Serikali yakana kualika anayejiita mmiliki wake
Atakiwa akamatwe kwa sheria ya uhujumu uchumi
January Makamba azidi kuipigia debe mitambo yake
Atakiwa akamatwe kwa sheria ya uhujumu uchumi
January Makamba azidi kuipigia debe mitambo yake
Siku moja tu baada ya mtu anayejitambulisha kuwa ni mmiliki wa Kampuni ya Dowans Tanzania Limited, Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi, kuibuka jijini Dar es Salaam, Serikali imeruka kumwalika nchini, lakini pia wito ukitolewa kuwa akamatwe na vyombo vya dola na kuhojiwa jinsi anavyohusika na kampuni hiyo ambayo iko katika mgogoro mkali na Tanesco.
Wito huo umetolewa baada ya mmiliki huyo kuibuka juzi na kuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari, akidai kuwa ndiye mmiliki wa Dowans, lakini akikataa katakata kupigwa picha kwa ajili ya magazeti au televisheni.
Kadhalika, utata mwingine wa mmiliki huyo anayedai kuwa ni Brigedia Jenerali Mstaafu kutoka Oman, ni kauli yake kwamba alikuwa amealikwa na Serikali kuja nchini kufanya mazungumzo juu ya fidia ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) dhidi ya Tanesco ya Sh. bilioni 94, lakini serikali imekana kuhusika na ujio wake.
Al Adawi juzi akizungumza na baadhi ya wahariri wa magazeti, bila kuhusisha televisheni na redio, na akiwa amekataa kabisa kupigwa picha, alisema alikuwa amealikwa na serikali, lakini baadaye akabadili kauli na kusema kuwa alikuwa amealikwa na Tanesco.
Juzi Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, alikanusha shirika hilo kumualika Al Adawi na kusema kama kweli alikuwa nchini basi atakuwa amealikwa na serikali.
Jana Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Aloyce Tesha, alikana serikali kumualika Al Adawi na kuliambia NIPASHE kuwa kama mmiliki huyo amekuja basi ni kwenye mambo yake na kama kuna waliomwalika serikali haina taarifa zake.
“Huyu mtu ana rasilimali zake hapa nchini sasa kama amekuja kuangalia mitambo yake tutajuaje, sisi hatuhusiki kabisa na ujio wake, kama kuna waliomwalika kawaulize, lakini sisi Wizara tumwalike wa kazi gani?” alihoji Tesha.
Katika mkanganyiko huo, wito wa kumuhoji mmiliki huyo unatakiwa kuzingatia sheria ya uhujumu uchumi na sheria nyinginezo kutokana na maelezo tata yaliyotolewa mpaka sasa kuhusiana na kampuni yake, yaani Dowans Holdings SA iliyosajiliwa nchini Costa Rica na Dowans Tanzania Limited.
Ushauri wa kumkamata Al Adawi ulitolewa jana na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini wa Kambi ya Upinzani.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Mnyika alisema Februari 16, 2011 alitoa tamko la kutaka serikali iitaifishe mitambo ya kuzalisha umeme ya Dowans iliyopo jimboni Ubungo na kuiwasha kama sehemu ya kupunguza makali ya mgawo wa umeme unaolikumba taifa kwa sasa.
“Katika tamko hilo nilitoa mwito kwa wamiliki wa Dowans popote walipo duniani kujitokeza hadharani iwapo wana sababu za kuepusha mitambo yao isitaifishwe,” alisema.
Siku chache baada ya tamko hilo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alinukuliwa na gazeti moja la kila siku (siyo NIPASHE) Februari 18, 2011 akisema kwamba serikali haitataifisha mitambo ya Dowans kwa kuwa hiyo siyo sera ya CCM.
Aidha, alisema Februari 20, 2011 amejitokeza Al Adawi aliyejitaja kuwa ndiye mmiliki mkuu wa makampuni ya Dowans na kueleza kwamba yuko tayari kukutana na Tanesco kuhusu madai ya fidia ya ICC pamoja na majadiliano ya kuzalisha umeme kama ambavyo ilinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari jana.
Mnyika alisema kuwa alitarajia kuwa mmiliki wa Dowans ambaye angejitokeza angekiri hadharani kama wamedanganywa na kampuni ya Richmond na vyombo vingine katika kuhamishiwa mkataba ili kuweka msingi muhimu wa majadiliano, lakini imekuwa tofauti.
Alisema kuwa itakumbukwa kuwa Machi mwaka 2009, Al Adawi alinukuliwa na gazeti moja la wiki nchini alikaririwa na gazeti moja la wiki nchini kuwa yeye si mmiliki wa Dowans kama alivyonukuliwa katika mahojiano na KLHN.
“Kama amekuwa akikanusha kuwa ni mmiliki, lakini sasa amejitokeza kuwa ndiye mmiliki, kuna kila sababu ya vyombo vya dola kumuhoji zaidi,” alisema Mnyika katika taarifa yake na kuongeza:
“Aidha, vyombo vya dola vimuhoji kuhusu utata kuhusu kampuni ya Dowans Holdings SA ambayo kumbukumbu zake kamili hazipo Costa Rica inapoelezwa kusajiliwa na kuwa na ofisi zake. Kwa kuwa sasa wanaotajwa kuwa wamiliki wa Dowans wameanza kujitokeza, ni muhimu pia wamiliki wa kampuni ya Portek Systems and Equipment PTE Ltd ambayo inatajwa kumiliki hisa takribani asilimia 40 kwenye Dowans wakatajwa na wakajitokeza.”
Mbunge huyo alisema kadhalika, kwa kuwa Waziri Ngeleja hakumtaja Al Adawi wakati anawataja aliowaita wamiliki wa Dowans Januari mwaka huu, ni muhimu Waziri akaeleza iwapo Wizara yake ambayo ndiyo inayosimamia pia kisera Tanesco ambayo Al Adawi anataka kufanya majadiliano nayo kama inamtambua kuwa ni mmiliki wa kampuni ya Dowans.
“Katika mazingira haya ya utata wa Dowans na hali tete ya umeme pamoja na mvua ambazo zimeanza kunyesha katika maeneo yenye mabwawa ya kuzalisha umeme, bado kuna umuhimu wa serikali kutafakari kuitaifisha mitambo hiyo na kuchukua hatua stahiki dhidi ya ukiukwaji wa sheria uliojitokeza ili kuepusha pia kasoro nyingine kujitokeza katika hatua za dharura nyingine ambazo serikali inakusudia kuzichukua hivi sasa.
“Kutaifisha mitambo ya Dowans sio kutekeleza sera ya chama chochote, bali ni kuzingatia maslahi ya taifa na kusimamia utawala wa sheria ikiwemo sheria ya uhujumu uchumi,” alisema.
Mnyika alikumbusha kuwa katika tamko lake la Februari 16, 2011 pamoja na kuitaka serikali kutaifisha mitambo ya Dowans kwa kutumia sheria ya uhujumu uchumi na sheria nyinginezo, alieleza kuwa wakati mjadala kuhusu MW 120 za Dowans ukiendelea na kwa kuwa kiasi hicho hakiwezi kuziba pengo la takribani MW 240 ambalo linalolikabili taifa hivi sasa, ni muhimu kwa Waziri Ngeleja kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua ambayo serikali inataka kuchukua ya kukodi mitambo ya MW 260.
Aidha, katika tamko hilo, Mnyika alimtaka Ngeleja atoe ufafanuzi wa kutokukamilika kwa mipango ya serikali wakati ambapo dharura ya umeme ilijulikana toka mwaka 2002, serikali ikaijadili kwa kina mwaka 2006, Bunge likapitisha maazimio mwaka 2008 na serikali ikaahidi tena mwaka 2009 kuweka utaratibu wa kukabiliana na dharura hiyo.
“Kwa kuwa Bunge halikupata wasaa wa kujadili dharura ya umeme kama nilivyotarajia, bado natarajia kutoa tamko la kina hivi karibuni kwa nafasi yangu ya uwaziri kivuli kuhusu suala la umeme kwa kuzingatia hali ya mgawo inavyoendelea sambamba na kupanda kwa gharama za nishati hiyo kunakoongeza ugumu wa maisha kwa Watanzania walio wengi baada ya majadiliano na baraza kivuli na mamlaka nyingine husika,” alieleza Mnyika.
SERIKALI YAONGEZA MSUMARI WA MOTO
Katika ufafanuzi wa Tesha kwa gazeti hili, alisema serikali haikumwalika Al Adawi na haihusiki kwa namna yoyote na ujio wake.
Alipoulizwa kuwa mmiliki huyo ameshazungumza na wizara hiyo na kukubali kupunguza deni lake ili mitambo ya Dowans iwashwe, Tesha alisema hakuna kitu kama hicho.
“Iliyohukumiwa ni Tanesco si Wizara ya Nishati na Madini, kwa hiyo kama wanadaiana wamalizane wenyewe huko na Tanesco sisi hilo jambo halituhusu na haliko kwetu,” alisema Tesha.
Katika mkutano na wahariri juzi, Al Adawi alisema anafanya biashara ya mabilioni katika nchi mbalimbali duniani, lakini hana kawaida ya kujitokeza katika vyombo vya habari.
Alilalamika kuwa vyombo vya Tanzania ndivyo vimemfanya aibuke kwa kuwa vinapotosha suala la Dowans, hivyo kuvunja mwiko wake.
Alisema anamiliki hisa nyingi katika kampuni ya Dowans Tanzania Ltd na Dowans SA na amekuja nchini mahsusi kwa ajili ya kushughulikia upotoshwaji na uwakilishi usio sahihi vyote vikilenga Dowans na kujua kama kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano kuhusu mambo yaliyopo sasa.
Alisema amekuja kwa mwaliko wa Tanesco, ingawa hakuweka bayana kuwa ameshakutana nao na kufanya mazungumzo.
JANUARy MAKAMBA: AIPIGIA DEBE MITAMBO YA DOWANS
Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema itaishauri serikali ifanye mazungumzo na kampuni ya Dowans ili iwashe mitambo yake kwa ajili kuzalisha umeme na kutatua tatizo linalolikumba taifa hivi sasa.
Kauli hiyo ilitolewa tena jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Januari Makamba, baada ya kukutana na wafanyabiashara wenye viwanda nchini na wadau wanaotumia umeme mwingi kwa ajili ya uzalishaji.
Alisema suala la kuwasha mitambo hiyo lipo chini ya serikali na wao kama kamati wanachoweza kufanya ni kutoa ushauri namna wanavyoona ili kukabiliana na tatizo hilo.
Aliongeza kuwa alishawahi kusema kwamba inaweza kutumika sheria ya kuhujumu uchumi ili kutaifisha mitambo hiyo, lakini hivi sasa jukumu hilo lipo kwa serikali ambayo inaweza kukaa na Dowans ili kufikia mwafaka.
Makamba alipuuzwa kutolea ufafanuzi wa kauli ya Tanesco, kwamba tatizo la mgawo wa umeme litamalizika kwa kudra za Mwenyezi Mungu, alisema kuna njia nyingi zinazoweza kutumika katika kupata ufumbuzi wa suala hilo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment