Na Tumaini Makene
MCHAKATO wa safari ya upatikanaji wa katiba mpya ya nchi sasa unaonekana kuiva ambapo mswada wa sheria itakayoweka utaratibu mzima, uko katika hatua ya
kuchapwa kabla ya kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kuridhiwa na kupitishwa.
"Mheshimiwa Mwenyekiti nitaanza na suala la katiba...kama unavyojua katiba ni mchakato mrefu. Suala hili lilianza mara baada ya wananchi walipoanza kulizungumzia. Pia rais katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka mwaka jana alilizungumzia.
"Kilichokuwa kikitakiwa ni kuandaa sheria ya mabadiliko ya katiba, waraka tayari ulishaandaliwa, ukapelekwa kwenye technical committee ya makatibu wakuu wa wizara, kisha ukapelekwa kujadiliwa katika baraza la mawaziri. Sasa uko kwa printer (mchapishaji) kwa ajili ya kuchapwa tayari kwa mchakato wa bungeni ambao unaujua jinsi ulivyo."
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Bw. Oliver Mhaiki alipokuwa akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na baadhi ya wabunge wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, ambao jana, chini ya Mwenyekiti wake, Bi. Pindi Chana walikutana na watendaji wa wizara hiyo.
Mapema wakati wakichangia na kuuliza maswali kutokana na taarifa ya Waziri wa Sheria na katiba, Bi. Celina Kombani, baadhi ya wabunge walitaka kujua pamoja na masuala mengine, maendeleo ya mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, kama ambavyo tayari serikali imeshaweka wazi, kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete.
Mmoja wa wabunge hao waliotaka kujua mwenendo wa mchakato wa uandaaji wa mswada kwa ajili ya sheria ya mabadiliko ya katiba, umefikia hatua gani, alikuwa ni Bi. Angellah Kairuki (Viti Maalum, CCM) ambaye pia alihoji masuala kadhaa ya utendaji wa wizara hiyo, ikiwemo kuzorota katika upandishaji vyeo wafanyakazi na ulipaji wa posho.
Mbunge wa Mbulu (CHADEMA), Bw. Mustapha Akunaay, alihoji umuhimu wa nchi kuwa na wataalamu au wanasheria wanaohusika wa mikataba lakini bado taifa limetumbukizwa katika mikataba mibovu, inayoligharimu hasara, tangu mwaka 1994.
"Nchi hii imekuwa imekumbwa na tatizo la mikataba mibovu tangu mwaka 1994, kila mkataba unaotiwa saini ni mbovu, basi kama ndivyo hivyo hakuna haja ya kuwa na idara hiyo, ni bora tukaifunga, kisha tuka-outsource (tukatoa nje ya nchi)...kitakuwa si kitu kigeni, nafikiri huko nyuma tuliwahi kufanya hivyo," alisema Bw. Akunaay.
Mbunge huyo pia alizungumzia matatizo ya wanafunzi wa Shule ya Sheria, ambapo alisema kuwa hawathaminiwi ipasavyo na kuwa hawasomi kwa vitendo, hivyo hakuna tofauti na masomo ya nadharia waliyofundishwa wakingali chuoni wakichukua shahada zao za sheria.
Mchangiaji mwingine, mmoja wa mawakili maarufu nchini, Bw. Nimrod Mkono (Mbunge wa Msoma Vijijini, CCM) naye alionekana kuunga mkono hoja ya 'kubinafsisha' baadhi ya maeneo katika mfumo wa mahakama nchini, ili kuwa na tija katika utendaji wake.
Akichangia kwa hoja yenye mifano, akidhihirisha uzoefu wake katika fani ya sheria, Bw. Mkono alionekana kusikitishwa na namna mhimili wa mahakama unavyotendewa na mihimili mingine ya serikali yaani bunge na dola, hususan katika suala la udogo wa bajeti.
Aliongeza kuwa kusema kuwa anajiandaa kuondoa 'shilingi moja' wakati wizara hiyo itakapokuwa ikiwasilisha bajeti ijayo, mpaka apate majibu ya kukithiri kwa rushwa na kucheleweshwa kwa hukumu katika mhimili huo, akisema kuwa kuchelewa kwake kumekuwa kukitengeneza mianya ya uovu huo.
Alisema mahakama imekuwa haitendewi haki na kujengewa mazingira mazuri ya kufanya kazi kama ilivyo kwa mihimili hiyo mingine, akisema kuwa serikali imekuwa haitaki kusikia juu ya suala la kujali mahakama.
"Mwenyekiti...mambo mengi hapa yanajirudia rudia tu, tangu nilipoanza kuwa mjumbe wa kamati hii, miaka kumi na moja sasa...tuwe fair kwa mahakama, hatuwatendei haki, wapewe mazingira mazuri kama ilivyo mihimili mingine, things are not okay (mambo hayako sawa), ndiyo maana kuna rushwa huku. Serikali haitaki kusikia hili.
Mapema akiwasilisha taarifa yake kwa kamati hiyo ya kudumu ya bunge, Bi. Kombani alisema kuwa moja ya changamoto inayoikabili wizara hiyo ni ufinyu wa bajeti, ambayo unasababisha haki kuchekeweshwa na hivyo kuonekana haijatendeka.
Alisema kuwa mpaka sasa mahakimu wa mahakama mbalimbali nchini hawatoshelezi mahitaji, ambapo wale wa mahakama za mwanzo wamekuwa wakilazimika kusafiri kutoka kata moja au tarafa, kwenda nyingine kusikiliza kesi na kutoa hukumu, kutokana na uhaba, akitaja takwimu kuwa kuna mahakama za mwanzo 1,105, mahakimu wakiwa ni 759.
No comments:
Post a Comment