ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 14, 2010

Zitto njia panda

Geofrey Nyang’oro
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kupima mwenyewe kama aendelee na wadhifa wake wa naibu kiongozi wa upinzani bungeni baada ya wabunge wa chama hicho kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.Pia, mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda ameundiwa tume ambayo itamchunguza mwenendo wake ikiwa ni baadhi ya mikakati ya chama hicho kujiweka sawa dhidi ya mtikisiko uliotokea baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.


Zitto, ambaye alijijengea umaarufu mkubwa katika Bunge la Tisa, aliingia matatizoni baada ya kupinga hadharani msimamo wa wabunge wa Chadema kutoka kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kutoa hotuba ya uzinduzi wa Bunge la Kumi.

Zitto, ambaye hakuingia kwenye ukumbi wa Bunge kutekeleza uamuzi wa wenzake wa kumsusia Rais Kikwete, aliitisha mkutano na waandishi wa habari baada ya kitendo hicho cha kihistoria na kusema kuwa hawakupaswa kutoka kwenye ukumbi huo na kuweka hadharani jinsi uamuzi huo ulivyofikiwa ndani ya vikao vya wabunge wa Chadema.
Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa chama chake hakiwezi kuwaachia viongozi wake kufanya mambo yaliyo kinyume na misimamo ya chama na hivyo kimempa fursa Zitto apime mwenyewe kama anaweza kuendelea kuogoza watu wasiokuwa na imani naye.
Alikuwa akizungumzia mambo yaliyojiri katika kikao cha wabunge kilichofanyika kwa muda wa siku mbili mjini Bagamoyo wiki iliyopita na kufikia uamuzi huo wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani mbunge huyo katika nafasi yake ya unaibu kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Dk Slaa alisema maamuzi ya wabunge ya kutokuwa na imani naye kwa nafasi ya unaibu kiongozi bungeni yalifikishwa kwenye kamati kuu ya Chadema iliyoketi Desemba 11 mwaka huu.
“Kamati kuu haikukutana kujadili suala za Zitto sababu chama hakina mamlaka ya kuingilia kazi ya kamati ya wabunge, bali kilipokea taarifa ya uamuzi wa wabunge hao,” alisema Dk Slaa.
Alisema kutokana na chama kutokuwa na uwezo wa kutoa uamuzi dhidi ya msimamo huo wa kamati ya wabunge, ni jukumu la Zitto mwenyewe kupima suala hilo na kuchukua uamuzi wa kujiuzulu au kuendelea na wadhifa wake.

Akizunguzia suala lililozua mjadala la uchaguzi mkuu, Dk Slaa alisema kamati kuu ilipokea taarifa ya matokea ya urais kujadili na kukubaliana kuwa matokeo yaliyompa ushindi Rais Jakaya Kikwete yalichezewa.
Alisema kutokana na sababu hizo, Chadema imependekeza kuundwa kwa kamati huru itakayochunguza matokeo hayo na kutoa taarifa itakayolenga kuweka wazi juu ya kila kitu kilichojiri kwa manufaa ya taifa.

“Ushahidi wa matokeo kutoka katika vituo kutofautiana na yale ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi; karatasi za matokea kufutwa ni vielelezo tosha kuwa matokea hayo yalichezewa,” alisema Dk Slaa.
“Kisheria Tanzania ina rais na sisi Chadema tunasema nchi hii ina rais, lakini njia iliyutumika kumpata rais huyo si halali na hilo ndilo lililosababisha wabunge wa Chadema kutoka nje siku ya ufunguzi wa Mkutano wa Bunge,” alisema Dk Slaa.
"Unajua hapa suala la kutambua au kutokumtambua rais siyo issue. Rais yupo na katiba inaelekeza kwamba rais akishachaguliwa huwezi kuhoji mahali popote na kwa maana hiyo rais yupo. Tatizo ni jinsi alivyopatikana."
Naye mkurugenzi wa habari na uenezi wa Chadema, Erasto Tumbo alisema kamati kuu iliunda tume inayoongozwa na Profesa Mwesiga Baregu na kutaja kazi zake mojawapo ikiwa ni kumpa ushauri Zitto na pili kumchunguza mbunge wa Jimbo la Maswa, John Shibuda.

Shibuda, ambaye alitokea CCM baada ya kuangushwa kwenye kura za maoni, aliripotiwa na vyombo vya habari kuwa alikorofishana na mbunge mwenzake wa chama hicho, Ezekiel Wenje wa Jimbo la Nyamagana kiasi cha kufikia kutupiana maneno makali.
Vyombo hivyo vilidai kuwa Shibuda aliahidi kumshtaki Wenje kwa wazee wa chama hicho kilichoshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“Kamati kuu ya imeunda tume itakayaofanya kazi mbili; ya kwanza itakuwa kukutana na Zitto na kumshauri na kazi ya pili ni kumchunguzi mbunge wa Maswa John Shibuda,” alisema Tumbo.

Kamati kuu, iliyokutana kwa siku moja jijini Dar es Salaam na pia kujadili suala la uchaguzi mkuu na mwenendo wa wanachama wake, imeeleza kuwa uamuzi wa kumchunguza Shibuda unatokana na mbunge huyo kuonekana kutokuwa na madili ndani ya chama.

“Kamati itamchunguza Shibuda na kutoa taarifa kwa chama na hii imetokana na mwenendo wake kubadilika na amekuwa akikiuka maadili ya chama,” alisema Tumbo.
Alisema Chadema ina maadili yake ambayo kila mwanachama na kiongozi anastahili kuyafuata na kwamba kitendo cha mbunge huyo kukiuka maadili hayo ikiwa ni pamoja na kuzungumza mambo ya chama kwenye vyombo vya habari bila utaratibu.

                                            CHANZO:MWANANCHI

No comments: