Wednesday, January 12, 2011
Mabomu yarindima kutawanya wanafunzi UDOM.
POLISI mjini Dodoma jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya wanafunzi na wahadhiri wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) walipojaribu kuandamana kwenda Ofisi ya waziri Mkuu kufikisha malalamiko yao.Jeshi
hilo lililazimika kufyatua mabomu ya machozi ambayo yaliwatawanya wanafunzi hao waliokuwa katika eneo la chuo hicho na kuwafanya kukimbia kila mmoja na njia yake kuelekea mjini kati na kukusanyika katika uwanja wa Nyerere Squire na baadaye kufikia muafaka na polisi kuwa wakiwa katika uwanja huo, wawe watulivu na wafikishe madai yao kwa Mkuu wa wilaya ya Dodoma mjini bila kufanya vurugu.
Miongoni mwa malalamiko ya wanafunzi hao ni mikopo ambapo baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa wapatiwe Desema 6 mwaka jana lakini hadi sasa hawajapatiwa na wanapofuatilia wanaelezwa kuwa mchakato bado unaendelea.
Madai mengine ni pamoja na uhaba wa maji na hali ya uchafu wa mazingira chuoni hapo lakini pia wakishinikiza kuwa hawamtaki naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Shaaban Mlacha.
Hata hivyo wanafunzi hao waliendelea kuimba katika eneo hilo huku wakiwafukuza waandishi wa habari kwa madai kuwa kituo kimojawapo cha televisheni kiliwahi kuchakachua habari zao hali ambayo ilisababisha baadhi ya waandishi kupigwa.
Mmoja wa waandishi wa habari aliyepigwa na wanafunzi hao akiwa kazini eneo la UDOM ni Bw. Haberi Chidawaliwa gazeti la Mwananchi ambaye mbali ya kujieleza kuwa yeye si mwandishi wa kituo hicho cha televisheni na kuonesha kitambulisho alishambuliwa huku wakitaka kumnyang’anya kamera yake.
Mbali ya mtafaruku huo wa wanafunzi, wahadhiri nao wamekuwa wakilalamika kutaka hali bora.
Katika tamko la wahadhiri hao lililotolewa na Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Wafanyakazi Wanataaluma chuoni hapo (UDOMASA), Bw. Paul Loisulie lilieleza kuwa uongozi umefanya jitihada kubwa kufuatilia utatuzi wa matatizo yao bila mafanikio na uongozi wa UDOM hauyajali madai yao hali ambayo imewalazimu kumtaka Rais aingile kati suala hilo.
Taarifa ya mwenyekiti huyo inasema kuwa kwa kuwa Menejimenti ya UDOM hadi wanataaluma hao wanakwenda kwenye mkutano, haikuwa tayari kushughulikia matatizo hayo na mkutano mkuu wa nne wa UDOMASA wa Januari 8 mwaka huu ulilazimu kumwomba Rais Kikwete kuingilia suala hilo.
Wahadhiri hao nao wameamua kuendelea kufanya mikutano mpaka hapo matatizo yao yatakapopatiwa ufumbuzi.Moja ya matatizo yanayolalamikiwa na wafanyakazi hao ni malipo ambapo wanasema hawajapata mishahara mipya tangu ilipotangazwa Julai mwaka jana ya ongezeko la asilimia 20-30.
Pia yapo madai kuwa Hazina imekuwa ikilipa mishahara ya juu ngazi husika lakini Menejimenti ya UDOM inapunguza kwa visingizio mbalimbali hali inayoaathiri uchagiaji wa wanataaluma hao katika mifuko ya jamii ikiwemo NSSF, LAPF,PPFna PSPF.
chanzo: majira
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake