.jpg)
Mshambuliaji Mrisho Ngassa alifunga goli lake la 12 na kuendelea kuongoza katika mbio za kusaka tuzo ya ufungaji bora msimu huu lakini klabu yake ilishindwa kupaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana.
Azam walikuwa na nafasi ya kuongoza katika msimamo wa ligi kwa tofauti ya magoli kama wangeshinda, lakini sare ya jana iliwaacha katika nafasi ya tatu waliyokuwa nayo awali baada ya kufikisha pointi 36, mbili nyuma ya vinara Yanga na pointi moja nyuma ya mabingwa watetezi, Simba.
Sare hiyo pia haikuwasaidia sana Majimaji baada ya kufikisha pointi 12 na kuendelea kubaki kwenye ukanda wa kuteremka daraja, pointi moja zaidi ya AFC ya Arusha wanaoburuza mkia baada ya kuambulia pointi 11 tu.
Azam walianza mechi ya jana kwa kasi na katika dakika ya nane, mshambuliaji John Bocco alipiga shuti kali lililogonga mwamba na kurejea uwanjani kabla ya kuokolewa na mabeki wa Majimaji.
Katika dakika ya 17, refa Judith Gamba aliwapa penati Azam baada ya kipa wa Majimaji Said Mohamed kumfanyia madhambi Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Ngassa akapiga shuti lililokwenda wavuni na kuipa timu yake goli la utangulizi lililodumu hadi mapumziko.
Majimaji walicharuka katika kipindi cha pili na Evarist Maganga akaisawazishia goli hilo kwa kichwa katika dakika ya 47, akitumia vyema krosi ya winga wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Ulimboka Mwakingwe.
Katika dakika ya 70, Ngasa alishindwa kuipatia timu yake goli la ushindi na pia kumuacha zaidi Gaudence Mwaikimba wa Kagera Sugar anayemfuatia kwa ufungaji akiwa na mabao 10 baada ya kumlenga kipa wa Majimaji, Said Mohamed wakati akiwa ana kwa ana na kipa huyo anayeidakia pia Taifa Stars.
Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa ambapo watani wa jadi, Simba na Yanga watavaana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE
i