Advertisements

Thursday, March 31, 2011

KAROTI; KINGA DHIDI YA SARATANI UGONJWA WA MOYO-2 GPL

WIKI iliyopita tulianza kuangalia umuhimu wa karoti kwa afya ya binadamu. Leo tunendelea na sehemu ya pili na ya mwisho juu ya mada hii. Endelea...

Kama karoti imestawishwa kwa kutumia madawa ya mimea na mbolea au kama huna uhakika na usafi wake, ni vizuri ukwangue maganda yake ya juu na kuyaondoa. Unaweza kuamua kukata vipande virefu au vya mviringo, kukata na mashine maalum vipande vidogo vidogo au kula nzima nzima.


Karoti ni tamu vyovyote utakavyoamua kuila, iwe mbichi au iliyochemshwa. Ingawa kula karoti mbichi ni bora zaidi, lakini hata ukila iliyopikwa bado haipotezi virutubisho vyake, zaidi inaelezwa kuwa, kambalishe, virutubisho pamoja na sukari yake inapatikana kirahisi na hivyo kuifanya kuwa tamu.

Jambo la kuzingatia kama ukiamua kuipika, usiipike sana, bali inatakiwa kuchemshwa au kupikwa kwa muda mfupi ili virutubisho vyake visipungue au kupotea kabisa.

DONDOO ZA KUTENGENEZA KAROTI
Unaweza kuitengeneza karoti kama unavyotaka ili kupata ladha tofauti bila kupoteza virutubisho vyake. Unaweza, kwa mfano, kutengeneza saladi ya karoti kwa kuchanganya na majani yake kwa kukatakata vipande.

Aidha, unaweza kutengeneza saladi kwa kukata vipande vidogo vidogo kisha kuchanganya tufaha na matango na kula pamoja kwenye mlo wako wa siku kama kachumbari.

Unaweza kutengeneza supu ya karoti kwa kuchemsha vipande vyake na nyanya. Chukua karoti na nyanya ulizochemsha, kisha weka kwenye ‘blender’ au chombo kingine unachoweza kusagia. Saga mchanganyiko huo ili kupata supu, unaweza kuongeza viungo vingine ili kupata ladha. Unaweza pia kuinywa ikiwa ya moto au ikiwa imepoa.

Kinywaji kingine unachoweza kutengeneza kwa afya yako ni juisi ya karoti, ‘soymilk’ na ndizi mbivu. Tengeneza nusu glasi ya juisi ya karoti, chukua glasi moja ya soymilk na ndizi mbivu moja kisha changanya kwa kutumia ‘blender’. Kama huna changanya kwa kutumia kijiko au mwiko na kupata ‘milk shake’ ya ukweli.

KAROTI IKIZIDI MWILINI
Ingawa siyo rahisi kutokea lakini inawezekana kuna watu matumizi ya mboga hii kwao yako juu. Karoti ikizidi mwilini, huweza kumfanya mtu aonekane ‘wa njano’, hasa katika sehemu za viganja vya mikono, nyayo za miguu na nyuma ya masikio. Kitaalamu hali hii hujulikana kama ‘carotoderma’.

Hata hivyo, hali hiyo hutoweka pale mtu huyo anapopunguza ulaji wa karoti au vyakula vingine vyenye kiwango kikubwa cha virutubisho vya ‘carotene’ na hakuna madhara mengine anayoweza kuyapata.
Mwisho, katika nchi za Asia, ambako ndiko karoti inaelezwa kuanzia, inaaminika pia kuwa na uwezo wa kurekebisha masuala ya nguvu za kiume na ukosefu wa hamu ya kufanya mapenzi (sexual dysfunction & sexual drive).

Pia karoti inaaminika kuimarisha ufanisi wa figo na kuondoa hewa chafu na baridi mwilini. Baada ya kujua faida za karoti, bila shaka kuanzia leo umepata sababu ya kuiangalia upya karoti kama ‘mzizi’ muhimu kwa afya yako.

No comments: