BAADHI ya wanasiasa wa upinzani wametakiwa kujiepusha na lugha kali na kutumia maandamano kama suluhisho la matatizo na watambue kuwa aliyechaguliwa na wananchi kuongoza nchi anahitaji nafasi na chama chake atekeleze aliyoyaahidi.
Mwito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na Waziri Mkuu wa zamani, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Spika wa zamani wa Bunge ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta.
Viongozi wanaopita mikoani na kuhubiri kuwa Serikali imeshindwa huku wakihubiri umwagaji damu, wametakiwa kuepukwa na kupuuzwa kwa sababu wanafanya hivyo wakijua kuwa hata wangekuwa madarakani kuna mambo wasingeweza kuyafanya.
Akizungumza juzi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Loksale, Monduli mkoani Arusha, kushukuru wananchi kwa kumpa kura nyingi Rais Jakaya Kikwete na yeye kuwa Mbunge, Lowassa alisema CCM ndiyo inaongoza nchi kupitia Rais Kikwete, hivyo chama hicho kipimwe kama kimetekeleza kwa vitendo ahadi zake, kwa mujibu ya ilani yake.
“Kwa sasa kuihukumu CCM ni mapema mno na hiyo sijui kama itakuwa na maana kwa jamii … iwapo CCM itashindwa kutekeleza kwa vitendo yaliyoahidiwa
katika uchaguzi mkuu uliopita, ndipo chama hicho kinapaswa kuhukumiwa katika uchaguzi ujao na si sasa kwa maandamano na mambo mengine,” alisema..
Amesema, kama kuna mtu au kiongozi wa siasa mwenye hoja, anapaswa kuipeleka
bungeni kujadiliwa na si kufanya maandamano au vurugu, kwani siasa hizo hazikubaliki nchini.
“Siasa si kuandamana, siasa si kupigana na siasa si kubezana kwa mambo binafsi bali ni kujibizana kwa hoja mahala panapostahili kama vile bungeni, ‘’ amesema Lowassa.
Akizungumzia ahadi ya umeme, barabara, maji na elimu katika jimbo la Monduli kwa ujumla, Lowassa alisema ni suala aliloahidi, hivyo hana budi kulivalia njuga.
‘’Najua nyie hapa Loksale mna shida sana ya umeme, lakini mimi nawaomba na ninyi mnisaidie kujenga nyumba zenye ubora, ili umeme uweze kuwekwa na suala la umeme halina shida, litatimizwa bila wasiwasi,’’ alisema.
Kwa upande wake, Sitta aliwahadharisha wananchi juu ya kauli zinazotolewa na vyama vya upinzani akisema zinatokana na wao kukosa nafasi ya kuwa na serikali.
Akizungumza mjini Mwanza jana, baada ya ufunguzi wa warsha ya mawaziri na makatibu wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), alisema utafika wakati Watanzania wataanza kuwa na shaka na viongozi wanaotaka kuchukua nchi, huku wakitumia lugha za chuki zilizokosa staha.
“Tusiwashangae wapinzani kuikosoa Serikali iliyoko madarakani, kwani nao wanataka siku moja wawe na Serikali, hivyo kutumia lugha kali isiyo na tija kwenye jamii,” alisema Sitta.
Amesema, baadhi ya mambo yanayosemwa na wapinzani ni kwa sababu hawapo kwenye utawala na kwamba mambo si mepesi kama wanavyodhani, kwani yanazingatia kuelewana na nchi nyingine zinazotoa misaada.
Alisema ukame ni balaa kwa nchi yoyote inayoongozwa na Serikali ya chama chochote, hivyo wapinzani wasitumie fursa hiyo kuwahadaa wananchi kuwa wanaweza kukabiliana na hali hiyo na kuwataka wananchi kuwa makini na kutambua kama kweli inaweza kuwa Serikali mbadala.
Sitta alisema hivi sasa nchi ipo kwenye matatizo makubwa ya kukosa mvua, hivyo wananchi watazame hali hiyo na kuwaangalia wapinzani wanaotumia fursa hiyo kuitaka Serikali ya CCM iondoke kwa kutumia lugha kali ili kufanikisha azma yao.
Aliongeza kuwa si busara kwa wapinzani kuhubiri umwagaji damu na kuwataka
wananchi kulinganisha wapinzani na Serikali iliyoko madarakani kwa kuhoji kama itaweza kuwa serikali mbadala.
Hata hivyo akizungumzia mtazamo wake juu ya CCM alisema ni lazima ikubali kuwa vyama vya upinzani vimeanza kukomaa na kuwa si rafiki wa CCM hivyo isitarajie lugha nyepesi au kusifiwa.
“Serikali ya CCM itatekeleza majukumu yake kadri ya uwezo wake kwa yale
Yanayowezekana, lakini tusitarajie upinzani kuwa na huruma kwa CCM,” alisema,
Aliwashauri wana CCM wenzake kukubali kujirekebisha pale wanapokosea na kuwachukulia hatua viongozi waliopo madarakani ambao ni kero kwa wananchi kwa kujinufaisha wenyewe.
“Wapo baadhi yetu wanajulikana kwenda kinyume na maadili, kwa kuwa na biashara kubwa wakati Baba wa Taifa alikuwa akipinga jambo hilo, huku akiwataka watu wote kuwa sawa,” alisema na kuongeza kuwa adui wa masikini ni tajiri.
Hivi karibuni viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema wamekuwa wakipita mikoani na kuandaa maandamano ya kuipinga Serikali wakidai kuwa imeshindwa kutatua matatizo ya wananchi na kuhamasisha uasi kwa wananchi hao huku wakiotoa lugha kali na za chuki na uchochezi.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment