ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 5, 2011

CCM waitaka dola iwadhibiti Chadema

WANAZUONI, WANASIASA WAPINGA
Na Waandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema nyendo za chama cha upinzani cha Chadema, zina agenda ya siri ya kuking’oa madarakani kwa kutumia nguvu kinyume cha katiba, hivyo kikaitaka serikali pamoja na vyombo vyake vya dola kuchukua hatua za kisheria haraka.

“CCM inaviomba vyombo vya dola viwe imara kuchukua hatua za kisheria…, wanachofanya Chadema ni kutuchonganisha na wananchi, kutoa kauli hatari za kujaribu kughilibu akili za watu ili kuchochea machafuko, umwagaji wa damu na uasi," alisema Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Itikadi na Uenezi, John Chiligati kwenye mkutano na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam na kuongeza:


“Wanachochea wanachi wakisema, peoples’ power! (nguvu ya umma). Je, mpo tayari kufanya kama Tunisia, Misri? (ambako serikali zilipinduliwa kwa nguvu ya umma).”  

Tamko la CCM limekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa, kukitahadharisha Chadema kwamba mikutano na maandamano ambayo waliyafanya kanda ya ziwa yanachochea uasi dhidi ya serikali iliyochaguliwa kikatiba kinyume cha sheria, hivyo akawaomba waache mtindo huo.

Chiligati jana alisema kwamba viongozi wa Chadema wameonekana kudharau ushauri huo wa mkuu wa nchi wakisisitiza kuwa “wembe ni ule ule hadi kieleweke.” 

Kwa sababu hiyo Chiligati alisema wanachofanya viongozi wa Chadema ni kinyume cha sheria za nchi hivyo wakaitaka serikali na vyombo vya dola vichukue hatua za haraka. 

Kinachoitisha CCM
Chiligati alisema tangu Chadema waanze ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, wameshuhudia viongozi wa chama hicho cha upinzani wakitoa kauli za kuupotosha umma na zenye kuchochea uasi na machafuko.

“Kauli za kuwafanya wananchi wafanye fujo ili nchi isitawalike, kauli za kuhamasisha wafanye vurugu kama zile za Misri na Tunisia ili kushinikiza Rais aondoke madarakani kwa mabavu. Kwa hakika ni kauli za hatari mno na zinazoashiria umwagikaji wa damu mkubwa hapa nchini”. 

“Mkuu wa nchi ameonya kauli hizi zikome… lakini cha kushangaza, tumesikia majibu ya Dk (Willbrod) Slaa (Katibu Mkuu wa Chadema), Mheshimiwa (Freeman) Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema Taifa) wakisema: Wembe ni ule ule hadi kieleweke.” 

Chiligati alifafanua kauli ya viongozi hao kuwa ina maana wataendelea na kauli za kuchochea vurugu na nchi isitawalike jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi.

Chiligati ambaye ni Mbunge wa Manyoni Mashariki, aliweka bayana kwamba tatizo la CCM siyo Chadema kufanya maandamano wala mikutano, bali kauli za viongozi hao.

“Tatizo siyo maandamano. Tatizo ni lugha na kauli za upotoshaji na za kuchochea vurugu, ghasia na uvunjaji wa sheria. Mambo hayo ndiyo Mheshimiwa Rais Kikwete amewaonya na kuyakemea wayaache,” alionya Chiligati.

Chiligati alisema kwamba kauli hizo zingetolewa na Chadema kwenye kampeni za uchaguzi, CCM isingeona ajabu kwa sababu wakati huo kila chama kinajaribu kuvuta hisia za wapigakura... “Sasa kipindi cha uchaguzi kimekwisha, lakini wenzetu bado wanaendelea na yale yale… Ni lini nchi itatulia, tuache malumbano na tufanye kazi ya kutatua matatizo ya wananchi?”

Chiligati alimfananisha Dk Slaa na kiongozi wa upinzani wa Angola, marehemu Jonas Savimbi kwa kile alichosema tafsiri yake ya kuendelea na malumbano baada ya uchaguzi ambao alishindwa kwenye nafasi ya urais akisema kila aliposhindwa hakumtambua aliyeshinda na badala yake kuhamasisha uasi.

Alisema CCM haipingi kukosolewa kwani hiyo ni kazi ya vyama vya upinzani hivyo baada ya uchaguzi, walitegemea Chadema kutumia wabunge wake 48 bungeni kuweka bayana kasoro za serikali ya chama hicho tawala ili zirekebishwe.

“Hapa tunapenda tueleweke kwamba hatusemi vyama vya upinzani visiikosoe serikali, hapana! Uhuru upo wa kutosha kwa Chadema na vyama vingine kukosoa lakini iwe kwa lugha ya kiungwana, siyo matusi, kudhalilishana wala ya uchochezi,” alionya Chiligati.

Chiligati ambaye ni Kapteni mstaafu wa jeshi, aliyataja matukio ambayo Chadema imekuwa ikiyatumia katika kuwapotosha wananchi ili kujipatia umaarufu kuwa ni milipuko ya mabomu katika Kambi ya Jeshi Gongo la Mboto, sakata la Dowans kuidai mabilioni serikali na kupanda kwa gharama za maisha.

Milipuko Gongo la Mboto
Chiligati alisema Dk Slaa amekuwa akitangaza kwenye mikutano yake kwamba baada ya milipuko ya mabomu Mbagala mwaka 2009, serikali ililinyima jeshi fedha za kuteketeza mabomu yaliyokwisha muda wake katika Kambi ya Gongo la Mboto hadi yalipolipuka hivi karibuni na kuua watu 25 kujeruhi 512.

Lakini akasema CCM inaamini kuwa kauli hiyo ni ya uongo na ya uchochezi kwa sababu tume mbili, ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na ya wataalamu wa nje, zinafanya uchunguzi wake na bado hazijatoa matokeo yake.

“Uchunguzi haujatolewa, sasa Dk Slaa amepata wapi matokeo hayo anayoyatangaza kama siyo kuendeleza hulka yake ya uzushi?” Alihoji Chiligati huku akiwataka wananchi wapuuze kauli hizo kwa kuwa ni za uzushi.

Sakata la Dowans
Chiligati alisema kwamba CCM imekuwa ikiwapotosha wananchi kwamba serikali na “CCM tayari wameamua tena kwa furaha kuilipa Dowans Sh 94 bilioni” kutokana na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Biashara.

Alisema huo ni uzushi na uchochezi kwa sababu suala hilo serikali pamoja na CCM wamekuwa wakisisitiza lisilipwe na ifanyike mikakakti ya kisheria ya ama kuliondosha kabisa au kupunguza mzigo. Alielezea hatua zilizochukuliwa na CCM pamoja na serikali kwa nyakati tofauti na kwamba zimewezesha suala hilo kuanza kufanyiwa kazi Mahakama Kuu ya Tanzania.

Isitoshe, alisema wamejaribu kuwatumia hata baadhi ya makada na wabunge wa CCM wenye umaarufu wa sheria kama vile Nimrod Mkono ili kuongeza nguvu ya kupambana na Dowans.

Aliitetea msimamo uliotolewa na Kamati Kuu ya CCM akisema iligundua mambo matatu makuu kuhusu malipo ya Dowans, kuwa ni suala la hukumu, ni jambo la kisheria na kwamba wakati kesi ipo mahakamani serikali isiilipe Dowans.

“Huu ni ukweli kuhusu suala hili, viongozi wa Chadema wanaelewa lakini wameamua kupotosha umma kwa makusudi ili kujenga chuki dhidi ya serikali na CCM,” alilalamika Chiligati.

Matatizo yanayolikabili Taifa
Chiligati alisema matatizo yanayolikabili Taifa ni upungufu wa nishati ya umeme na kupanda kwa gharama za maisha na upungufu wa chakula uliotokana na ukame kwa baadhi ya wilaya nchini.  Alisema matatizo hayo yote Rais Kikwete aliyaelezea katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari pamoja na mikakati ambayo inachukuliwa na serikali yake.

Alirejea hotuba hiyo akisema kwamba Rais Kikwete alisema suala la njaa katika wilaya 23 nchini tayari limeshughulikiwa na vyakula vimepelekwa ili kusambazwa.

Kuhusu kupanda kwa gharama za maisha, Chiligati alisema kuwa Rais Kikwete alisema ni kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo vitu mbalimbali nchini navyo bei yake imepaa.

Alisema suala la kupanda kwa sukari serikali imechukua hatua za kuingiza sukari bila kulipiwa ushuru wa forodha na kwamba watahakikisha bei inashuka kutoka Sh 2,200 kwa kilo hadi 1,700.

Hata hivyo, baadhi ya waandishi wa habari walikosoa wakisema bado wafanyabiashara wa Dar es Salaam wanakiuka agizo hilo la Rais na wanauza kwa bei ya kati ya Sh 2,000 na 2,200.

Wasomi, wanasiasa wapinga
Wasomi na wanasiasa wamepinga msimamo huo wa CCM wakisema kauli yake na ile ya Serikali ni hofu isiyokuwa na msingi dhidi ya chama hicho na ndiyo inayovunja Katiba kwa kubana uhuru wa kujieleza.

Wakizungumza na gazeti hili jana, walisema kwa kauli hiyo, Serikali ndiyo inayotaka kuvunja amani na siyo Chadema kwani maandamano yao yamefanywa kwa vibali maalumu vya mamlaka husika.

Chama cha NCCR-Mageuzi na Chama cha Kijamii (CCK) vimeyaunga mkono maandamano hayo vikisema ni sahihi kufanywa kwa kuwa hiyo ndiyo kazi ya vyama vya siasa. Kauli za vyama hivyo zimetolewa siku moja baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Steven Wassira kukitisha Chadema na kukionya kisije kikailaumu serikali itakapokosa uvumilivu na kutumia dola kupambana nacho.

Wassira alisema chama hicho kinapandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya serikali na kuandaa mpango wa kuiondoa kwa nguvu serikali iliyoko madarakani.

Kauli hiyo ya Wassira iliungwa mkono na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango ambaye alidai kuwa maandamano hayo ya Chadema hayana nia ya kushinikiza Dowans isilipwe, bali kuhamasisha vurugu nchini.

Mwenyekiti wa CCK, Costantine Akitanda alisema serikali ndiyo inayoweza kuvuruga amani kwa kuogopa kivuli cha Chadema ambayo ina wabunge 47 tu bungeni.

“Nchi hii itabaki kuwa tulivu……, labda serikali iamue kwa kuogopa kivuli cha Chadema, kama tulivyoweza kuwaondoa wakoloni bila kumwaga damu, ndivyo hivyo hivyo tutakavyoweza kuiondoa CCM madarakani,” alisema Akitanda.

Alisema Rais Kikwete kujitokeza hadharani na kuilaumu Chadema si jambo sahihi badala yake alitakiwa  atoe msimamo wa serikali kuhusu maandamano yanayofanywa na chama hicho.

Naye Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni na Uenezi wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura alisema lingekuwa jambo jema kama Wassira angefafanua ni kauli zipi zinazohatarisha amani ambazo Chadema wamezitoa na asipofanya hivyo atakuwa anaitia aibu Serikali.

“Serikali lazima watoe ushahidi unaoonyesha Chadema wamevunjaje amani, kisheria ukipeleka kesi mahakamani ni lazima uwe na ushahidi wa kutosha, watuonyeshe ushahidi wao," alisema Sungura.

Alisema ziara inayofanywa na Chadema ni ya kisiasa na imepewa baraka zote na Jeshi la Polisi: “Kama kuna mtu ndani ya Chadema katoa kauli za uchochezi achukuliwe hatua na si serikali kutoa vitisho kuwa itasitisha maandamano, kosa la mtu mmoja haliwezi kukigharimu chama.”

Sungura alisema CCM kinatakiwa kujiuliza kwa nini hivi sasa Watanzania wakiambiwa waandamane wanakubali kirahisi? “Ukiona watu wanashabikia maandamano tambua kuwa wamechoshwa na yale yanayofanywa na viongozi wao, siku zote imani kutoka kwa wananchi ndiyo kipimo cha mazuri ya Serikali,” alisema na kuongeza: 

“Mwaka 2005 wakati Rais Kikwete anaingia madarakani bei ya petroli ilikuwa kati ya Sh950 na 1,050 lakini mwaka huu bei imepanda na kufikia Sh1,800 mpaka 1,890, kipindi hicho hicho sukari ilikuwa Sh600 kwa kilo na leo hii bei ni Sh2,000, sasa hapo wananchi wataendelea kuipenda CCM?”

Alikitaka Chadema kutumia maandamano hayo kuwaelimisha wananchi ili wawe na ufahamu juu ya haki zao za msingi katika kuchagua kiongozi bora.

Wakili wa kujitegemea, Barnaba Luguwa alisema migogoro inayotokea nchini ambayo inaambatana na maandamano inatokana na serikali kushindwa kutekeleza ahadi zake. Alisema hali hiyo inatoa mwanya  kwa raia na vyama vya kisiasa kuingia katika maandamano yanayosababisha madhara mbalimbali kijamii na kiuchumi.

Alisema maandamano yanayofanywa na Chadema ni halali kwa mujibu wa sheria na kuitaka serikali  kupunguza kauli za mabavu zinazotolewa na baadhi ya viongozi wake. 

“Chama chochote au mtu binafsi ana haki ya kufanya maandamano ya amani ilimradi tu isivunjwe sheria,” alisema na kuongeza kuwa vyama vya siasa vikifanya maandamano ya amani ni msaada kwa serikali kwani vinaikumbusha wajibu wake katika jamii ili kuzifanyia kazi.

Imeandaliwa na Leon Bahati, Fredy Azzah, Edom Mwasamya na Alphey Athanas wa gazeti la Mwananchi

No comments: