ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 23, 2011

Umekata tamaa ya kupenda na kupendwa tena?

NI siku nyingine ya Jumatano tunakutana katika Uwanja wa Huba, najua mkononi mwako hivi sasa umekamata  Gazeti la Risasi na  moja kwa moja umefunua ukurasa huu ili uweze  kupata kitu kile roho inapenda.


Turudi kwenye mada yetu ya leo, wapendwa wangu! Nataka niwape ushuhuda wa dada zangu wawili ambao nilikutana nao na kubadilishana mawazo kuhusiana na masuala ya mapenzi.

Dada zangu hao ambao walionekana kukata tamaa ya kupenda na kupendwa tena baada ya kutendwa na wanaume waliokutana nao kwa nyakati tofauti katika pilikapilika za maisha.

Mmoja aliahidiwa kuolewa na mwanaume mwenye fedha ambaye alitaka kumuacha mke wake ili amuoe!  Lakini yeye alikuwa ameoza kwa mwanaume mwingine  ambaye alimzalisha kisha akamtelekeza na kuhamia kwa demu mwingine!

Hivi sasa anakumbuka bahati yake kwamba angekuwa ameshaolewa na tajiri kama siyo kuendekeza penzi la kijana yule.

Mwingine alishaolewa lakini mumewe alikuwa kiwembe, akaamua kuachana naye kwa vile kila siku ugomvi ulikuwa hauishi kwa kukuta ujumbe wa mapenzi kutoka kwa wanawake wengine kwenda kwa mumewe.

Kilichomuuma zaidi siyo kukuta ujumbe tu, bali tabia ya mumewe kuhonga vitu vyake kwa mahawara hao, hilo ilimtibua zaidi.

Jamani! dada zangu hawa, wanasema hawataki tena kupenda na wala kusikia wanaume wakiwaambia kwamba wanawapenda na wanataka kufunga nao pingu za maisha. Kauli  hii imekuwa ikitolewa na wanawake wengi pale wanapokumbana na ajali za mapenzi.

Kwa kifupi hawataki tena kuolewa, laiti kama wataolewa wanataka waachwe huru kufanya vile wanavyotaka wao kama kwenda muziki peke yao, kushinda baa na kutolazimishwa kupika wala kufua nguo za mume.

Wanasema wanataka uhuru na wala wanaume wasiwabughudhi kwa kuwabana kwani awali walipenda wakaishia kutendwa, hivyo hawana hamu tena na mapenzi na hawataki kusikia jina linaloitwa mwanaume!

Wamesema wanawaona wanaume wote ni baba mmoja na mama mmoja, hivyo hawataki kumuamini hata mmoja, wakaongeza kama watasikia hamu ya tendo watatumia njia nyingine kumaliza haja zao!

Kutendwa ni ajali ya mapenzi
Binafsi niliwaambia dada zangu hawa kwamba wajue maisha  ni mapenzi na katika hilo kuna kupenda na kupendwa ingawaje kutendwa ni sehemu ya  mchezo huo wa mapenzi ambao huchukuliwa kama ajali.

Niliwataka watulie na kujipanga upya katika maisha yao na wasikurupuke kumuamini kila mwanaume anayewaambia anawapenda na wao wakafikia hatua ya kujiachia miili yao.

Kikubwa nilichokibaini katika maelezo yao ni kuwa hawakuwa waangalifu kuchagua wanaume wa kuwa nao katika uhusiano zaidi ya kukimbilia kuwaamini wanaume zao, aidha kwa ajili ya tamaa za maisha au ulimbukeni.

Maisha ni mapenzi
Niliwataka waamini kuwa maisha ni mapenzi na hawawezi kuishi bila ya kuingia katika Uwanja wa Huba na kama wakiishi hivyo hawatakuwa binaadamu wa kawaida, watakuwa na matatizo katika vichwa vyao kwa kuwa kupenda na kupendwa nako  hutokea kama ajali.

Niliwataka wajue kuwa  Mwenyezi Mungu ametufanya watu tujue kusamehe na kusahau pindi tunapopatwa na matatizo na kuwatolea mifano binaadamu anavyoweza kusahau msiba wa baba au mama yake, sembuse mapenzi!.

Wao ni akina nani wasiweze kusahau kutendwa kimapenzi?  Nikataka wajue kuwa maisha ni mapenzi bila ya kuishi katika bahari hiyo hakuna maisha, hivyo hawataweza kuthubutu kuweza kuishi bila ya  kuwa na wapenzi kama wanavyotaka kuzidanganya nafsi zao.

Mwisho mmbaya
Niliwaambia kama kweli watathubutu kuishi maisha ya kukesha katika  kumbi za muziki na mabaa  watakuwa na mwisho mmbaya kwa kuwa wataendelea kuchezewa na wanaume kila watakapoamini wamempata  mtu mwaminifu.

Baa na kwenye kumbi za muziki ni sehemu ambazo zina vishawishi vingi sana vya kuwafanya kuingia katika ngono zembe ambazo zinaweza kuwaingiza hatarini. Pia huko watakutana na wanaume ambao nao walishatendwa na hawataki wanawake kwa sababu ya ndoa bali ni kwa ajili ya kusterehesha nafsi zao.

Njia moja tu!
Niliwaambia kuwa kuna njia moja ya starehe ya kukata kiu zao tofauti na njia mbadala wanayoitumia, kwani Mwenyezi Mungu si mjinga kuumba njia ya kukutana kwa mume na mke, kama ingekuwa vinginevyo angehalalisha hiyo wanayoitumia wao.

Wanataka  wanaume mabwege?
Kikubwa nilichokibaini ni  kwamba dada zangu hawa ndiyo chanzo  cha migogoro katika uhusiano na wenza wao, nikawaambia sidhani kama wataweza kuwapata wanaume wanaowafikiria kwa urahisi, wanaume  wanaoweza kuuchapa usingizi wakati wao wakijirusha klabu.

Sijui, labda inawezekana leo hii kumpata mwanaume ambaye anamuacha  mke wake akikesha baa na kutofanya kazi yoyote ya nyumbani kama vile kupika na kufuta vumbi bila ya makubaliano ya msingi.

Kwa mtazamo wa haraka niligundua kuwa, dada zangu hao hawajui maisha ya mapenzi kuwa yanaendana na mila na desturi zetu, hivyo ingekuwa vyema kama wangeamua kubadilika na kuishi katika dunia  ambayo Watanzania wengi wanaishi.

Wivu
Siku zote wachambuzi wa mapenzi wanasema kwamba penzi bila ya wivu usio wa kupitiliza ni sawa na mchuzi bila ya viungo, hivi kweli mwanaume mwenye hisia zake anaweza kukoroma wakati mkewe anakata nyonga  Ngwasuma au Twanga Pepeta?

Kama hivyo ndivyo,  mwanaume huyo akisikia mkewe amepata ajali wakati anarudi kutoka viwanja, anaweza  asishtuke kwa kuwa mishipa yake ya hisia itakuwa  imekatika kiasi kwamba hawezi kutimiza majukumu yake muhimu. Wapendwa wasomaji wangu, hivi kuna haja ya kukata tamaa ya kupenda au kupendwa?

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya  True Love na Let’s Talk About Love  vilivyopo mitaani.  Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake;www. Shaluwanewblogspot.com

No comments: