ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 4, 2011

Jaji ajitoa kesi ya samaki wa Magufulu

Jaji Radhia Sherkh amejitoa kuendelea kusikiliza kesi inayowakabili raia wa kigeni 36 kwa kufanya uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi upande wa Tanzania ili haki itendeka.
Kesi hiyo ambayo inasikilizwa na jaji Radhia katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana iliitishwa kwa ajili kutolewa uamuzi wa jaji kuendelea kusikiliza kesi hiyo au kujitoa kutokana na washtakiwa kudai kuwa hawana imani naye.

Awali, washtakiwa hao baada ya kunyimwa dhamana na Jaji Sherkh kwa kudai kuwa haramu na kuamua kuwanyima dhamana, walimtaka jaji huyo kujitoa katika kesi hiyo.
Washtakiwa hao walifikia uamuzi huo baada ya jaji huyo kuwanyima dhamana licha ya Mahakama hiyo awali kuwapa kwa masharti waliyoshindwa kuyatimiza.
Kupitia mawakili wao wa utetezi, Ibrahhim Bendera, akisaidiana na John Mapinduzi, washitakiwa hao walidai kuwa hawana imani na jaji Radhia baada ya uamuzi huo wa mahakama ambao wanaamini kuwa haki haitatendeka.
Jaji Radhia alisema kuwa kutokana na mazingira ya kesi hiyo, ameamua kujitoa ili kesi hiyo itendewe haki na kwamba si kwa sababu walizozitoa washitakiwa dhidi yake.
Alisema sababu walizozitoa dhidi yake sio za msingi kwa mujibu wa sheria na kwamba ucheleweshaji wa kesi ulikuwa ukisababishwa na wakili Mapinduzi kutokufika mahakamani pasipo na sababu za msingi.
Jaji Radhia alisema pamoja na kwamba kwa makosa waliyonayo wana haki ya kudhaminiwa ila kwa kuwa hawana vibali vya kuishi nchini ndiyo sababu iliyomfanya awanyime dhamana.
Alisema alichokiona ni upande wa utetezi umekuwa ukifanya mambo bila kuwepo kwa utaalamu na kwamba walichotakiwa ni kwenda kukata rufaa kwa kuwa wameona hawatendewi haki.
Alisema kuwa kesi hiyo ameirudisha kwa Jaji Mfawidhi ili aweze kupanga Jaji mwingine kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.
Washtakiwa wanadaiwa kuwa waliingia eneo la bahari hiyo isivyo halali kinyume na sheria ya nchi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na raia wa China, Vietnam, Indonesia, Taiwan, Ufilipino na Kenya.
CHANZO: NIPASHE

No comments: