4th March 2011
.jpg)
Wakati presha ikizidi kupanda kuelekea mechi ya marudiano ya Ligi Kuu ya Bara baina ya watani wa jadi, makocha, Patrick Phiri wa Simba na Sam Timbe wa Yanga pamoja na wachezaji wao wametamba kila mmoja ataibuka na ushindi ili kuweza kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa msimu huu.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, kocha wa Simba, Phiri alisema kuwa wachezaji wake wamejiandaa vyema kuhakikisha wanashinda na hawana wasiwasi wowote juu ya mchezo huo.
Phiri alisema kuwa licha ya kuwakosa nyota wake wawili beki, Joseph Owino na mshambuliaji, Emmanuel Okwi, pengo lao litazibwa na chipukizi wengine ambao wameonyesha uwezo wa juu tangu walipoanza mechi za mzunguko wa pili.
Alisema kuwa mazoezi yao yamekwenda kama walivyopanga na kila mchezaji ameahidi kuonyesha uwezo ili aweze kupata namba katika mechi hiyo na ijayo ya kimataifa.
"Wachezaji wangu wako vizuri isipokuwa Owino na Echessa, ila naamini watakuwa wamepona na kurejea katika stamina kuanzia wiki ijayo, naamini watakuwa tayari kabla timu haijasafiri kwenda Kongo (kuwavaa TP Mazembe katika Ligi ya Klabu Bingwa Afrika)," alisema Phiri.
Aliongeza kuwa amezungumza na mchezaji mmoja mmoja na kumueleza kwamba wanatakiwa kuwa makini na kutoruhusu wapinzani wao wawafunge kwa mara ya tatu msimu huu baada ya kupoteza mechi yao ya ufunguzi wa msimu (Ngao ya Jamii) na mechi yao ya awali ya Ligi Kuu.
Nahodha wa timu hiyo, Nico Nyagawa, aliliambia gazeti hili kwamba mechi ya kesho itakuwa ngumu lakini wamepanga kujituma ili kuibuka na pointi tatu.
Nyagawa alisema pia wanawaomba mashabiki wao kujitokeza na kuwaombea dua ili malengo yao yatimie.
"Itakuwa ni mechi ya kihistoria, tunapambana na Yanga kama mechi ya fainali, tunawaomba wote wanaoipenda Simba tuwe na mshikamano ili tutimize kile tunachokitarajia wachezaji," aliongeza Nyagawa.
Naye Timbe ambaye atakuwa anasimama katika benchi la ufundi kwa mara ya kwanza wakati timu yake mpya inakutana na mahasimu wake alisema kuwa kila kinachotakiwa kufanywa katika maandalizi ya muda mfupi amekikamilisha.
Timbe alisema kuwa anafahamu kwamba ushindi katika mchezo huo ni muhimu kwake na vile vile utaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yake ya kutwaa ubingwa msimu huu.
"Ni mechi yenye upinzani lakini tunatakiwa kufanya juhudi za ziada, nimelifanyia kazi kila tatizo nililoliona kwa wachezaji wangu, tutahakikisha tunapata matokeo mazuri," aliongeza Timbe.
Licha ya uongozi wa Yanga kuwakataza wachezaji wake kuzungumza na vyombo vya habari, habari kutoka ndani ya kambi hiyo zinasema kuwa wamejipanga kufanya vizuri ili kumaliza hali ya 'migogoro' ya chini kwa chini inayoendelea.
"Kwa kifupi tuko vizuri, hakuna mchezaji ambaye ni majeruhi sana, wapo wenye maumivu ya kawaida," alisema mmoja wa wachezaji hao jina lake tunamuhifadhi.
Mechi hiyo itakayochezwa kesho kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam itakuwa ni ya nne kwa timu hizo kukutana msimu huu ikiwemo ya Januari 12 mjini Zanzibar katika fainali ya Kombe la Mapinduzi ambapo Simba ilitwaa kombe hilo kwa ushindi wa 2-0 mbele ya Rais Mpya wa Serikali ya Mapinduzi, Dr, Ali Mohammed Shein.
Simba iliyoko Zanzibar ikijifua kwenye uwanja wa Fuoni inatarajia kurejea jijini Dar es Salaam leo jioni wakati Yanga iliyoko kambini Bagamoyo itarejea kesho na kuelekea moja kwa moja uwanjani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment