ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 20, 2011

Ikulu: Tanzania Daima waongo

SERIKALI imesikitishwa na habari za kutungwa kwamba mawaziri wake wawili wamezibwa mdomo kutoa maoni yao katika suala la malipo ya fidia kwa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, habari hiyo iliyochapishwa na gazeti la Tanzania Daima Jumatano, si ya kweli na haina msingi.
 

Gazeti hilo jana katika ukurasa wake wa mbele, liliandika kwamba Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk. Harrison Mwakyembe walifungwa midomo na Rais Jakaya Kikwete katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika juzi Ikulu. 

Lakini taarifa ya Ikulu, iliyotumwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo ilibainisha kuwa juzi hapakuwa na kikao chochote cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete na kuelezea kushangazwa na chanzo cha habari hiyo. 

“Nachukua nafasi hii, kwa mara nyingine tena, kuviasa vyombo vyetu vya habari kufanya kazi zao kwa misingi mikuu ya uandishi wa habari, msingi wa kwanza miongoni mwa misingi hiyo ukiwa ni kuandika, kuchapisha ama kutangaza habari za ukweli. 

“Uandishi wa habari zisizokuwa za kweli siyo tu unavunja misingi ya taaluma ya uandishi na utangazaji wa habari, lakini pia unawapotosha wananchi bila sababu za msingi,” alisema Luhanjo katika taarifa hiyo na kuonya vyombo vya habari kuacha tabia ya kuokoteza habari mitaani bila uthibitisho kutoka kwa wahusika. 

Wakati huo huo, Waziri Sitta na Naibu Waziri Mwakyembe, wamelitaka gazeti hilo kuomba radhi kwa uongo huo katika ukurasa wake wa mbele la sivyo wataliburuta mahakamani. 

Mawaziri hao wamesema katika taarifa yao kuwa wanaheshimu uhuru wa habari lakini habari hizo zisizozingatia maadili ya uandishi wa habari, zimewafikisha mahali ambapo hawana namna, isipokuwa kulifikisha gazeti hilo mahakamani. 

“Tunakuandikia barua hii, upime mwenyewe, utuombe radhi kwa uongo huo uliotutungia ukurasa wa mbele wa gazeti lako au usubiri tukuburute mahakamani kukumbusha kuwa Tanzania...ni nchi yenye kuheshimu utawala wa sheria,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Sitta na Mwakyembe. 

Taarifa hiyo ilieleza kuwa gazeti hilo limeanzisha mchezo wa kubuni na kuchakachua taarifa na kuendesha kampeni zilizoitwa za majitaka dhidi ya mawaziri hao kwa maslahi ambayo gazeti hilo inayojua. 

Gazeti hili liliwasiliana na Mhariri wa gazeti hilo, Martin Malera alisema hajapata taarifa hiyo kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi. 

Hata hivyo alisisitiza kwamba kama hawajazibwa mdomo, Watanzania wanatarajia wataendelea kutetea Kampuni ya Dowans isilipwe.


Chanzo:Habari Leo

No comments: