ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 17, 2010

Uwazi mwanzo wa mapenzi ni uhuru wa moyo


KAMA kawaida yetu tumekutana tena kwenye kona yetu ya mahaba ili kukumbushana mambo muhimu ambayo ndiyo mhimili mkubwa katika maisha yetu ya kila siku. Nina imani baada ya kuona kichwa cha habari mna shauku ya kujua leo nimekuja na kitu gani.

Mada hii imekuja baada ya kupata malalamiko kwa watu wengi juu ya matatizo yawakutayo katikati ya uhusiano wao kwa mtu kugundua kitu ambacho mwanzo wa uhusiano kilifichwa na mpenzi wake na kupoteza uaminifu.

Kumekuwa na tabia zilizoota sugu miongoni mwa watu kutokuwa wakweli mwanzo wa uhusiano wao kwa kuficha baadhi ya vitu wakiamini kabisa kama watavisema huenda vikapoteza penzi. Lakini watu hao wamesahau kuwa unalolificha kwa muda mrefu ni sawa na kuficha kitu kinachovunda, siku kikijulikana harufu yake haivumiliki.

Wapo watu hutumia uongo kwa ajili ya kumpata mtu na kusahau uongo wa leo ni kitanzi cha kesho.  Tatizo linalopelekea watu wengi wadanganye ni kutokana na baadhi yao kuonekana hawapendi vitu fulani kwa kusema kama mwenzake atakuwa vile basi hakuna penzi.

Hii imesababisha watu wengi kuficha mambo yao ya nyuma ambayo humfanya aishi kwa mashaka kwa kuhofia siri yake kuvuja.

Nataka niliweke wazi hili ambalo huenda ni hofu ya kupoteza penzi, lakini hili huwa tiba ambayo itakupa uhuru wa kuishi na mtu anayetambua historia yako ambayo kama angeisikia kupitia watu ingekuondolea uaminifu na kuonekana ni muongo usiyefaa. Wengi huamini mwanzo wa mapenzi uongo ndiyo unaochukua nafasi kumnasa mwenzako, kumbe siyo kweli.

Lakini ni vizuri mwanzo wa mapenzi kutumia nafasi hiyo kuelezea historia yako au udhaifu ambao hata ukitokea mbele kisionekane kitu kigeni. Kwa mfano uliwahi kuzaa kabla ya kuanzisha uhusiano mpya au ulikuwa na mpenzi uliyeachana naye kwa kueleza sababu zilizosababisha mtengane.

Hii itakusaidia hata mpenzi wako wa zamani anapotaka kulazimisha penzi kupata utetezi kwa mpenzi wako mpya kwa vile kila kitu anakifahamu. Lakini kama ulikaa kimya utakuwa umejiharibia.

Pia hata kama kuna tukio ambalo kwako uliliweka wazi kabla ya kuanza uhusiano kiasi cha mwenzako kukubaliana na wewe muwe wapenzi.

Hii itakusaidia uishi kwa uhuru moyoni kwa kuamini hakuna kigeni kwa mwenzako. Lakini kama utakuwa msiri na kuamini siri hiyo itadumu milele lazima utaishi kwa mashaka kwa kukosa amani ya moyo wako. Kumpima  mpenzi wa kweli usimfiche kitu ili ujue kweli anakupenda au anapenda kilicho kizuri tu.

Kumbuka mpenzi anayechagua mazuri tu si mtu mwenye mapenzi ya dhati humpenda mtu kwa umbile, sura au fedha. Lakini siku vitu hivyo vikiondoka na yeye mapenzi yamekwisha. Siku zote tanguliza ukweli katika kitu chochote ambacho kitakutengenezea kusoma na kutambua umesimama sehemu ipi. 

Na ukishajitambua hutakuwa na hofu tena kwa vile aliyekupokea, kakupokea kama ulivyo. Jiepushe na kutanguliza uongo mwisho wa siku unakuumbua na kulia kilio cha majuto.

Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

No comments: