Advertisements

Wednesday, February 23, 2011

Maandamano makubwa CHADEMA Mwanza

*Ni kupinga malipo Dowans, kupanda gharama za maisha

Na Waandishi Wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinatarajia kuanza kutekeleza agizo la Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, kufanya maandamano na
mikutano kesho, ikiwa ni ishara ya kupinga mambo kadhaa, ikiwemo mgawo na ongezeko la bei ya umeme kwa kuwa yameongeza ugumu wa maisha ya kila siku kwa Mtanzania.

Kwa mujibu wa viongozi wa juu wa CHADEMA, Mwenyekiti wa taifa, Bw. Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dkt. Willibrod Slaa pia watazungumzia matukio kadhaa yanayotokea nchini ikiwemo suala la milipuko katika kambi za jeshi, hasa tukio la karibuni la mlipuko katika kambi ya Gongolamboto.

“Kwa kifupi niseme tunatarajia kuanza kampeni yetu ya maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima wiki hii kama tulivyoahidi. Tunaanzia mikoa ya Kanda ya Ziwa na kituo cha kwanza kitakuwa Mkoa wa Mwanza na baadaye mikoa mingine. Tutazungumzia mambo mengi yenye maslahi kwa taifa letu,” alisema Dkt. Slaa.


Akizungumza mara baada ya kuahirishwa kwa kesi ya kufanya kusanyiko bila kibali inayowakabili viongozi kadhaa na wanachama wa Chama hicho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Dkt. Slaa alisema watatumia mikutano hiyo kuwaeleza wananchi
ukweli wa tukio la mauaji ya Arusha ili kuzuia upotoshaji unaofanywa na serikali kupitia vyombo na idara zake mbalimbali.

Wakati serikali kupitia jeshi la polisi na mamlaka zingine imekuwa ikielezea tukio hilo na kukitupia lawama chama hicho kwa vurugu zilizosababisha mauaji hayo Januari 5, mwaka huu, CHADEMA nao kwa upande wao wamedai kukusanya ushahidi ukiwemo wa kielektroniki kuthibitisha kuwa mauaji hayo yalipangwa na kutekelezwa na polisi kwa makusudi kwa shiniko la wanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa pande wake, Bw. Mbowe alisisitiza kuwa CHADEMA haitapumzika katika kudai mabadiliko na mambo ya msingi yanayohusu maisha ya Watanzania na kutamba kuwa hakuna nguvu yoyote, iwe ya dola, mabomu wala risasi itakayozuia hamu ya mabadiliko inayotakiwa na umma wa watanzania.

“Hakuna njia ya kuzuia mabadiliko yanayotakiwa wa umma, CHADEMA kama tulivyoanza tutaongoza kampeni kudai mabadiliko yenye tija na maslahi kwa nchi bila kujali tofauti za kiitikadi za vyama. Maisha magumu yanayowakabili Watanzania kwa sasa haubagui, wote wamepigika sawa sawa. Lazima tuungane sote kudai maisha bora
tunayoahidiwa kila siku bila utekelezaji,” alisema, Bw. Mbowe.

Akifafanua alisema mateso wanayopata Watanzania yanasababishwa na viongozi walioko madarakani kukosa utashi wa kisiasa kuyakabili na kutolea mfano mfumuko wa bei unaosababisha bidhaa kupanda bei kila kukicha wakati uwezo wa kununua kwa mwananchi wa kawaida ukipungua huku viongozi wakipita na kutamba kuwa uchumi umekua na
kuimarika.

“Watanzania hawahitaji uchumi unaokuwa kwenye makaratasi na takwimu za wataalamu. Kinachotakiwa ni ukuaji huo kuonekana katika maisha ya kila siku ya mwananchi wa kawaida na hii inahusu uwezo wa kununua bidhaa na mahitaji muhimu. Uchumi utakuaje wakati mtu hana uhakika wa bei ya sukari dukani kwani inapanda kila siku licha
kujengwa viwanda vingi vya sukari nchini kuliko kipindi kingine chochote?.

"Mwaka 2005 wakati rais Kikwete anaingia madarakani, bei ya kilo moja ya sukari ilikuwa sh. 600. Lakini kiasi hicho kwa sasa kinauzwa kati ya sh. 1,700 hadi 2,000 ambayo ni karibia ongezeko la asilimia 150 ndani kipindi cha miaka sita tofauti na kipindi cha awamu ya tatu chini, Bw. Benjamin Mkapa ambapo bei ya bidhaa
ilidhibiti kwa karibu miaka yote kumi aliyokaa madarakani.

"Pamoja na sukari baadhi ya bidhaa zingine za mahitaji ya kila siku zilizopanda bei mara dufu na bei za zamani na mpya kwenye mabano ni pamoja na paketi moja ya kiberiti (sh. 20 hadi 50), kipande cha sabuni (sh. 100 hadi 350), pakiti moja ya chumvi (sh. 50 au 100 hadi sh. 200 au 300), kilo moja ya nyama ya ng’ombe (sh.
2,000 hadi 4,000 au 5,000). Hii ni mifano michache kwani orodha ni ndefu," alisema.

Wakati hali ikiwa hivyo, makusanyo ya serikali kutokana kodi mbalimbali imeongezeka kutoka sh. bilioni 250 kwa mwezi hadi zaidi ya bilioni 400 na hivyo kuipa nguvu hoja kuwa tatizo siyo fedha bali utashi wa viongozi na mipango ya vipaumbele vya taifa katika matumizi ya serikali na haya ni baadhi ya mambo ambayo CHADEMA wameahidi kufafanua na kuyahainisha katika kampeni yao nchi nzima.

Hivi karibuni akitoa taarifa ya CC kwa waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa alisema kuwa mbali ya kuwahimiza wana-CHADEMA, wabunge na wananchi kwa ujumla kuendelea kupinga kwa nguvu zote malipo ya Dowans, CC ya chama hicho pia iliagiza sekretarieti kuanza maandalizi ya maandamano ya nchi nzima kupinga ongezeko la bei ya umeme, gesi na malipo kwa Dowans yatakayoanzia jijini Mwanza, Februari 24, mwaka huu.

"Kamati kuu imesikitishwa na kupanda holela kwa bei ya nishati muhimu ya umeme na gesi, pamoja na kushindwa kwa serikali ya CCM katika kuwekeza kikamilifu katika sekta ya nishati hapa nchini," alisema Dkt. Slaa.

Akizungumza na Majira jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Bw. Erasto Tumbo, alisema wataanza kwa maandamano jijini Mwanza, yatakayofuatiwa na mkutano katika viwanja vya Furahisha, kisha katika wilaya za mkoa huo.

"Kesho yake tutasambaa na kufanya mikutano katika wilaya zote za Mkoa wa Mwanza. Mikutano hiyo itafanyika pia kwa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, baada ya Mwanza, itafuata Shinyanga, kisha Mara halafu Kagera, kwa staili hiyo hiyo ya kufanya mkutano makao makuu ya mkoa kisha katika wilaya zote za mkoa husika," alisema Bw. Tumbo.

Aliongeza "tunawaomba Watanzania wote wajitokeze kwa wingi katika kila eneo husika, tutafanya maandamano ya amani, tayari tumeshatoa taarifa kwa polisi, hivyo hatuna mgogoro nao tena, na kwa sababu tumetoa muda mrefu bila shaka taarifa za kiintelijensia watakuwa wameshafanyia kazi ili kuhakikisha kuwa raia na mali zao wanalindwa."

Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha, imeamuru kesi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA isijadiliwe nje ya mahakama hata kama inawahusu viongozi wakuu wa kitaifa wa chama hicho.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Arusha, Bw. Charles Magesa alisema hayo jana wakati akizungumzia hoja zilizotolewa mahakamani hapo na mawakili wa upande wa utetezi na upande wa washtakiwa. 

Bw. Magesa alikubaliana na hoja ya wakili wa upande wa utetezi na kutoa onyo kwa wale wote wanaoeleza masuala ya mahakamani nje ya mahakama.

“Mahakama hii, inatoa onyo kuacha mara moja kwa mtu yoyote kuzungumzia kesi iliyopo mahakamani, kwani wanaofanya hivi wanajua wazi sheria zinakataa na hata wale wanaotoa vielelezo kwenye vyombo vya habari, nao waache mara moja, kwa kuwa wanavunja sheria,” alisema Bw. Magesa.

Imeandikwa na Tumaini Makene, Peter Saramba na Glory Mhiliwa


CHANZO:MAJIRA

No comments: