Na Shakoor Jongo
STAA wa muziki wa mwambao aliye pia Mkurugenzi wa Kundi la Jahazi Modern Taarab, Mzee Yusuf ‘Mfalme’, (pichani) amelazwa katika Hospitali ya Dokta Baki Kibaha mkoani Pwani akisumbuliwa na maumivu makali ya mguu.
Mwimbaji huyo ambaye anatamba na albamu yake ya ‘My Valentine’ amelazwa kitandani akiwa hoi katika hospitali hiyo baada ya kugundulika kwamba mguu wake wa kulia aliowahi kupata ajali na kufanyiwa upasuaji, haujaunga vizuri.
Akizungumza kwa njia ya simu na Amani juzi, Mzee Yusuf alisema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na maumivu katika mguu huo lakini alikuwa akiyapuuza.
“Unajua hili tatizo la mguu lilinianza siku nyingi sana, lakini chanzo chake kikubwa ni ile ajali niliyoipata nikiwa Zanzibar wakati wa maandalizi ya albamu yangu ya kwanza, ‘Two in One’”, alisema.
Ajali hiyo ambayo ilihusishwa na imani za kishirikina ilisababisha kuvunjika kwa mguu Mzee Yusuf na kushauriwa kwenda nchini India kwa ajili ya uchunguzi zaidi lakini pia staa huyo akapuuza.
“Tangu nilipopata ajali ile, mguu umekuwa ukinitesa kwa maumivu mara kwa mara, kiasi cha kutakiwa kwenda India kwa uchunguzi zaidi lakini nimekuwa nikidharau,” alisema.
Kuna siku mwimbaji na mpiga kinanda huyo aliyepata kupitia Bendi za Zanzibar Star na East African Melody aliteguka mguu wake huo katika mechi za bonanza la mpira wa miguu alitoneshwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Madaktari wakaniambia tena suala la kupelekwa India lakini nikadharau,” alisema Mzee Yusuf ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu katika Klabu ya Soka ya Yanga ya Dar.
Baadhi ya watu wa karibu wa msanii huyo wamesema kuwa, huenda akafanyiwa upasuaji upya kwa kuwa inawezekana mguu huo haukuunga vema.
Kama vile haitoshi, wadau wa muziki wa mwambao wamedai kwamba bado tukio hilo linahusiana na imani za kishirikina kutokana na nyota ya staa huyo kuwa juu kwa sasa.
chanzo:Global Publishers
No comments:
Post a Comment