Mkazi wa Kata ya Mngazi , Tarafa ya Bwakila, Wilaya ya Morogoro, Jonisia Kibeo ( kulia) akimfunika nguo mdogo wake, Stella Theodori ( 16), mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari Milengwelengwe, aliyelazwa katika wodi ya zahanati ya kijiji cha Mngazi baada ya kupigwa na radi jioni ya Machi 25, mwaka huu. Wanafunzi 17 walikumbwa na balaa hilo, watatu walikufa akiwemo wa shule ya msingi. Aliyekaa nyuma) ni majeruhi mwingine, Zaina Litambiko ( 17) ambaye pia ni wa shule hiyo ya sekondari hiyo. (Picha na John Nditi).
WATU watano wakiwemo wanafunzi watatu wa shule mbili katika Tarafa ya Bwakila wilayani Morogoro, wamekufa papo hapo baada ya kupigwa radi.
Wanafunzi waliokufa na wengine 14 kujeruhiwa, ni kutoka Shule ya Sekondari ya Milengwelengwe na Shule ya Msingi Mngazi. Matukio hayo ni ya wiki iliyopita.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Milengwelengwe walipatwa na mkasa huo wakati wakiwa kwenye mchezo wa kirafiki wa mpira wa miguu na timu ya Kijiji cha Gomero, ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya Ummiseta ngazi ya Wilaya ya Morogoro.
Diwani wa Kata ya Ngerengere, Kibena Kingo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alithibitisha tukio hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Issa Machibya na viongozi wengine wa Serikali ya Wilaya na Mkoa.
Mkuu wa Shule hiyo ya Milengwelengwe , Mugusi Burwae aliyekuwa mwamuzi wa mechi hiyo, alisema ajali hiyo ilitokea saa 11: 43 jioni Machi 25, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Burwae, siku hiyo kulikuwa na mchezo wa kirafiki wa mpira wa miguu baina ya Shule yake na timu ya Kijiji cha Gomero, ambapo kabla ya kufikia mapunziko, mvua ilianza kunyesha kitendo kilichowafanya wanafunzi waliokuwa wakishangilia kukimbilia kujificha madarasani.
Hata hivyo, alisema punde ilipiga radi kubwa wakiwa mchezoni na kuwafanya wachezaji wa timu hizo kulala chini na yeye kubaki amesimama.
Alisema, baada ya dakika mbili kupita, Mwalimu mwenzake alifika uwanjani kumpatia taarifa kuwa radi iliyopiga imewaua baadhi ya wanafunzi waliokuwemo madarasani.
Aliwataja waliokufa papo hapo baada ya kupigwa na radi hiyo ni Richard Abias (15), mwanafunzi wa kidato cha kwanza na mwingine ni Adolf Kunambi (20) wa kidato cha nne.
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mngazi wa darasa la tano aliyekufa ni Abdallah Kibwe (12).
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Shule, wanafunzi wengine 14 walijeruhiwa na kukimbizwa katika Zahanati ya Kijiji cha Mngazi na kulazwa.
Alisema, watatu walikuwa na hali mbaya na walihamishiwa Kituo cha Afya cha Duthumi kupata matibabu zaidi.
Alisema, majeruhi wawili kati ya watatu waliokuwa bado wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Duthumi na zahanati ya kijiji hicho walihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.
Majeruhi hao ni Stella Theodori (16) wa kidato cha pili na Seleman Omari wa kidato cha nne. Majeruhi mwingine, Zainabu Litambiko (17) wa kidato cha pili hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri.
Katika tukio lingine, wafugaji wawili walikufa kwa kupigwa na radi Machi 19, mwaka huu katika Kitongoji cha Mikobola, Kata ya Ngerengere.
Waliokufa wametambuliwa kwa jina moja kuwa ni Sembeu (28) mkazi wa Kijiji cha Sinyaulime pamoja na Chamiti (55) mkazi wa Kijiji cha Diguzi ambao kwa pamoja walifika katika kitongoji hicho kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa kifamilia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Machibya, alisema ndani ya mwezi huu, watu wanane wamekufa kwa mpigo.
Alisema, majanga hayo ya radi yapo kila mahali hasa nyakati hizo za mvua na kutolea mfano kuwa katika Mkoa wa Iringa, ambapo yeye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa, radi iliua watu watano kwa mara moja.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Mwambungu, aliwataka wananchi kuwa na utulivu na kuona vifo hivyo vimetokana na mapenzi ya Mungu na si kuingiza imani za ushirikina ndani yake.
Serikali ya Mkoa pamoja na viongozi wengine akiwemo Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Innocent Kalogeries kwa pamoja walitoa Sh 700,000 kwa wafiwa wa familia hizo tatu ikiwa ni rambirambi.
CHANZO:HABARI LEO |
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake