ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 4, 2011

Dk. Alwyn Mziray kuagwa leo


Aliyekuwa daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Alwyn Mziray

Mwili wa aliyekuwa daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Alwyn Mziray (38) (pichani) ambaye alihusika kwa kiasi kikubwa kuwatibu majeruhi wa milipuko ya mabomu wa Gongo la Mboto, unatarajiwa kuagwa leo jijini Dar es Salaam.
Dk. Mziray alifariki ghafla Jumapili iliyopita wakati akiwa hotelini mjini Zanzibar.
Kwa mujibu wa msemaji wa familia, Frank Mziray, ambaye ni kaka wa marehemu, shughuli ya kuagwa kwa mwili wa Dk. Mziray itafanyika nyumbani kwa baba yake mzazi Oysterbay ambapo utalala.
Alisema kutakuwa na misa na baada ya hapo ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wafanyakazi wenzake watatoa heshima zao za mwisho kisha mwili huo utasafirishwa kuelekea nyumbani kwao Usangi, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kesho.
“Tunatarajia misa ya Ijumaa itaanza asubuhi na shughuli ya kuuaga mwili huo itakuwa kati ya saa 5:00 hadi saa 7:00 mchana, mwili wake utazikwa siku itakayofuata saa 8:00 mchana,” alisema.
Dk. Mziray alifariki siku hiyo saa 11:00 jioni wakati akiwa na wageni wake kutoka Marekani waliokwenda visiwani humo kwa ajili ya mapumziko.
Katika toleo letu la jana tuliandika kwa makosa kwa kumuita marehemu kuwa ni Dk. David. Jina sahihi ni Dk. Alwyn Mziray. Tunaomba radhi kwa usumbufu uliowapata wahusika-Mhariri.
CHANZO: NIPASHE

No comments: