
MBOWE, KAFULILA WAMSHANGAA KUTOFAHAU WAMILIKI WA KAMPUNI HIYO
Boniface Meena naRaymond Kaminyoge
HOTUBA ya Rais Jakaya Kikwete imeibua mjadala mpana baada ya baadhi ya wanasiasa, wasomi na wanaharakati kumpongeza huku wengine wakimkosoa kutokana na kile walichokiita ni kauli yake tata ya kutowafahamu wamiliki wa Dowans na kutaka aitishe kikao cha Baraza la Mawaziri na kutangaza kutoilipa kampuni hiyo tata.
Boniface Meena naRaymond Kaminyoge
HOTUBA ya Rais Jakaya Kikwete imeibua mjadala mpana baada ya baadhi ya wanasiasa, wasomi na wanaharakati kumpongeza huku wengine wakimkosoa kutokana na kile walichokiita ni kauli yake tata ya kutowafahamu wamiliki wa Dowans na kutaka aitishe kikao cha Baraza la Mawaziri na kutangaza kutoilipa kampuni hiyo tata.
Juzi akizungumza na wana-CCM wakati wa maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa chama hicho kikongwe Afrika, pamoja na kuelezea mlolongo mrefu kuanzia Richmond aliyoiita "Phantom Company,' Rais Kikwete aliweka bayana, "Sina hisa Dowans, wala wamiliki wake siwajui na hawajawahi kuniita kwasababu hawanihitaji."
Hata hivyo, msimamo huo wa Rais kujivua tuhuma hizo za kuwa mmoja wa wamiliki wa Dowans zilizoelekezwa kwake na Dk Willibrod Slaa, bado haujamnasua baada ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kushangaa kauli hiyo wakati Serikali ya Awamu ya Nne ndiyo iliyoingia mkataba na kampuni hiyo.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, alifafanua kwamba kitendo hicho cha Rais Kikwete ni hadaa kwa wananchi akifikiri wanataka kujua uhusiano wake na wamiliki hao.
"Ni kazi ngumu sana kulinda uongo, Rais anasahau kwa jinsi gani Richmond na Dowans zilivyoisumbua Serikali yake hivyo kama anasema hajui basi hafai kuwa Rais wa nchi,"aliweka bayana Mbowe.
Mbowe alisisitiza kwamba, Rais wa nchi si mtu anayepaswa kulalamika bali ni mtu wa kuchukua hatua.
"Ni aibu kwake kunung'unika badala ya kuchukua hatua, ni lazima ajue anapozungumza kwenye vikao vya CCM ajue bado ni Rais wa nchi,"alisema Mbowe.
Kuhusu onyo la Rais kuhusu wanaochochea migomo na maandamano kwa kudai kile alichokiita madaraka waliyokosa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Mbowe alisema mkuu huyo wa nchi aache madai hayo akimtaka atambue kila mtu ana haki ya kudai kile anachoona ni haki yake.
Mwenyekiti huyo wa Chadema aliongeza kwamba, kuandamana ni haki ya watu hivyo kama Rais hataki kuwepo kwa maandamano afute haki hiyo ili wananchi wajue haipo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (TCID), Deus Kibamba alisema kauli aliyoitoa Rais Kikwete juzi ilikuwa ni maoni yake binafsi.
“Tunataka Rais Kikwete aitishe kikao cha Baraza la Mawaziri, ili kitoe msimamo mmoja wa Serikali wa kukataa kuilipa kampuni ya Dowans,” alisema.
Alisema kauli ya Rais kwamba, ni mmoja kati ya watu wanaotaka Tanesco isiilipe kampuni ya Dowans, ilikuwa ni maoni yake binafsi.
“Tunataka msimamo wa Serikali, tunataka uamuzi wa Baraza la Mawaziri, mawaziri wamepingana kuhusu Dowans kwa sababu hakuna kikao kilichowahi kufanyika,”alirejea kauli na msimamo huo uliowahi kutolewa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Kibamba alifafanua kwamba, baada ya kikao hicho, ndipo mawaziri na wanasheria wanatakiwa kuweka mikakati ya namna wanavyoweza kuinusuru nchi na ulipaji wa fidia hiyo.
Tayari kauli ya Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa na kusimamia Serikali kuwaadhibu waliohusika Richmond na kisha kuvunja mkataba wa Dowans, inapingana na msimamo wa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliyetangaza kwamba, Serikali lazima iilipe kampuni ya Dowans fidia ya Sh 94 milioni.
Mwanasheria Mkuu wa serikali (AG) Frederick Werema, naye aliangukia katika kundi hilo la Ngeleja akisema deni hilo halikwepeki kauli ambayo ilipingwa si tu na Sitta, bali pia Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe huku wanaharakati kwa upande wao wakifungua kesi Mahakama Kuu kutaka shauri hili litolewe uamuzi nchini na kuanisha hoja 16 za kwanini kampuni hiyo isilipwe.
Kafulila adai JK hawajui Dowans, Ngeleja anawajua
Kwa upande wa mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi, David Kafulila, alimshangaa Rais Kikwete kusema hawajui wamiliki wa Dowans wakati waziri wake Ngeleja alikwishawataja.
“Ngeleja alikwishawataja wamiliki wa Dowans, inakuwaje Rais anasema hawafahamu..., suala hili linazidi kuwachanganya wananchi, inabidi likajadiliwe bungeni,”alirejea msimamo wa hoja yake anayotarajia kuiwasilisha bungeni kama ikikubaliwa.
Kafulila alifafanua kwamba, suala hilo likijadiliwa bungeni ndipo linaweza kutoa majibu sahihi kwa wananchi.
“Kwa ujumla Rais Kikwete kusema hawajui wamiliki wa Dowans ni kielelezo kuwa wale tuliotangaziwa na Waziri Ngeleja sio wenyewe kwani wangekuwa wamiliki Rais angewajua,” alisema Kafulila na kuongeza:
Je waziri wake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliposema lazima tulipe Dowans hawakumwambia wanamlipa nani?
Alisema katika sakata hili ataendelea kupigana hadi ijulikane nani amefikisha taifa katika hali hii. “Serikali ilipe isilipe ni lazima iwajibike maana hoja ya msingi hapa tumefikishwaje hapa hadi kushindwa kesi,” alihoji Kafulila
Mwanasheria maarufu, Profesa Abdallah Safari alisema Serikali inazidi kuwachanganya wananchi kwa namna vigogo wanavyotofautiana kuhusu suala hilo.
“Rais kuwa upande wa wanaopinga kuilipa kampuni hiyo ni jambo jema, lakini inasikitisha kuona mawaziri wanapingana hadharani, hakuna msimamo wa pamoja, Baraza la Mawaziri likae ili kutoa msimamo wa Serikali.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema ni jambo la busara kutafuta njia mbalimbali za kisheria ili fidia hiyo isilipwe.
“Kuna mambo mawili ya kuangalia tunapojadili suala hili..., ni vizuri tukitafuta njia za kutuokoa kulipa fedha hizi, lakini tukumbuke tukishindwa tutatozwa fedha zaidi ambazo ni asilimia 7.5,”alisema.
Kuanzia siku hukumu ilivyotoka, faini ya Dowans imeongezeka hadi kufikia Sh97 bilioni kutokana na riba ya Sh20milioni kwa siku.
Mkataba wa Dowans na Tanesco ulivunjwa Agosti 31 mwaka juzi, baada ya Bunge kuagiza uvunjwe baada ya kuibuka sakata la Kampuni ya kufua umeme ya Richmond mwaka 2008, l ililomfanya Edward Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu na Baraza la Mawaziri likavunjwa.
No comments:
Post a Comment