21st March 2011
.jpg)
Wasomi, wanasiasa na wananchi wamesema kauli iliyotolewa na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, kuwa kila Mtanzania atakula kwa jasho lake ni dalili ya kulewa madaraka na wamemshauri ajiuzulu.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Dk. Benson Bana amesema Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo ameteleza kutokana na kauli yake kuwa kila Mtanzania atakula kwa jasho lake.
Dk.Bana alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na NIPASHE kuhusiana na kauli ya Mkulo.
“Mimi nafikiri Waziri ameteleza kwa sababu tangu ameingia katika Wizara hiyo sijamsikia hata siku moja akitoa kauli kama hiyo. Ni muhimu akafahamu kuwa Watanzania wanalipa kodi ili watengenezewe mazingira ya kufanya shudhuli zao. Kama ni mjasiriamali ,mkulima, mfanyabiashara, wote hawa wanahitaji mazingira ya kuwawezesha kutumia jasho lao ili waweze kujiendeleza,” alisema.
Dk Bana alisema kwamba bahati mbaya serikali ambayo Waziri Mkulo yumo ndani yake bado haijaweza kuwatengenezea wananchi hao mazingira ambapo watalitumia jasho lao kupata riziki ya kila siku.
Aliwataka mawaziri na viongozi wengine wa serikali kujifunza somo la mawasiliano na umma ili waepuke kutoa maneno yatakayosababisha wananchi kuichukia serikali yao na hata chama kinachotawala.
Alisema kuwa huko nyuma mawaziri Cleopa Msuya na Basil Mramba walioshikilia wizara hizo waliwahi kutoa maneno ya aina hiyo yaliyowakwaza wananchi.
Naye Mhadhiri Mashuhuri nchini kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) kilichoko mwanza, Profesa Mwesiga Baregu alisema kauli iliyotolewa na Waziri Mkulo inaonyesha ni kwa jinsi gani ambavyo yeye na serikali iliyopo madarakani walivyochoka kuwatumikia wananchi.
“Ukiona Waziri anasema hivyo ujue kuna mawili,amechoka kazi au hana uwezo na nafasi hiyo…Kama alijua hawezi kazi asingechukua nafasi hiyo,kwa sababu wananchi wamemchagua yeye na serikali yake ili wasimamie maeneo yatakayowawezesha wananchi kula kwa jasho lao” alisema.
“Unajua haiingii akilini kuwaambia wananchi wale kwa kutumia jasho lao wakati wewe unakula jasho lao kupitia kodi mbalimbali wanazolipa serikalini,”alisema.
Alisema maneno hayo ni ishara ya wazi kuwa yeye binafsi au serikali yake imechoka wakati ndiyo bado kunakucha.
Profesa Baregu alifafanua kwamba kauli iliyotolewa na Mkulo ni ya wachovu waliojisahau kuwa utumishi wa umma una sifa, taratibu na nidhamu yake.
Alimtaka kama amechoka ajiuzulu na siyo kuwatukana Watanzania kwa kuwa hakuna mtu aliyemwingiza madarakani kwa nguvu.
Aidha aliiasa serikali kama imeshindwa kazi ijiuzulu mapema iwapishe walio tayari kuwatumikia wananchi sasa badala ya kusubiri hadi miaka mitano ipite kwa kuwa mawaziri wake kama alivyo mkulo wameshachoka tayari.
Naye Mwenyekiti wa APPT Maendeleo Peter Mziray, amemtaka Waziri Mkulo kujiuluzu kwa kuwatukana Watanzania kwamba kila mtu atakula kwa jasho lake.
Mziray alisema kauli ya Mkulo kuwataka watanzania kula kwa jasho lao wakati viongozi wote wanakula kwa jasho la walala hoi ni sawa na unyonyaji.
“Mimi nasema Mkulo aachie ngazi na ajiuzulu kwa sababu mawaziri, wabunge na viongozi wengine wa serikali wanakula kwa jasho letu walala hoi … inakuwaje anasema kila Mtanzania atakula kwa jasho lake wakati wao wanafaidika bila kutoka jasho lolote,” alihoji Mziray.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment