ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 5, 2011

Tanzania yaweka historia mpya UN-Mwananchi

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi, Dk Servacius Likwelile (kushoto), akiwasilisha Mpango wa Pamoja wa Maendeleo Katio ya Tanzania na Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa (UN), kwenye vikao vya bodi tendaji za mashirika hayo; UNDP, Unicef, WFP na UNFPA vinavyofanyika Makao Makuu ya UN, jijini New York, Marekani.
Mwandishi Maalum, New York, Marekani
TANZANIA imeweka historia kuwa nchi ya kwanza duniani kuandaa Mpango wa  Pamoja wa Maendeleo kwa kushirikiana na mashirika manne yaliyopo chini ya Umoja wa Mataifa (UN).

Mashirika hayo ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa  (UNDP),  Shirika la kuhudumia watoto (Unicef), Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika linalohusika na Idadi ya watu (UNFPA). 

Kufuatia kukamilishwa kwa mchakato huo wa aina yake, Jumuiya ya  kimataifa imeipongeza na kuisifu Tanzania kwa kuonyesha njia, na kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine.

Mpango huo ambao unajulikana kama Common Country Programme  Document (CCPD), Uliwasilishwa juzi kwenye bodi tendaji za UNDP na UNFPA na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Uchumi, Dk Servacius Likwelile. 
Bodi tendaji za mashirika hayo manne zinafanya mikutano ya kikazi  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, huku Tanzania ikipatiwa fursa ya kuwasilisha mpango huo.

Utekelezaji wa CCPD utafanyika kwa miaka minne kuanzia Julai mwaka huu hadi June 2015. Tanzania kupitia mpango huo itapata dola 773 milioni za Marekani zitakazotolewa na UN.

Dk Likwelile alisema maandalizi na utekelezaji wake umezingatia vipaumbele na mipango ya maendeleo, ambayo serikali zimeainisha kupitia Mpango wa Kupunguza na Kukuza Uchumi (Mkukuta) kwa Tanzania Bara na Mkuza kwa Zanzibar.

“ Ingawa tumeshirikiana na mashirika hayo tangu hatua zote za maandalizi hadi utekelezaji wake, huu ni mpango wetu, tunaumiliki wenyewe na tumehakikisha unakidhi vipaumbele ambavyo serikali zimejiwekea kuharakisha maendeleo ya wananchi wake,” alisema Dk Likwelile.

Kuhusu manufaa ya CCPD, Dk Likwelile alisema ni kuboresha utendaji kazi, utekelezaji, ufuatiliaji, ufanisi kwenye matumizi ya rasilimali fedha.

Manufaa mengine ni kujenga uwezo wa rasilimali watu ndani ya serikali  na wafanyakazi wa UN, ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto za kuleta maendeleo.

Kupitia  CCPD, sasa inakuwa rahisi kujua nani anafanya nini na katika eneo gani, na  itasaidia kupunguza muingiliano wa shughuli kati ya  shirika moja na jingine, huku serikali ikiaondokana na urasimu na ukiritimba wa kufanya kazi na shirika moja moja.

Maeneo yatakayonufaika na mpango huo ni mazingira, Ukimwi, elimu, afya, ukuaji uchumi, utawala bora na masuala ya wakimbizi.

 Bi Anne Webster kutoka Ubalozi wa Ireland, akizungumza kwa  niaba ya mataifa 17 anasema.
“ Kama marafiki wa  maboresho ya mfumo wa UM, na baada ya kufuatilia kwa makini mchakato wote huu.  Tumeridhishwa sana na kazi iliyofanywa. Tunapenda kutambua na kuipongeza Tanzania, kwa hatua hii ya kihistoria”

No comments: