
Naibu Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia, Charles Kitwanga
SERIKALI imeitaka kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), kuanzisha mfumo wa kulipia huduma za simu kabla kutumia ili kukusanya mapato kwa urahisi zaidi.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Charles Kitwanga alitoa wito huo, jana jijini Dar es Salaam wakati baada ya kutembelea kwa mara ya kwanza ofisi za kampuni hiyo tangu ateuliwe na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo.
Alisema sekta ya mawasiliano ya simu nchini ina ushindani mkubwa na kwamba ubunifu unahitajika kufanya biashara.
Kitwanga alisema kama kuna wateja ambao hawalipii gharama za matumizi ya simu, wanatakiwa kufungiwa mfumo wa kulipia huduma za simu kabla ya kuzitumia.
Kwa mujibu wa uongozi wa TTCL, Serikali inadaiwa Sh 7.2 bilioni zikiwa ni gharama za matumizi ya simu katika ofisi zake.
“Hamuwezi kuendelea kulalamikia wateja ambao wanadaiwa wakati hamchukui hatua za kisasa za kukusanya mapato,”alisema.
Alisema mfumo wa kulipia gharama kabla ya kutumia, unapunguza gharama za uendeshaji na itaongeza mapato.
Naibu Waziri aliwataka wafanyakazi wa kampuni hiyo, kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuiletea tija kampuni hiyo.
Alisema kwa sasa taasisi za serikali zinalipia gharama za huduma za simu kwa wakati na kwamba yaliyobaki ni madeni ya zamani.
“ Ni lazima taasisi za serikali ziendelee kulipia huduma za simu kwa sababu bajeti ya huduma hiyo wanayo, wasipolipa kwa wakati tutashangaa,”alisema.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment