Wednesday, January 12, 2011

TTCL sasa kuuzwa Vietnam-TEWUTA


CHAMA cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) kimesema serikali ina mpango wa 'kuiuza' tena Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa mwekezaji kutoka Vietnam, hatua ambayo wanaamini itaifanya izidi kudumaa.

Akizungumza na Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Bw. Junus Ndaro alisema kuwa uwekezaji huo hauna nia nzuri, bali kuiuza TTCL kwa gharama poa.

"Upo ushahidi wa kutosha kuwa bado serikali haijajifunza kutokana na matukio ya nyuma. Kwa mara nyingine serikali inakusudia kuleta kampuni nyingine ya simu (VIETEL) kutoka Vietnam kuwekeza ndani ya TTCL, mazungumzo bado yanaendelea kwa pande zote mbili, na sasa ipo kampuni nyingine kutoka India (Airtel) nayo imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza ndani ya TTCL," alisema.

Alisema kuwa TEWUTA wanatambua kuwa nia yao ya kuwekeza si nzuri, zaidi sana madhumuni yao ni kutaka kuimiliki TTCL yao ambayo ni mali ya Watanzania kwa gharama poa.

Bw. Ndaro alisema Tanzania haipaswi kutegemea makampuni kutoka nje, kwani waliowahi kupewa dhamana ya uendeshaji wa TTCL kama wataalamu hawakuwa na uwezo wa kitaaluma wa kusimamia na kuleta mabadiliko yoyote ya mawasiliano ndani ya kampuni hiyo.

"Kwa muda mrefu serikali yetu ilikuwa inafanya makosa kwa kuruhusu na kuleta kampuni za nje na kuzipa dhamana kubwa ya utawala pasipo kufuatilia utendaji kazi wake," alisema.

Alisema kutokana na serikali kuruhusu uwepo wa makosa hayo, kampuni hizo zilifuja fedha ovyo pasipo kuwekeza kwenye miundombinu ya mwasiliano, bali ni katika kuhakikisha kuwa TTCL inatoweka katika huduma ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa Bw. Ndaro, TTCL inao uwezo wa kujiendesha iwapo itapata sapoti kidogo ya serikali, hivyo aliiomba serikali idhamini mkopo wa sh. bilioni 70 ili kampuni hiyo iweze kujiimarisha katika mtandao wake na kuingia sokoni kibiashara na kuwa ya kisasa.

Bw. Ndaro alisema kuwa wanaamini serikali itakapoimarisha TTCL na kuwa bora katika maeneo ya sauti na data, nchi itakuwa imepiga hatua kubwa mbele katika sekta ya mawasiliano hapa nchini.

"Nchi yetu haipaswi hata kidogo kutegemea kampuni kutoka nje ya nchi, kampuni zilizopo hapa zinajiendesha na muda wowote wanaweza kusitisha huduma zao mara watakapoona hawapati faida waliyoitarajia.

"Mfano kampuni ya (anaitaja) imeuzwa mara kadhaa, tutambue kuwa haya ni makampuni ya kibepari, yapo kibishara tu na si uimarishaji wa huduma hapa nchini," alisema.

Alisema kuwa fedha zinazohitajika ni lazima zipatikane kwa njia yoyote ile, serikali inaweza kuisadia TTCL kupata fedha hizo kwa njia ya mkopo kutoka taasisi za fedha za ndani na nje hususani katika mabenki au kampuni kubwa za vifaa vya mawasialino zilizopo nje ya nchi.

TTCL iliwahi kuletewa mwekezaji mbia, MSI/Detecon, na hadi inamaliza mkataba wake mwaka 2006, kampuni hiyo ilizaa kampuni ya Celtel, huku ikidaiwa kuwa mwekezaji huyo hakumaliza gharama za uwekezaji kadri ya mkataba.

Kampuni ya MSI/Detecon iliyokubaliwa na serikali kuwa mbia wa TTCL tangu kusainiwa kwa mkataba Februari, 21 2001, 'hadi inaondoka mwaka 2007, ililipa dola 60 milioni tu ambazo ni nusu ya gharama.

Kwa mujibu wa mkataba, MSI/Detecon ilikuwa inachukua hisa 35 kwa gharama ya dola 120 milioni (sawa na sh. 150 bilioni), lakini walichuma karibu sh. bilioni 4 kila mwaka tangu 2001 hadi Septemba 2005.
 
chanzo: Majira

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake