ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 20, 2011

Usipokuwa tayari kumsikiliza mwenza wako, penzi lako lina walakani

Awali ya yote tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu ambaye ametukutanisha tena kupitia safu hii tukiwa wazima. Tuna kila sababu ya kufanya hivyo kwa sababu wapo ambao walitarajia kuiona wiki hii wakiwa wazima lakini haikuwa hivyo.


Baadhi wameshatangulia mbele za haki na wengine wako hoi vitandani. Kwa maana hiyo basi sisi ambao bado tunaendelea kudunda juu ya ardhi hii tuone kwamba tumependelewa na hivyo tushukuru.

Mpenzi msomaji wangu, tunaambiwa mapenzi ili yaweze kuwa imara ni lazima ziwepo nguzo mbalimbali. Hii ikimaanisha kwamba ili uhusiano wenu wa kimapenzi uweze kudumu tena katika mazingira ya amani na furaha, mambo kadhaa lazima yazingatiwe.

Mambo hayo yako mengi na nikisema niyazungumzie hapa, ukurasa huu mzima hauwezi kutosha ila leo nataka kuzungumzia hili la wapenzi kusikilizana. Hili litawagusa walio ndani ya ndoa na wale wanaotarajia kuingia katika au walio katika uhusiano wa kawaida.

Bila shaka utakubaliana nami kwamba, kama kutakuwa na mazingira ya wapenzi kutokusikilizana katika yale ambayo yanagusa maisha yao ya kila siku, ni vigumu kuweza kupiga hatua na mwishowe kushindwa kutimiza ndoto zao za kuishi pamoja milele.

Nimefikia hatua ya kuandika makala haya baada ya kuona baadhi ya wapenzi wakihitilafiana kwa sababu tu mmoja kashindwa kumsikiliza mwenzake tena yawezekana suala lenyewe ni kwa manufaa ya wote.

Hivi unaathirika nini kwa kusikiliza kile anachokuambia mpenzi wako kisha ukakipima kuliko kudharau na kuona huna sababu ya kumpa sikio lako na kile anachotaka kukuambia kikapenya?

Yawezekana kweli akawa anataka kukuambia jambo ambalo wewe usingependa kulisikia lakini huwezi kujua kama hutamsikiliza kwanza.
Kwa mfano, mpenzi wako anakushauri juu ya maisha yenu kwamba, umefika wakati wa kuwa makini na matumizi ya kila shilingi inayopatikana ili muweze kutimiza malengo yenu.

Hilo nalo ni jambo baya? Huoni kwamba anachokuambia ni cha msingi na unatakiwa kumsikiliza kisha  kushirikiana katika kukitekeleza?
Cha ajabu sasa, unakuta mtu anashauriwa jambo na mpenzi wake, badala ya kusikiliza anaanza kuwaka na kuona kwamba mwenza wake huyo hana nafasi ya kushauri lolote, kwa staili hiyo mtafika kweli?

Achilia mbali hilo, yawezekama mpenzi wako kuna jambo linamkosesha amani na anahisi mtu wa kumweleza ili aweze kumsaidia ni wewe, hivi utamfanya ajisikieje endapo utapuuza na kuona kwamba anakupa usumbufu? Kama wewe utaona hivyo unadhani ni nani atamsikiliza na kumsaidia?

Tujue kwamba, kukataa kumsikilza mpenzi wako ni miongoni mwa dalili za kutokumpenda kwa dhati kwa sababu unayempenda lazima utamthamini na kumheshimu. Hayo yote yatakuja kwa kumsikiliza pale anapohisi anastahili kufunguka mbele yako.

Wapo watu huko mtaani ambao wamewafanya wenza wao wasiwe huru kuwaeleza yale ambayo wanahisi wanastahili kuwaambia, sasa hili ni tatizo! Mpenzi wako ni sawa na rafiki yako, mpe uhuru wa kukuambia chochote ili mradi na yeye awe amekitafakari na kuona kwamba hakiwezi kukutibua.

Cha kuzingatia hapa ni kila mmoja kutambua amuambie nini mpenzi wake na katika muda gani. Yawezekana jambo unalotaka kumuambia mwenza wako ni la msingi lakini ukashindwa kumueleza katika wakati muafaka, matokeo yake ukapata majibu ambayo hukuyatarajia.

Kwa mfano, mpenzi wako au mume wako anarudi kazini na kabla hajatulia tayari umeanza kumueleza kuhusu taarifa ulizozipata kwamba anakusaliti.

Hivi kwa muda huo unatarajia kupata jibu sahihi kweli? Huwezi na zaidi ya yote unaweza kusababisha mtifuano mkubwa ambao ungeweza kuuepuka.

Jamani nilichotaka kukizungumza leo ni kila mmoja kuwa makini na nini amuambie mpenzi wake na wakati gani kisha kila mmoja awe tayari kumsikiliza mwenzake.

Hata hivyo, si kila kitu lazima umuambie mpenzi wako, kwa jinsi ulivyomsoma unaweza kuwa umjua vizuri na kutambua lipi la kumuambia na lipi unaweza kulimezea.

Ukiwa ni mtu wa kuongea kila jambo bila hata kujua madhara au mpenzi wako atachukuliaje, unaweza kuwa chanzo cha kuhitilafiana kila siku na wakati mwingine kujuta kwanini uliliongea jambo hilo kisha likaleta kizazaa.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.

No comments: