ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 8, 2011

CUF waandamana kupinga Dowans-Majira

[Civic United Front]
*Wahofia 'ya Tunisia, Misri' endapo italipwa mabilioni
*Lipumba ataka waliosababisha kashfa hiyo wawajibishwe 


Na Heri Shaban

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimefanya maandamano makubwa jijini Dar es Salaam na kutoa tamko la
kupinga malipo ya sh. bilioni 94 kwa Kampuni ya Dowans na kutaka waliosababisha kashfa hiyo kuwajibishwa.


Maandamano hayo yaliyoongozwa viongozi wa ngazi ya juu wa CUF na kumshirikisha Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bw. Ambar Haji Khamisi, yalianzia Buguruni Sheli hadi Viwanja vya  Kidongo Chekundu jirani na maeneo ya Mnazi Mmoja.

Walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali wa kupinga malipo hayo, yakiwamo, 'CCM chama cha mafisadi', 'Yaliyotokea Tunisia yatatokea hapa kwetu endapo fedha hiyo italipwa' na 'Bei ya mkate 750/ badala ya 300/ baada ya bei ya umeme kupanda'.

Maandamano hayo yaliongozwa na polisi wa kawaida na wale wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakiwa hawana silaha.

Akitoa tamko hilo baada ya maandamano hayo Mwenyekiti wa chama hicho, Prof Ibrahim Lipumba alisema CUF inapinga kulipwa kwa fedha hizo kutokana na kuwa zinahitajika katika matumizi mengine kama elimu, afya, maji ufuaji na usambazaji wa umeme.

"Nchi yetu hivi sasa inakabiliwa na mgao mkubwa wa umeme ambao ni mkali kuliko ule 2006, umeme unafuliwa haukidhi mahitaji. Tunaambiwa maji katika mabwawa yanayofua umeme yamepungua sana.

"Tatizo hili ni la muda mrefu Watanzania wana kila sababu kukasirishwa na mgao huu wa umeme kwa miaka mitano baada ya mgao wa 2006 na kuahidiwa na serikali kuwa mgao huo utakuwa ni historia," alisema Prof Lipumba.

Alisema athari za umeme ni kubwa kwa kuwa wananchi wanasumbuka vyombo vya umeme maofisini na viwandani vinaharibika kwa sababu ya ukataji wa umeme wa mara kwa mara shughuli za uzalishaji bidhaa na utoaji huduma zimeathirika na ajira zimepungua.

Alisema kuwa wawekezaji wa ndani na nje wanasita kuwekeza vitega uchumi na hivyo kuongeza ajira kwa sababu ya kutokuwa na umeme wa uhakika, umeme ambao ndio nishati kuu kwa kuwa matumizi ya mitambo viwandani na majumbani ili kupunguza matumizi ya nishati ya mkaa kwa lengo la kulinda mazingira.

Prof Lipumba alisema uzalishaji wa umeme nchini kwa asilimia 90 unategemea maji ya mvua hivyo isingekuwa tatizo iwapo kungekuwa na hifadhi ya maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme yangekuwa ni ya uhakika kwa bahati mbaya uhakika huo haupo kwa sababu ya maji

"Nchi yetu imejaliwa vianzo vingi vya nishati ya umeme maeneo ya maporomoko ya maji yakitumiwa yote yanaweza kufua umeme wa MW 5,000 ilinganishwa na uwezo wa sasa wa MW 562 na umeme wa gridi ya taifa MW 791 makaa ya mawe yamegundulika yanaweza kufua umeme wa MW 1,000 kwa zaidi ya miaka 50 ijayo," alisema Prof Lipumba.

Alisema kuwa gesi iliyogundulika Mnazi Bay, Mtwara; Mkuranga, Pwani na Songosongo, Lindi inaweza kufua umeme wa zaidi ya MW 1,000 kwa zaidi ya miaka hamsini ijayo, pia madini ya urani (uranium) yaliyogundulika Namtumbo na Manyoni nayo yana uwezo pia wa kufua umeme.

Chimbuko la Dowans

Akielezea chimbuko la kampuni hiyo, Prof. Lipumba alisema kuwa Dowans Holdings SA ni Kampuni iliyoanzishwa Julai Mosi 2005 chini ya sheria za Costa Rica.

Alisema kampuni hiyo haina raslimali nyingine isipokuwa Dowans Tanzania Ltd, iliyoianzisha Novemba 28 2005 na ilimpa mamlaka ya kisheria (Power of Attorney), Bw. Rostam Azizi kuendesha shughuli zote za Kampuni ya Costa Rica ikiwa ni pamoja  kufungua, kufunga akaunti za kampuni na kutia sahihi hundi za kampuni.

Alisema mamlaka aliyopewa Bw. Aziz ni makubwa kwa kuwa yanampa uwezo wa kusimamia na kuendesha kampuni hiyo kama mali yake.

Alisema kampuni hiyo ilisajiliwa Costa Rica siyo kwa madhumini ya kufanya biashara bali kuitumia kampuni hiyo nje ya nchi hiyo na wamiliki wao wasijulikane.

No comments: