Mapigano makali yanaarifiwa kutokea katika maeneo matatu nchini Somalia.
Mwaandishi wa BBC anasema haya ni mapigano makali kabisa kati ya majeshi ya serikali na wapiganaji wa kundi la wanaharakati wa kiislamu la Al-Shabab, katika mji mkuu, Mogadishu, katika kipindi cha miezi michache iliyopita.
Vikosi vya serikali vikisaidiwa na wanajeshi wa Muungano wa Afrika, inasemekana vimeiteka ngome kuu ya al-Shabaab .
Kuna taarifa za kutokea mapambano katika mji wa Beledweyne kwenye mpaka wa Ethiopia na Bulahawa, na kwenye mpaka na Kenya.
Mapigano makali ya mjini Mogadishu yaliendelea siku nzima Jumatano.
Wanajeshi kutoka Burundi ambao ni sehemu ya jeshi la Muungano wa Afrika wamekuwa wakipigana bega kwa bega na wanajeshi wa serikali hiyo ya mpito ya Somalia.
Wamefanikiwa kuyateka maeneo ya wapiganaji wa Al Shabab baada ya kusonga mbele mtaa kwa mtaa.
Eneo liliotekwa ikiwemo iliyokuwa wizara ya ulinzi ni dogo lakini ni muhimu katika mikakati ya kijeshi.
Kundi la Al Shabab pia limekabiliwa na shinikizo katika mji wa Beledweyne kwenye mkoa wa kati wa Somalia ambako wanajeshi wa serikali na wanamgambo washirika wamekuwa wakifanya mashambulizi.
Katika medani ya tatu ya mapigano Bula Hawo karibu na mpaka wa Kenya wapiganaji wanaohusishwa na kundi la Al Qaeda walishambuliwa na kundi jingine la wanamgambo wanaoiunga mkono serikali.
Ingawa mpaka huo umefungwa rasmi , wakazi wamekuwa wakikimbia mapigano ya huko na kuelekea mji wa Mandera nchini Kenya.
Rais wa Somalia, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed alihutubia waandishi wa habari mjini Mogadishu.
Rais wa Somalia, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed alihutubia waandishi wa habari mjini Mogadishu.
Akiwa amevalia sare ya kijeshi , aliwasifu wanajeshi wa serikali na kusisitiza kwamba mashambulio hayo katika maeneo tofauti yameratibiwa.
Jeshi la Muungano wa Afrika na wanajeshi wa serikali wanazungumzia kuendelea kulivunja nguvu kundi la Al Shabab, hata hivyo kundi hili la msimamo mkali wa kiislamu bado linadhibiti maeneo makubwa ya nchi na linaweza kusababisha vurugu kubwa.
Siku ya Jumatatu bomu liliotegwa ndani ya gari liliwaua watu wasiopungua 17 karibu na kituo cha mafunzo ya polisi mjini Mogadishu.
No comments:
Post a Comment