Sunday, January 23, 2011

Cecafa isikatae Shirikisho la mto Nile


Image
Rais Jakaya Kikwete akiangalia Kombe la Chalenji. Kushoto ni Rais wa TFF, Leodegar Tenga na wa pili kulia ni kocha wa timu ya taifa, Jan Poulsen na Waziri wa Habari, vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi.

PENDEKEZO la Shirikisho la soka nchini Misri kuanzishwa kwa shirikisho jipya la soka kwa nchi za bonde la mto Nile lina maslahi makubwa katika soka. 

Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia mashindano ya nchi zilizopo bonde la mto Nile yaliyomalizika nchini Misri hivi karibuni. 

Katika mashindano ya mwaka huu, nchi zilizoshiriki ni pamoja na wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Tanzania, Kenya, Uganda, Sudani na Burundi, huku DRC ikiwa inashiriki kama timu mwaliko wa mashindano hayo. 

Sote tumeshasikia kwamba Rais wa shirikisho la soka la Misri, Samir Zahir akisema ni muhimu na inapaswa kufanyika uundwaji shirikisho la soka kwa nchi zinazounda bonde la mto Nile (kihistoria mto Nile unaitwa mto Hapi, walivyoita mababu wa Afrika). 


Mashindano ya mwaka huu mshindi alijinyakulia dola za Marekani 170,000 mshindi wa pili dola za Marekani 125,000 na mshindi wa tatu ni dola 100,000. Katika mantiki rahisi ni kwamba uundwaji wa shirikisho hilo unapangwa kukubaliwa na washiriki wa mashindano hayo. 

Nchi zinazounda bonde la mto Nile ni Sudan, Misri, Ethiopia, Burundi, Uganda, Tanzania na 
Kenya. Pengine tunaweza kusema kwamba shirikisho hilo litakuwa linasimamiwa zaidi na mataifa mawili Sudan na Misri kutokana na mikataba yao ya umiliki wa maji ya mto Nile tangu mwaka 1929. 

Lakini suala hilo la kuunda kwa shirikisho tunaweza kuliweka mbali na masuala ya kisiasa kwani linaweza kuwa changamoto nzuri na fursa ya kuinua kiwango cha nchi za Afrika Mashariki na Kati. 

Katika mashindano ya mwaka huu tumeona kwamba Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, 
Burundi na Sudan hazijaweza kufanya vema lakini kuna ishara nzuri ya kufanikiwa siku zijazo. 
Cecafa inapaswa kukubaliana na maombi ya Shirikisho la Soka Misri (EFA) na kuungana kisha 
kuunda shirikisho hilo jipya kwa utaratibu ufuatao. 

Kwanza, Cecafa itambue kuwa kuundwa kwa shirikisho la soka kwa nchi zinazounda bonde la mto Nile ni fursa ya kuwaendeleza wanachama wake. Pili ni lazima Cecafa ikubali kwamba ili kufanikisha kutangaza na kupanua shughuli zake ni muhimu kuunda shirikisho la bonde la mto Nile. 

Sababu ni kwamba, Cecafa inaweza kubaki na mashindano yake kama ilivyo, toka vijana hadi timu za wakubwa. Pia inaweza kukubali kuunda shirikisho kwa sharti kwamba inapaswa kufanyika katika nchi zinazoshiriki. 

Kwa mfano, mashindano ya mwaka huu yamefanyika huko Misri na mashindano yanayofuata 
yanaweza kufanyika aidha Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi au Sudan. Kila taifa linaloshiriki ni lazima liwe na sauti kwa asilimia 100 bila kujali kiwango chake cha soka. 

Pia mashindano hayo yanaweza kuzialika mataifa mengine kama Nigeria, Afrika Kusini na kadhalika. Cecafa inatakiwa kuelewa kwamba kuunda kwa shirikisho la nchi hizo hakuna maana kwamba ni ishara ya kutaka kuvunja kwa shirikisho lililopo, bali ni kuongeza fursa kwa wanachama wake. 

Kwa kutambua ushirikiano wake na nchi jirani Misri imeona kuna umuhimu mkubwa wa 
kuanzisha shirikisho hilo, lakini ni vema Cecafa ikaweka wazi mipango yake endapo shirikiho la 
nchi zinazounda bonde la mto Nile litaanzishwa. 

Katika mashindano ya Cecafa tumekuwa tukishirikisha timu zilezile, na bado hatujaona 
mabadiliko makubwa. Angalau mwaka jana tuliialika Ivory Coast ambayo ilileta changamoto 
licha ya kutumia kikosi cha pili. 

Lakini kwa hakika soka la Afrika Mashariki linahitaji changamoto mpya ambayo inaweza 
kulisaidia shirikisho lenyewe na nchi wanachama. Na vilevile tunaweza kutoa ombi la nchi zote zinazoshiriki mashindano ya mto Nile ikiwemo ile itakayoalikwa, kushiriki mashindano ya Cecafa. 

Hii ina maana kwamba mbali na Sudan, Ethiopia, Burundi, Uganda na DRC, ni Misri peke yake siyo mwanachama wa Cecafa. Hivyo tunachohitaji hapa ni kuitaka Misri ikubali mwaliko wa kila mwaka kushiriki mashindano ya Cecafa kama sehemu ya kuunda shirikisho jipya la nchi 
za bonde la mto Nile. 

Cecafa inapaswa kufahamu kuwa kuzialika Malawi na Zambia hakuna tija, hivyo ni muhimu 
kwake kuangalia mkondo mpya ambao unaweza kuzipata nchi ambazo zitaleta changamoto zaidi. 

Sababu Zambia na Malawi walikuwa mwanachama wa Cecafa, lakini wakajitoa na kujiunga 
COSAFA (Shirikisho la nchi za Kusini mwaka Afrika). Baada ya kujitoa ilikuwa ni ishara kwamba hawahitaji kuwa wanachama wa Cecafa, hivyo ni mbinu hiyo inaweza kutumiwa na Cecafa kutozipa uzito mkubwa nchi hizo. 

Cecafa inatakiwa kufahamu kuwa kuanzisha kwa Shirikisho la mto Nile ni kuongeza njia ya 
kuweza kujipatia mapato zaidi na kuzifuata nchi mbalimbali zenye kiwango cha juu cha soka 
kutokana na nafasi ya Misri. 

Misri ikiwa nchi inayokamata nafasi ya 10 katika ubora wa soka duniani, popote inapocheza 
inafuatiliwa zaidi hivyo kuongeza umakini kutazamwa kwa nchi wanachama wa Cecafa. Sababu hii inaweza kuongeza wimbi la mawakala wa soka ambao wataichukulia uzito mkubwa 
mashindano hayo. 

Cecafa inaweza kujifunza kwa kuchukua mfano huu; Klabu ya Arsenal ya Uingereza inaendesha mashindano ya kombe la Emirates. Mashindano hayo yanazishirikishi klabu mbalimbali 
ambazo hualikwa kushiriki. 

Tunaona klabu kama AC Milan, Paris Saint Germain, Hambrug SV kwa kuzitaja chache. Yapo mataifa mengine ambayo huanzisha mashindano ya mataifa matatu ambayo yanaongezewa nguvu kwa timu mwalikwa. 

Cecafa inatakiwa kujifunza kwamba kwa muda mrefu nchi zetu hazijapiga hatua madhubuti za soka. Tunahitaji sana changamoto mpya ambayo itaondoa dhana ya kukutana sisi kwa sisi kila mwaka. 

Ni miaka nenda rudi tumekuwa tukipambana na Uganda, Kenya, Burundi, Ethiopia, Tanzania, Rwanda na Sudan. Tunaweza kupendekeza shirikisho la soka la mto Nile liwe na timu mbili zinazoalikwa. 

Timu hizi zinapaswa kuwa na hadhi kubwa ili kuweza kutoa fursa mpya kwa wachezaji kuweza kujifunza mbinu mpya na kuongeza mapato. Cecafa inatakiwa kufahamu kuwa ligi za nchi wanachama wake ni dhaifu na zinatakiwa marekebisho makubwa ili ziweze kufanya vema. 

Ligi ya Tanzania Bara inashirikisha timu 12, Kenya inayo idadi ndogo, Uganda, Burundi na Rwanda hali inakuwa hivyohiyvo. Ingawaje tunaona kwamba ligi ya Kenya imefanikiwa 
kuoneshwa katika televisheni ya Super Sport, lakini zipo changamoto kubwa sana juu ya ligi za 
wanachama wa Cecafa. 

Hakuna sababu ya kusubiri zaidi, ni muhimu Cecafa ikubali kuwa muda ni huu na hatua za 
kuelekea mafanikio ya kweli yanakuja endapo zitakubali kuunda ushirika mpya wa Nile Basin huku wakiboresha ule wa zamani (Cecafa). Umoja ni nguvu!


                                                                   Chanzo:HabariLeo

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake