
KLABU ya soka ya Yanga imetenga bajeti ya Sh bilioni nne na nusu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa soka pamoja na jengo la kitegauchumi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya klabu hiyo kujiondoa kwenye utegemezi.
Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu alibainisha hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia masuala mbalimbali ya klabu hiyo ambapo alibainisha kuwa klabu hiyo itaujenga upya uwanja wake wa Kaunda uliopo makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Twiga na Jangwani na kuwa wa kisasa.
Kwa mujibu wa Sendeu uwanja huo ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 25,000 utajengwa na kampuni ya ukandarasi ya Nedco ambayo ndio imepewa zabuni ya kujenga uwanja huo na kamati ya kuendeleza miradi ya klabu hiyo ambayo inaongozwa na Baraka Igangula.
“Ujenzi huo wa uwanja wa kisasa wa klabu yetu utasimamiwa na kampuni ya Nedco ambayo ndio imepewa kazi ya kusimamia miradi hiyo miwili ya ujenzi wa uwanja pamoja na kitega uchumi cha klabu yetu katika mtaa wa Mafia-Kariakoo hapa jijini,” Sendeu alibainisha.
Aidha Sendeu amebainisha kuwa kitega uchumi ambacho kitajengwa katika mtaa huo wa Mafia ni jengo lenye ghorofa zisizozidi 10 na kwamba ujenzi wa miradi hiyo miwili unatarajiwa kukamilika si chini ya kipindi cha miaka miwili ambapo fedha za ujenzi huo Sh bilioni 4.5 zinatarajiwa kupatikana kupitia hafla mbalimbali za kuchangia miradi hiyo kama ile ya kuandaa chakula cha usiku ambao watu maarufu pamoja na wanachama wa klabu hiyo watakaribishwa kuchangia.
Mbali na kufanyika kwa hafla hizo, pia watapeleka maombi mbalimbali kwa kampuni za ndani na nje ya nchi kudhamini miradi hiyo miwili ili kuwezesha klabu hiyo kutimiza malengo yake hayo.
Hata hivyo suala la ujenzi wa uwanja wa kisasa wa klabu hiyo lina ukakasi kiasi kwani awali ilikuwa inafahamika kuwa ujenzi wa uwanja huo unafadhiliwa na mdhamini mkuu wa klabu hiyo Yusuf Manji, ingawa uongozi wa Yanga ulipoulizwa juu ya suala hilo ulikana Manji kuhusika na kugharamia ujenzi huo.
Katika hatua nyingine, Yanga jana ilithibitisha rasmi kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2 mjini Zanzibar na kufikia kilele Januari 12 ambapo ndio sherehe za kuadhimisha miaka 36 ya Mapinduzi.
Sendeu alisema kiungo Athumani Iddi hatokuwepo kwenye kikosi kitakachokwenda Zanzibar keshokutwa kutokana na kuumia nyama ya paja.
“Athumani Iddi amekuwa haonekani katika mazoezi na mechi za siku za hivi karibuni kutokana na kuwa majeruhi, anasumbuliwa na matatizo ya misuli ya paja kuchanika na ndio maana hatosafiri na timu kwenda Zanzibar kwenye michuano hiyo ya Mapinduzi,” alisema Sendeu.
Mbali na Iddi, mchezaji mwingine ambaye atakosa michuano hiyo ni Shamte Ally ambaye bado anaendelea na matibabu ya mguu ambao umefungwa plasta ngumu (P.O.P) ambayo itaondolewa Januari 8 mwakani na kwa sasa mchezaji huyo ameanza mazoezi ya kutembea.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment