
Kila sifa njema anastahili Mungu muweza wa yote. Imekuwa furaha kukutana leo katika siku hii ya wapendanao, Valentine’s Day. Leo nitakupa mawazo sahihi ya jinsi ya kufurahia siku yenyewe.
Muhimu ni upendo. Valentine’s Day haitakuwa na amani kwako ikiwa bado upo kwenye mgogoro na mwandani wako. Tumia thamani ya siku ya leo, kurejesha mahaba yaliyofifia.
Muhimu ni upendo. Valentine’s Day haitakuwa na amani kwako ikiwa bado upo kwenye mgogoro na mwandani wako. Tumia thamani ya siku ya leo, kurejesha mahaba yaliyofifia.
Inawezekana unaona ni uzungu lakini ukweli ni kwamba kila kitu kinahitaji maadhimisho. Siku ya mahaba ulimwenguni kote ni Valentine’s Day. Tusipingane na ukweli, tujumuike pamoja.
Upo na mwenzi wako. Mnakutana kila siku, inafikia kipindi mnazoeana. Inapendeza kuwepo na siku ambayo itakuwa inawakumbusha nyuma na kurejesha upya mawazo yenu katika siku za mwanzo za uhusiano. Itumie Valentine’s Day vizuri.
WAJIBU WA VALENTINE’S DAY
Kuna kitu kinakosewa. Wanaume wengi huishi kama ‘maroboti’, ni wao ndiyo wanaoitumikisha mifuko yao kununua maua na chokoleti au zawadi nyingine zozote kwa ajili ya wapenzi wao.
Swali la kujiuliza ni hili: Wajibu wa mwanamke kwa mwenzi wake ni upi? Kila mmoja anahitaji kuboresha upendo, kwa hiyo ni vyema kwa wanawake nao kujituma katika kuwajali na kuwafurahisha wenzi wao.
Tatizo lingine ambalo linasababisha kukosewa kwa mantiki ya Valentine’s Day ni kitendo cha watu wengi kutoka na wenzi wao kwenda maeneo mbalimbali kwa kulazimishwa, yaani si kwa matakwa yao kwenda kusherehekea.
Hapa kuna njia chache ambazo zitakuwezesha kusherehekea Siku ya Wapendanao kwa hamasa ya kimahaba na ubunifu.
ANGALIZO
Wengi wanadhani Siku ya Valentine ni kuingia benki na kuchota fedha za kutumia. Hiyo siyo kweli. Tafsiri yake ni upendo, aliye nacho na kapuku, wote wanaweza kujumuika na kujenga misingi imara ya uhusiano wao.
1. CHAKULA KIZURI CHA JIONI KINATOSHA
Badala ya kwenda safari za mbali ambako unaweza kugharamia usafiri na mambo mengine yatakayokutoboa mfuko, unaweza kuandaa chakula kizuri cha jioni nyumbani ambacho kitakuwa ‘sapraizi’.
Muhimu kuzingatia kwenye chakula hicho ni kuchagua kile mwenzi wako anachokipenda na ambacho ana muda mrefu hajakitumia. Kama jana alikula ubwabwa wa Kichina na leo ukamuwekea huo huo, hapo hakutakuwa na ‘uspesho’ wowote.
2. ANDAA MAUA
Kama unamudu kununua, basi tekeleza kwa ajili ya mwenzi wako. Ukishindwa, fanya kila uwezalo upate na umpe mwandani wako. Ni nafasi ya kumfanya mwenzi wako kujiona wa kipekee.
3. FANYA CHUMBA KIWE CHA MAHABA
Kama unajiweza kidogo, basi unaweza kukodi chumba hotelini halafu uingie mapema. Weka mishumaa na maua katika mpangilio mzuri. Mwisho mwalike na mpitishe usiku mkiwa sehemu hiyo yenye sura ya kipekee.
Kama huna uwezo wa kukodi chumba hotelini, basi ni vyema ukaking’arisha kile ambacho mnakitumia kila siku na kukiweka kwenye sura mpya itakayoleta kionjo cha kipekee.
POINTI NYINGINE MUHIMU
Siku ya Wapendanao inatakiwa kutumika kuwasilisha hisia zako za upendo kwa wale ambao unawajali sana. Hapa namaanisha kwamba unaweza kuonesha upendo wako hata kwa wazazi, ndugu wengine na marafiki ikiwa unaona ni sawa kufanya hivyo.
Mwisho nakutakia Sikukuu njema ya Valentine (Siku ya Wapendanao).
No comments:
Post a Comment