua kuna kitu kinaendelea.
Ambaye umemchagua kuwa sehemu ya pili ya mwili wako utakaowaunganisha mwili mmoja haguswi na maumivu yako, hana huruma, si mkwel,i si muaminifu, si muelewa ukimueleza hakusikilizi zaidi ya kuamua kufanya anavyojisikia.
Ikifika hivyo ni wakati wa kujifikiria upo kwenye penzi gani? Jiulize ni kweli unayempenda anakupenda? Ukipata jibu utachukua uamuzi sahihi.
Ni kosa kuzama katika penzi ambalo huelewi upande wa pili mwenzako ana mapenzi kiasi gani kwako. Kila dalili zinaonyesha kabisa mpenzi wako hana mapenzi na wewe zaidi ya wewe kulazimisha penzi. Hapo lazima utaendelea kuumia na kuteseka, siku zote mbegu ya mapenzi umea katika moyo wenye rutuba ya mapenzi.
Usiipoteze mbegu yako ya mapenzi kwa mtu unayemuona kabisa hana mapenzi na wewe, kwa nini uumie wakati unaona kabisa hakuna mapenzi? Narudia kusema, ni makosa kulazimisha penzi au kupenda pasipo na penzi. Mpende akupendaye na asiye kupenda achana naye.
Bado una nafasi ya kuutafuta upendo wa kweli usiwe mvivu wa kuchagua, siku zote utakula wa chuya kwa uvivu wa kuchagua.
Kwa hayo machache nakutakia Heri ya Mwaka Mpya, Bwana atutangulie tuonane 2011.
No comments:
Post a Comment