ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 22, 2011

Ushirikina wasababisha aishi kanisani

MWANAMKE mkazi wa Kijiji cha Kikondo Mwela kilichopo wilayani Mbeya, amelazimika kuishi uhamishoni katika Kanisa la Living Covenant Global lililopo eneo la Mwanjelwa jijini Mbeya baada ya wakazi wa kijiji chake kumzuia asirudi kijijini kwao kwa sababu za uchawi. 

Judith Juma (24) anaishi kanisani hapo tangu Februari 12 alipofika akitokea kijijini kwao alikofukuzwa na wanakijiji wenzake kwa kujihusisha na masuala ya ushirikina. 


Akizungumzia tukio hilo, Judith alisema, wanakijiji wenzake walikuwa wakimtuhumu kuwa anahusika kuharibu mimba au kuchukua vipawa vya watoto wachanga kijijini hapo na kuvipoteza. 

Hata hivyo, alikiri kuhusika na matukio hayo, lakini akafafanua kwamba alikuwa akitumwa na watu hivyo baada ya kuona tabia hiyo haina manufaa, aliamua kwenda kanisani hapo ili aombewe na kutubu. 

Alisema, baada ya kufika kanisani, alipokewa na Mchungaji Jack Mwakindile aliyemwombea na kuiondoa roho aliyokuwa nayo, lakini kabla ya kurejea kijijini kwao wanakijiji wenzake wakamtumia ujumbe kupitia kwa mumewe, Mawazo Solo kuwa hapaswi kurejea kijijini. 

“Baada ya taarifa hiyo inayoonyesha wanakijiji wenzangu kutokuwa na imani na mimi nimeshindwa kurejea kwangu na sasa nalazimika kuishi hapa kanisani. Nawaomba wanakijiji wenzangu watambue kuwa kwa sasa mimi si mwanamke yule waliyekuwa wakimjua. Nimebadilika na ni mtu safi hivyo waniruhusu kurejea kwangu,” alisema Judith. 

Kwa upande wake, Mchungaji Mwakindile aliwaomba wanakijiji wampokee mwanamke huyo akisema kwa sasa amebadilika na hawezi kurudia kufanya vitendo vya kishirikina alivyokuwa akishiriki. 

Wakati huo huo, wananchi katika eneo la soko la Sido lililopo Mwanjelwa mwishoni mwa wiki, walivunja kibanda cha biashara cha Poa Mwanyerere (60) mkazi wa Makunguru kwa madai ya kuhusika na ushirikina. 

Ilidaiwa kuwa mama huyo ambaye shughuli yake ni biashara ya chai sokoni hapo, anahusika na kifo cha mmoja wa wafanyabiashara aliyekuwa wanapakana naye kilichotokea mwishoni mwa mwaka jana na kwa sasa kuna mfanyabiashara mwingine aliyeugua ghafla baada ya kurushiana maneno naye. 

Katika tukio la kubomoa kibanda chake mwanamke huyo aliokolewa na askari Polisi wa Kituo cha Mwanjelwa walioamua kumtoa sokoni hapo na kumpeleka kituoni.



CHANZO:HABARI LEO

No comments: