ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 18, 2011

Mwape airejesha Yanga kileleni

Mshambuliaji Davis Mwape alifunga goli lake la sita katika mechi nne za Ligi Kuu ya Bara msimu huu na kuisaidia Yanga kurejea kileleni mwa msimamo katika ushindi 1-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba jana.
Mzambia huyo aliyejiunga na Yanga katika kipindi cha usajili cha Januari maarufu kama "dirisha dogo" alifunga goli hilo katika dakika ya 7 na likadumu kwa dakika zilizobaki za mchezo huo uliojaa ushindani.
Hata hivyo, Yanga kwa mara nyingine watalazimika kupongeza kazi nzuri ya kipa Mghana, Yaw Berko aliyeokoa hatari kadhaa ikiwamo ya dakika ya 65 kutoka kwa mshambuliaji wao wa zamani, Gaudence Mwaikimba aliyebaki na mlinda mlango huyo kabla ya kupiga shuti lililopanguliwa na kuinyima Kagera Sugar goli la kusawazisha.
Kwa ushindi huo, Yanga imerejea kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 35, moja zaidi ya Simba iliyoshikiliwa juzi katika sare ya 2-2 ugenini kwa Toto African jijini Mwanza. Hata hivyo, Simba ina mechi moja mkononi. Azam FC iliyocheza mechi 16 sawa na Yanga, iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 32.
Kulikuwa na kosa kosa kadhaa za wazi jana ukiacha ya Mwaikimba, ambapo mshambuliaji wa Yanga, Jerryson Tegete alikuwa na nafasi ya kuifungia timu yake goli la pili katika dakika ya 33 lakini alishindwa kulenga lango akiwa amebaki peke yake na kipa baada ya 'gonga' safi iliyofanywa baina ya Davis Mwape na Kigi Makasi kabla ya mpira kumfikia Tegete.
Godfrey Taita aliyekuwa akiiandama ngome ya wageni, alikaribia kufunga katikati ya kipindi cha pili lakini beki wa kati wa Yanga, Chacha Marwa alitokea na kuokoa vizuri kabla mpira haujamfikia kipa Yaw Berko, ambaye kwa mara nyingine tena alidaka kwa kiwango cha juu na kuiepushia timu yake kipigo.
Wenyeji walifanya mabadiliko kadhaa kwa kuwaingiza Sunday Frank, Paul Ngwai na Juma Seif badala ya George Kavila, Jumanne na Mohammed Dilunga lakini mabadiliko hayo hayakuwasaidia wakati Yanga iliyowaingiza Omega Seme badala ya Razak Khalfani katika dakika ya 87 na Idd Mbaga badala ya mfungaji Davis Mwape (dk.90) walionekana mabadiliko yao yalikuwa ni kwa ajili ya "kula" muda.
Kipa Berko alilimwa kadi ya njano kwa kosa la kupoteza muda katika dakika ya 83.na kiungo Kigi Makasi walilimwa kadi za njano baada ya mchezea rafu Mwaikimba.
CHANZO: NIPASHE

No comments: