Awabebesha polisi lawama.jpg)
Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapile maarufu kama ‘Babu’, amesitisha huduma ya kutoa dawa kwa wagonjwa akiwashutumu polisi wanaolinda usalama na kuongoza foleni ya magari kuanza kupokea rushwa kutoka kwa vigogo na watu wenye uwezo mkubwa kifedha ili wawahi kupata huduma yake.
Babu alisitisha zoezi hilo juzi saa 6:00 usiku baada ya kuwaona watu wakipita njia zisizo halali kumfikia.
Akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu, mmoja wa wagonjwa hao, Godbles Massawe, alisema hali ni mbaya kwani huduma hiyo ilisitishwa tangu saa 6:00 usiku wa kuamkia Jumapili na hadi jana jioni alikuwa hajaanza kutoa huduma hiyo.
Alisema hali hiyo imetokea baada ya Mchungaji huyo kugundua utapeli huo hivyo kusitisha huduma kwa muda usiofahamika hadi hapo watu watakapojipanga sawa kwa kufuata utaratibu.
“Haya yote yamekuja baada ya hawa mapolisi waliokuwa wanalinda usalama wa hapa kuanza kupitisha vigogo na watu wenye pesa zao na kuacha kufuata foleni hali inayosababisha kuvurugika kwa ratiba ya hapa,” alisema.
Massawe alisema vigogo hao walikuwa wakipitishiwa barabara ya kutokea kwa Babu kuelekea Arusha badala ya kupitia barabara iliyopangwa kwa ajili ya kuingilia kutokana haraka haraka jambo lililomkera.
Alifafanua kuwa kutokana na huduma hiyo kusimamishwa, watu wapatao wanane tayari wamefariki dunia baada ya kuzidiwa na maradhi yao ikiwa ni pamoja na foleni kuwa kubwa.
Alisema foleni hiyo imekuwa ikiongezeka kutokana na watu wengi kuzidi kumiminika kutoka Arusha, Serengeti na sehemu mbalimbali hapa nchini, kuelekea kwa mchungaji Mwasapile huku huduma ikiwa imesitishwa, jambo ambalo limesababisha mazingira ya eneo hilo kuwa magumu zaidi.
“Kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani hapa, watu wanaishi katika mazingira magumu huku njaa ikitawala na bidhaa kupanda bei kila kukicha…Pia, ukosefu wa chakula na maji umesababisha baadhi ya watu kuwa katika mazingira magumu baada ya vyakula walivyokuwa wamebeba kuwaishia wakati wakisubiri zamu yao iliyowachukua siku nne,” alisema Massawe.
Aidha, aliomba serikali kuboresha mazingira ya kijijini hapo ikiwemo huduma za vyoo, maji, chakula na sehemu za huduma ya kwanza.
Alisema serikali pia isaidie kudhibiti wale wanaotumia njia za panya kusitisha kufanya hivyo ili Babu aendelee kutoa huduma hiyo.
Kwa mujibu wa Massawe, chupa ya robo lita ya maji kwa sasa inauzwa Sh. 500, nusu lita Sh.1,000 huku unga robo kilo ukiwa unauzwa Sh. 500.
Wakati huohuo, magari yaliyokuwa yanakwenda kwa Mchungaji Mchungaji Mwasapile katika kijiji cha Samange, wilayani Ngorongoro jana yalikwama njiani na kushindwa kuendelea na safari kutokana na mito kujaa maji yanayotokana na mvua inayoendelea kunyesha mkoani Arusha.
Akizungumza na NIPASHE, Mkuu wa Wilaya ya Loliondo, Elias Wawalali, alisema magari mengi yaliyokuwa yanapeleka watu kunywa dawa kwa Babu, yalishidwa kwenda kutokana na mito ambayo ipo njiani kufurika hali iliyosababisha magari hayo kusubiri kwa muda mrefu.
"Mito imejaa kutokana na hii mvua ambayo inaendelea kunyesha hali linayosababisha magari kushidwa kuvuka mpaka maji hayo yatakapopungua na uzuri huku kwetu maji yanapungua haraka sana mito yetu inapitisha maji mengi na yanawahi kupungua ndiyo kitu cha kushukuru hicho maana yangekuwa hayapungui sijui ingekuwaje," alisema Wawalali.
Aliongeza kuwa kadiri siku zinavyozidi kwenda, ndivyo watu wanavyozidi kufurika na mpaka jana kulikuwa na watu wengi haijawahi kutokea na magari yalikuwa yamejipanga umbali wa kilomita 30 hadi kuyafikia makazi ya Babu.
Alisema watu ambao wanapitia barabara ya Mto wa Mbu wamekuwa wakielewa na wamepungua kwa kiasi fulani lakini tatizo ni watu ambao wanatoka Kanda ya Ziwa kwani wao ndiyo wanaonekana kuingia kwa kasi kubwa.
Aliwaomba viongozi wa sehemu hizo kutoa elimu kwa wananchi wao ili kupunguza mkusanyiko wa watu ambao wako Loliondo ndio wao waende.
"Unajua sisi tukiwaambia wakae watulie kwanza wasije hawatuamini sijui niseme hawatuelewi maana tunaimba kila siku watu ni wengi subirini wapungue lakini hawaamini kabisa. Sisi tunawaomba wakae wasubiri watu wakipungua tutawaambia maana huku wanakuja kuteseka tu na jinsi mvua zinavyonyesha watateseka sana, wangoje watu ambao tuko huku tutawaambia na watu wanaotoka huku wawaambie wenzao hali halisi," alisema Wawalali.
Mchungaji Mwasapile alisema yeye anapenda kuwahudumia watu ila kilio chake kikubwa kwa wale watu ambao wanawaleta wagonjwa wao wakiwa mahututi.
"Jamani, napenda kuhudumia ila watu wasilete wagonjwa wao wakiwa mahututi kwani huku wakiwaleta mpaka wafikie kupata huduma ni kazi hali ambayo inasabaisha wagonjwa wengi wanaoletwa wakiwa na hali hiyo kufariki dunia " alisema Mchungaji Mwasapile.
Aliongeza kuwa katika Kijiji cha Sumange hakuna watu wa huduma ya kwanza wala hospitali hali inayosababisha watu ambao wanapelekwa na dripu zao ikiisha kukosa huduma na vifaa vya huduma ya kwanza hivyo wasubiri wapate nafuu ndipo wawapeleke.
Hata hivyo, katika kituo cha mabasi ya Loliondo, mjini hapa, kumekuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu wanaoelekea huko na pia nauli zimekuwa zikipanda siku hadi siku.
Nauli kwa sasa ni kati ya Sh. 60,000 na 100,000 na kwa magari aina ya Land Cruizer.
Mmoja wa abiria ambaye alikuwa katika kituo cha basi cha Loliondo mkoani hapa, Meshack Alex, alisema abiria wamekuwa wakipata shida ya usafiri kwani nauli zinapanda kila siku na aliiomba serikali ifuatilie suala hilo ili kila mtu aweze kwenda kwa Babu kupata tiba hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment