Na Suleiman Abeid, Bukoba
PAMOJA na Rais Jakaya Kikwete juzi kuwaomba wananchi kususia maandamano yanayoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), maelfu ya
wakazi wa mji wa Bukoba na vitongoji vyake jana wamepuuza ushauri huo na wamejitokeza kwa wingi kushiriki maandamano hayo.
Hata hivyo msafara wa viongozi wa CHADEMA ukiongozwa na Katibu Mkuu wake, Dkt. Willibroad Slaa ulichelewea kuwasili mjini Bukoba kutokana na kiongozi huyo kukamatwa na kuhojiwa na polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga kwa saa kadhaa.
Polisi jana saa 1:15 asubuhi walimkamata Dkt. Slaa pamoja na wabunge wawili wa viti maalumu, Bi. Chiku Abwao na Bi. Rachel Mashishanga wakituhumiwa kwa kosa la kufanya mkutano katika eneo la Malampaka wilayani Maswa ambao haukuwa na kibali cha polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani alisema jeshi lake liliamua kumkamata Dkt. Slaa na wabunge wawili wa viti maalumu ambao walihojiwa kutokana na kitendo hicho cha kufanya mkutano katika eneo hilo bila kibali kwa kuwa wangeweza kusababisha kutokea kwa uvunjifu wa amani.
Kamanda Athumani alisema baada ya mahojiano ya takriban saa moja na robo viongozi hao waliachiwa na kuendelea na msafara wao kuelekea mkoani Kagera ambako waliendelea na ratiba yao kama kawaida.
Viongozi wa CHADEMA kwa upande wao walikanusha madai ya kuendesha mkutano pasipo kibali kwa vile kila mkoa wanakopita kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara hutolewa kibali kwa wilaya zote za mkoa husika.
Dkt. Slaa alisema anazo habari zilizodai kwamba kukamatwa kwao haikuwa sababu ya tatizo la kibali bali ni katika juhudi za kutaka kuvuruga ratiba za shughuli ya maandamano ya amani na mkutano mkubwa wa hadhara uliokuwa umeandaliwa kufanyika mjini Bukoba jana mchana.
Alisema mipango hiyo inatokana na shinikizo la Balozi Khamis Kagasheki, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi kutaka kukwamisha maandamano hayo yasifanyike katika jimbo lake, baada ya njama za awali za kuwazuia vijana waendesha pikipiki na baiskeli kushiriki katika maandamano
kukwama.
Mbali ya tukio hilo la kukamatwa kwa viongozi hao wa CHADEMA, maelfu ya wakazi wa mji wa Bukoba walijipanga kuanzia eneo la Kemondo Bay ambako ndiko walikowapokea viongozi hao na kuandamana kwa msafara wa magari, pikipiki na baiskeli hadi eneo la Rwamishenye ambako maandamano ya kutembea kwa miguu yalipoanzia.
Maandamano hayo yalipita katika mitaa mbalimbali ya mji wa Bukoba na kuishia katika uwanja wa Uhuru katikati ya mji huo ambako shughuli zote za kibiashara zilisimama kwa muda kabla ya Bw. Mbowe na Dkt. Slaa kuwahutubia wananchi waliojitokeza kwa wingi.
Akihutubia katika mkutano huo, Dkt. Slaa aliwashukuru wakazi wa mji wa Bukoba na vitongoji vyake kwa kupuuza wito wa Rais Kikwete na kujitokeza kwa wingi na pia kwa jinsi walivyoshiriki katika maandamano ya amani.
Alisema wakazi wa Bukoba wameonesha jinsi gani ambavyo wanakiunga mkono CHADEMA kwa vile ndicho chama ambacho hivi sasa kinaonesha wazi nia halisi ya kuwakomboa Watanzania katika kupigania haki zao.
Hata hivyo alisema amepata taarifa ya kufanyika kwa ziara ya Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda ambapo aliwaomba wajitokeze kwa wingi katika mkutano utakaohutubiwa na Bw. Pinda, na wamuulize kuhusu fedha za Watanzania zilizopotea katika mazingira ya kifisadi ikiwa ni pamoja na zile zilizochotwa na kampuni ya Meremeta zaidi ya sh. bilioni 155.
Ndugu zangu mimi nakupongezeni sana kwa jinsi mlivyotuunga mkono katika uchaguzi mkuu uliopita, pamoja na mlivyoshiriki katika maandamano ya amani na mkutano wa hadhara leo hii (jana) bila kujali vitisho vya Rais Kikwete.
Rais wetu ni mtu wa ajabu ni sawa na kinyonga, anasahau sana, awali alikuwa akivilaumu vyama vya upinzani kwamba haviendi vijijini ambako ndiko waliko wananchi, lakini leo tumekwenda anapata hofu na kutaka kutuzuia kwa kisingizio kuwa tunawachochea Watanzania kufanya vurugu,รข€ alieleza Dkt. Slaa.
Alisema CHADEMA haiwatii hofu Watanzania bali CCM na serikali yake ndiyo inayowatia hofu kutokana na kuwakumbatia matajiri wanaomiliki biashara zote kubwa na kupandisha bei za bidhaa ovyo na hivyo kupanda kwa bei za vitu kila siku na Watanzania kukabiliwa na ugumu wa maisha.
Alisema Rais Kikwete na waziri mkuu wake Bw. Pinda wanapaswa sasa kutoa majibu yote yanayoulizwa na Watanzania kuhusiana na ugumu wa maisha, Meremeta, Kagoda na Mwananchi Gold Mine ambazo zote kwa pamoja zimechota zaidi ya moja ya tano ya bajeti ya nchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Taifa, Bw. Mbowe alisema pamoja na kupinga suala la malipo ya Dowans, lakini huenda chama chake kikawahamasisha wananchi kuingia tena mitaani kupinga mkataba mwingine unaofanana na ule wa Richmond ambao serikali inatarajia kuingia tena kwa kipindi cha miezi minne.
Bw. Mbowe alisema serikali hivi sasa inakamilisha mchakato wa kuingia mkataba mwingine mfano ya ule wa Richmond, ambapo itakodi mitambo ya kuzalisha umeme kwa kipindi cha miezi minne kuanzia Julai mwaka huu ambapo kila mwezi itakuwa ikilipa sh. bilioni 400.
Ndugu zangu serikali yetu inatushangaza, hivi sasa inajipanga kuingia mkataba mwingine wa kifisadi wa kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme kwa gharama ya sh. bilioni 400 kila mwezi ambapo pia itakuwa ikilipa sh. bilioni 23 kwa ajili ya kununulia mafuta, sasa hii tunaikataa pia, alieleza Bw. Mbowe.
Leo viongozi wa CHADEMA wanahitimisha ziara yao katika mikoa ya kanda ya Ziwa ambapo pia kitatoa tamko rasmi kuhusiana na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa mwishoni mwa mwezi uliopita akiituhumu CHADEMA kutaka kuchochea vurugu nchini.
CHANZO:MAJIRA
No comments:
Post a Comment