Friday, January 14, 2011

Dowans ‘yawatafuna’ Sitta na Mwakyembe

SAKATA la malipo ya kampuni ya kufua umeme ya Dowans, limeingia hatua mpya baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, Mathias Chikawe, kusema mawaziri wawili waliompinga Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kutangaza serikali kuilipa 
kampuni hiyo, walikiuka utaratibu wa serikali. 


Aidha, amewataka mawaziri hao, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuacha kutoa maelezo ya sekta zisizowahusu kwani si utaratibu wa utawala bora na ni kuwachanganya wananchi. 

Akifafanua kuhusu kauli zilizompinga Waziri Ngeleja, Chikawe alisema mawaziri hao walipaswa kufuata utaratibu wa kufikisha hoja zao kwa Mamlaka husika, au wajiondoe serikalini kabla ya kupingana na waziri mwenzao. 

Alisema Waziri Sitta ni mzoefu na wa siku nyingi, hahitaji kufundishwa, kwa kuwa ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini na anafahamu namna za kutoa maoni kwa mawaziri bila kuathiri utaratibu. 

Kuhusu Mwakyembe, alisema ingawa ni mpya katika uwaziri, lakini ni mwanasheria wa siku nyingi na anajua utaratibu wa sheria ulivyo, hivyo pia hakuhitaji kufundishwa kuhusu namna ya kutoa mawazo yake kuhusu Dowans wakati akiwa serikalini tena Naibu Waziri. 

“Umefika wakati Sitta na Mwakyembe waache kuendesha mambo kisiasa, bali waangalie sheria zaidi katika suala la Dowans,” alisema Chikawe. 

Alisema kitendo cha mawaziri hao kumkosoa Waziri Ngeleja, kutokana na kutangaza hadharani kuilipa kampuni hiyo Sh bilioni 94, kimetoa picha kuwa kuna mgongano ndani ya Baraza la Mawaziri. 

Alisema jambo zito kama hilo, halikupaswa kutolewa maelezo magazetini, bali wangetumia utaratibu wa kumfuata waziri husika na kutoa maoni na ushahidi walionao na iwapo wangeona waziri huyo hawatilii maanani, wangekwenda kwa Waziri Mkuu au Rais. 

“Unajua Rais wetu ni mwepesi sana kuwasikiliza mawaziri wake wakati wowote, sasa iwapo wangeona waziri husika hawasikilizi, wangepeleka hoja yao kwake ambaye kama angeridhishwa na hoja zao, angeitisha kikao cha Baraza la Mawaziri kutoa uamuzi wa pamoja,” alisema Chikawe. 

Chikawe alisema kuna utaratibu wa aina mbili, ambao waziri anaweza kuutumia kutoa uamuzi wa Serikali; kwanza ni kutoa uamuzi unaohusu wizara yake na mwingine, uamuzi wa pamoja. 

Alifafanua kuwa waziri wa sekta husika, ana jukumu la kutoa uamuzi wowote wa wizara yake bila kuingiliwa na akiona kuna jambo zito linaloathiri sera za nchi, ndio hupeleka kwenye Baraza la Mawaziri ili lijadiliwe kabla ya kutoa uamuzi wa pamoja. 

Chikawe alisema Waziri Sitta na Naibu Waziri Mwakyembe, walikuwa na nafasi ya kumwona Rais na kutoa ushahidi wao na iwapo Rais angeona kuna umuhimu wa kuitisha Baraza la Mawaziri, angefanya hivyo na si kutoa siri za Baraza kuwa hawajalijadili suala hilo. 

Alisema maoni binafsi kwa mawaziri hao si tatizo, ndiyo maana katika Baraza la Mawaziri, kikao kinaweza kujadili suala moja kwa siku nzima mpaka wanafikia uamuzi wa pamoja, lakini kuyazungumzia hadharani ni kosa, kwa kuwa wamekiuka utaratibu wa utawala bora kwa kutoa siri za Baraza hilo. 

Chikawe alimtetea Ngeleja kuwa inawezekana hakuona sababu ya kupeleka suala la kuilipa Dowans kwa Baraza la Mawaziri kwa kuwa alishirikisha wataalamu mbalimbali wa sheria na 
kujiridhisha katika kufanya malipo kwa kampuni hiyo. 

Wiki iliyopita, Waziri Sitta alipinga tamko la Waziri Ngeleja la kuilipa kampuni ya Dowans na kusema kuwa inashangaza waziri kutoa tamko hilo kabla hata Baraza la Mawaziri halijalijadili. 

Juzi pia Naibu Waziri Mwakyembe, aliibuka na kusema anashangaa kusikia kampuni hiyo aliyoiita ya kitapeli, inalipwa kwa madai kuwa ilirithi mkataba wa kufua umeme kutoka katika kampuni hewa ya Richmond LCC Ltd. 

Katika Bunge lililopita chini ya Spika Sitta, Mwakyembe aliongoza Kamati Maalumu iliyochunguza suala la kampuni ya kufua umeme ya Richmond hata kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha, kujiuzulu kutokana na kashfa ya kampuni hiyo.


                                                         Chanzo:Habari Leo

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake