MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amezua jambo jingine kwenye chama chake cha Chadema baada ya kueleza kuwa kelele zote ndani ya chama hicho, zinatokana na fitina ambazo zimejengwa baada ya kutangaza kuwa mwaka 2015 atagombea nafasi kubwa kwenye uchaguzi mkuu.
Zitto, ambaye alijipatia umaarufu katika Bunge la Tisa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja, ndio kwanza ametoka kwenye mgogoro na wabunge wenzake baada ya kutofautiana na uamuzi wao wa kutoka kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kuhutubia ili kutuma ujumbe wa msimamo wa chama wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais.
Kabla ya uchaguzi, Zitto alisababisha kizaazaa baada ya kutangaza kugombea uenyekiti wa Chadema katika kipindi ambacho chama hicho kilionekana kutaka mwenyekiti wake wa sasa, Freeman Mbowe aendeleze kazi ya kukijenga chama.
Zitto pia alitofautiana na viongozi wenzake baada ya kutamka hadharani kuwa haungi mkono uamuzi wa katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa wa kuwaachisha kazi wafanyakazi wawili kwenye ofisi ya makao makuu ya chama hicho kwa tuhuma za kuvujisha siri.
Tamko lake kwenye mkutano wa hadhara aliouitisha kwenye Uwanja wa Cine Atlas mjini Kigoma juzi unaonekana kukaribisha mgogoro mwingine baina yake na wanachama wenzake baada ya kutuhumu kuwepo na njama dhidi yake kutokana na nia ya kugombea urais mwaka 2015 baada ya Dk Slaa kuzoa kura nyingi katika uchaguzi wa mwaka huu alipogombea nafasi hiyo.
Zitto, ambaye katika siku za karibuni amekuwa akitofautiana na wanachama wenzake kiasi cha kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye katika uongozi wa kambi ya upinzani bungeni, alisema hayo juzi katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika eneo la Cine-Atlas lililo Ujiji mjini Kigoma.
Zitto aliuambia mkutano wa hadhara kuwa kelele zote ndani ya Chadema zimetokana na fitina zinazotengenezwa dhidi yake kwa kuwa kuna uwezekano kwake wa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
"Baada ya uchaguzi kumalizika, watu sasa wanajipanga kwa ajili ya uchaguzi mwingine. Kuna watu wanaotaka nihame Chadema kwa kuwa wananiona ni kikwazo kwao, lakini nasema siwezi kuhama kwa kuwa nina mtazamo wa mbele wa kugombea urais," alisema Zitto.
"Kigoma inaweza kumtoa rais ingawa watu wanasema haiwezekani kwa sababu ni mwisho wa reli (ya Kati). Nasema siwezi kufanya makosa ya kuhama kama walivyofanya walionitangulia na wakapoteza dira.
"Kingine najua mtakuwa mmesikia mengi kupitia vyombo vya habari, lakini nataka niwaeleze kwamba sikulishwa sumu na hakuna anayeweza kunipa sumu."
Mbunge huyo ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa Chadema, aliongeza kusema: "Mimi sing’oki Chadema kamwe na wale wanaotaka nitoke basi waanze wao. Kwa sababu, chama hiki ni chetu. Watu waliteswa, walifungwa jela, hata kupigwa na polisi na kuumizwa kwa ajili ya Chadema. Nasema siwezi kukimbia hata mara moja."
Alisema baadhi ya watu wa Kigoma waliokuwa viongozi wa Chadema na kuamua kukimbilia CCM baada ya kutokea mifarakano ndani ya chama hicho, wamejikuta wakipata aibu kwa kupoteza heshima mkoani Kigoma.
Alisema viongozi hao licha ya kukimbilia CCM, bado mkoa huo haujapiga hatua yoyote kubwa ya kimaendeleo jambo linaloonyesha kwamba maendeleo hayaletwi na chama bali ni juhudi na mikakati ya viongozi kwa kushirikiana na wananchi katika kuibua miradi, kuisimamia na kuitunza kwa faida ya Jamii.
Zitto alibainisha kuwa migogoro yote inayoonekana Chadema ni mchakato wa kidemokrasia lakini kwa ujumla mambo ni shwari ndani ya chama hicho.
"Ndugu zangu nataka niwaambie kwamba, kwa kawaida, baada ya uchaguzi mmoja, watu hujipanga kwa ajili ya uchaguzi ujao. Sasa haya mnayoyasikia ni mchakato wa kidemokrasia tu ndani ya Chadema, lakini kwa ujumla mambo ni shwari," alisema.
Zitto ametoa kauli hiyo takriban majuma mawili tangu alieleza gazeti hili kuwa ameamua kutozungumzia masuala ya chama chake kwa kuwa ameona kufanya hivyo ni kuchochea migogoro.
Zitto alikuwa ametakiwa kutoa msimamo wake baada ya kamati kuu ya Chadema kukataa kuidhinisha uamuzi wa wabunge wa chama hicho kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye na kumtaka mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kupima mwenyewe uzito wa kitendo hicho cha wabunge wenzake.
Katika hatua nyingine, Zitto aliwataka viongozi wa Chadema kujiuliza sababu zilizosababisha NCCR Mageuzi kushinda majimbo manne mkoani Kigoma huku walioshinda ubunge wakiwa wanachama walioihama Chadema.
"Viongozi (Chadema), tunapaswa kukaa chini na kutafakari kwa kina, tatizo lipo kwetu sisi viongozi au tulisimika wagombea wasiokubalika?
"Kati ya wabunge wanne wa NCCR, watatu walikuwa viongozi wetu wa chama hadi mwaka 2009 na kama tungekaa nao vizuri, pengine leo hii wangekuwa wabunge wetu na kuongeza idadi yetu Kigoma."
Aliwaeleza Wananchi hao kwamba Serikali ina tabia ya kusikiliza sauti ya Kigoma wakati mbunge anapokuwa chama cha upinzani na kwamba hali hiyo imechangia mkoa huo kuanza kupata miradi ya barabara kadhaa za lami, hivyo kurahisisha shughuli za uchukuzi na usafirishaji, jambo lililokuwa kikwazo kwa miaka mingi mkoani humo.
Kuhusu kesi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Ally Mleh Zitto alieleza kwamba wabunge wa Chadema wanaotoka Kigoma watahakikishiwa wanaisimamia kesi hiyo, ili iweze kusikilizwa na maamuzi kutolewa kwa haki na kwamba chama hicho kinatarajia ushindi.
Zitto alisema kwa mujibu wa fomu za matokeo zilizokusanywa kutoka vituoni, mgombea wa Chadema alishinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu.
Katika uchaguzi huo zilizuka vurugu kubwa baada ya polisi kuwapiga mabomu ya mochozi wananchi waliofurika kwa wingi katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini kufuatilia matokeo.
Hata hivyo, Serukamba aliwaeleza wananchi Desemba 17 kwamba kamwe hatarajii kupoteza nafasi hiyo kutokana na kesi dhidi yake kutokuwea na ushahidi wowote wa kumkwamisha.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa kwa mara ya kwanza Januari 15, 2011 katika Mahakama Kuu Kanda ya Magharibi ambapo inatarajiwa kutawala hisia za wengi ndani na nje ya Jimbo hilo.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment