ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 23, 2011

KIYAMA

Na Mwandishi Wetu
WAKATI masikio na macho ya maelfu ya watu duniani yakiwa Loliondo, Tanzania kwa Babu Ambilikile Masapile kupata kikombe cha dawa, muumini wa Kanisa la EAGT wilayani Mufindi, mkoani Iringa, Bahati Ngeniuko ameibuka na kudai kuwa na yeye amepewa maono na Mungu.


Katika waraka wake kwa vyombo vya habari hivi karibuni (Risasi Mchanganyiko lina nakala), Ngeniuko ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi ya Makalala, Mufindi, alisema kuwa, hivi karibuni alipelekewa maono na Muumba akiambiwa kwamba, dunia itakuwa imefikia mwisho, Mei 21, mwaka huu, siku 59 kuanzia leo.
Katika waraka huo, Ngeniuko alisema kwamba, amepewa maono hayo ili awatangazie Watanzania kuwa, wale na kunywa lakini ule mwisho umefika na Mei 21 itakuwa unyakuo utakaotanguliwa na ufufuo wa waliolala makaburini (kiyama). 

Ili kutia nguvu maono yake, Ngeniuko alisema kuwa, Mungu amemwambia, kutokea kwa Mchungaji Ambilikile Masapile ‘Babu’ wa Loliondo akitoa dawa kwa watu wenye magonjwa sugu na tetemeko la Tsunami nchini Japan hivi karibuni ni dalili za mwisho wa dunia.
Ngeniuko alitoa baadhi ya vifungu vya maandiko kutoka kwenye Biblia Takatifu na kusema vinaashiria mwisho huo.

Mathayo 24: 4-14, Yesu akajibu, akawaambia: “Angalieni, mtu asiwadangaye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, mimi ni Kristo;  nao watawandanganya wengi. Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; ….kutakuwa na njaa na matetemeko ya nchi mahali mahali.”

Aidha, Ngeniuko alisisitiza kuwa, kitakachotokea Mei 21 mwaka huu ni unyakuo wa kanisa kwanza, lakini dunia itafikia mwisho kabisa, Oktoba 21, mwaka huu ambapo ulimwengu mzima utakumbwa na tetemeko kubwa la ardhi na kuteketea.

Katika hali ya kushangaza, Ngeniuko alisema kuwa, amemwachisha masomo binti yake (hakumtaja jina), ili ajiandae na unyakuo badala ya kuendelea kujifuza elimu ya dunia ambayo haina maana tena.

Mwalimu huyo, akaweka wazi kuwa, endapo unabii wake hautatimia, yuko tayari kupigwa mawe hadi kufa.

“Nauamini utabiri wangu, namwamini Mungu. Kama hautatimia, nifanyiwe kama wale manabii wengi wa uongo waliotokea zamani (walipigwa mawe hadi kufa),” alisema mwalimu huyo.

Utabiri wa Ngeniuko unafanana na ule uliotolewa na Taasisi ya Marekani ya Family Radio uliosambazwa kwenye mitandao ya  habari ukisema kuwa, Mei 21, mwaka huu ndiyo mwisho wa dunia. 

Hivi karibuni, manabii wengi wa uongo wameibuka na kufanya matendo ya ajabu kiasi cha kuwadanganya wengi, wakiwemo waumini.

Mtu mmoja aliibuka nchini Urusi akidai yeye ni Yesu, akakusanya watu wengi na kuwafanyia miujiza mikubwa, ukiwemo wa kutembea juu ya maji, akaaminika.
Hata hivyo, siku chache baadaye, ‘Yesu’ huyo  aliugua tumbo na kulazimika kulazwa hospitali moja mjini Moscow hali iliyosababisha kutengezwa kwa vichwa vya habari vya kumkejeli magazetini nchini humo.

Miaka ya karibuni, mkoani Mbeya, kundi la waumini wa Kisabato liliibuka na kutaja tarehe ya mwisho wa dunia, walichoma moto nyumba zao na kuuza mali wakisubiri siku hiyo ya unyakuo.

Kama vile haitoshi, mtu mmoja anayejiita Nabii Tito, ameibuka jijini Dar es Salaam akitumia Biblia kudai kwamba, wanaume ruksa kuoa mke zaidi ya mmoja na ‘kutembea’ na wasichana wao wa kazi ‘mahausigeli’. Yeye mwenyewe ana wake wawili, anakunywa pombe.

Nchini Uganda, wananchi wake bado wanamkumbuka Nabii Kibwetere ambaye alitangaza tarehe ya mwisho wa dunia, waumini wake wakaacha kila kitu na kusubiri unyakuo, lakini mwisho, nabii huyo aliwachoma moto wauamini ndani ya kanisa  yeye akaingia mitini.

Yesu mweyewe anasemaje katika Mathayo 24: 36: “Walakini habari ya siku ile na saa ile  hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni, wala mwana, ila Baba (Mungu) peke yake.”


CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS

No comments: