Monday, March 28, 2011

'Babu wa Loliondo' azuia wagonjwa

MCHUNGAJI Mstaafu, Ambilikile Mwaisapile ‘Babu wa Loliondo’, ameomba Serikali kusitisha huduma za kupeleka magari na watu kijijini kwake Samunge wilayani Ngorongoro hadi Ijumaa wiki hii ili kuwezesha wagonjwa zaidi ya 24,000 waliopo huko kupata tiba. 

Akizungumza na jopo la wanahabari waliofika kijijini hapo juzi, Babu alisema magari yamefika 4,000 ambayo yapo katika foleni ya kupata tiba na magari yaliyoharibika yanakadiriwa kufika 100, hivyo hali hiyo ni mbaya, kwani inawasababisha wagonjwa kukata roho wakiwa wanasubiri kupata tiba katika foleni.
 

“Ni lazima sasa jitihada za makusudi zifanyike na naomba Serikali baada ya hapa, waruhusu watu 2,000 kuingia huko kwa siku ili wawe wanapata tiba na kugeuza na siyo kulala huku,” alisema Mwaisapile. 

Aidha, alisema watu waliopo sasa wamefika hadi umbali wa kilometa 55, hali inayosababisha kukaa zaidi ya siku tatu hadi saba na baada ya hapo matokeo yake ni vifo. 

Alisema hali hiyo inawezekana kuidhibiti kabla ya hatari kubwa kutokea na hajisikii vizuri kuona tiba hiyo imegeuka kuwa kero na adha kwa watu, kwani haimpendezi hata Mwenyezi Mungu aliyeleta uponyaji huo. 

Mchungaji huyo mstaafu pia alikubaliana na ombi la Serikali la kutaka kutoza Sh 5,000 kwa gari na Sh 150,000 kwa helikopta ili kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mapato ya kuwezesha kujenga miundombinu ya eneo hilo. 

“Pia wakati Serikali inazuia kuingia kwa magari na watu kijijini hapa, naomba wajenge miundombinu mizuri na kuleta maji na kujenga vyoo, pamoja na mahali pa kupumzikia wagonjwa ili kuondoa adha iliyopo” alisisitiza Mchungaji Mwaisapile. 

Alisema aliwaomba wagonjwa wanaotumia dawa za aina mbalimbali, wasiache kutumia dawa zao, pindi wanapotembelea kijijini hapo. 

Aliwataka waendelee na dawa zao hata wakiwa katika foleni mpaka pale watakapopata tiba yake, ili kuepuka vifo vinavyotokana na kukatiza tiba za hospitalini. 

“Lakini pia naomba wagonjwa mahututi pia wasije hapa, kwani hapa siyo hospitali ya rufaa na hawezi kuzuia kifo kwa namna yoyote ile, waje wagonjwa wenye hali nzuri na wenye kumudu kunywa kikombe chote cha tiba,” alisema Mchungaji Mwaisapile. 

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige alimuuliza Mchungaji huyo, uwezekano wa kuhifadhi miti hiyo, ili isipotee. 

Akijibu swali la Waziri, Mchungaji huyo alisema miti hiyo iko mingi na uwezekano wa kuisha ni ndoto, hivyo hakuna wasiwasi juu ya kutoweka kwa miti hiyo kwa sasa na hata kesho. 

Naye mkazi wa Mbeya, Magdalena Maglasa (65), naye alishuhudia uponyaji wa moyo mkubwa uliokuwa ukimsumbua miaka zaidi ya 10, saa chache baada ya kupata kikombe cha tiba ya Mwaisapile. 

Akizungumza na wanahabari waliotembelea kijijini hapo, mgonjwa huyo akiwa ndani ya gari aina ya Coaster, alisema anayo furaha, kwani kwa miaka mingi mwili wake ulikuwa mzito kama mtu aliyebeba jiwe na kumsababishia shida ya kutembea. 

“Lakini leo nina masaa mawili tangu nipate kikombe hiki, nasikia mwepesi kama karatasi na najisikia uhai umenirudia, nashukuru Mungu, kwani nimehangaika hospitali zote nchini, lakini sikupata nafuu hadi leo nilipopata kikombe hiki,” alisema. 

Alisema mwito wake kwa watu wenye matatizo mbalimbali watembelee Samunge ili wapate uponyaji wa kweli na waache kusikiliza maneno ya watu. 

Naye Amiri Hassan (54), mkazi wa Tabora, ameiomba Serikali, kuingilia kati kuzuia magari yanayoingia kwa wingi kila siku, ili kunusuru maisha ya walioko huko. 

Ombi hilo alitoa jana wakati akizungumza na wanahabari, waliotembelea Samunge na kujionea maiti za watu zaidi ya 10 zikiwa zimetupwa kila mahali, na ndugu zao hawaonekani. 

Alisema hali hiyo inatokana na watu kupanga foleni kwa wiki moja, huku hali zao zikiwa mbaya na kujikuta wakifikwa na mauti wakiwa katika foleni, hivyo Serikali ikiingilia kati, itawezesha watu kufika kijijini hapo mara moja na kurudi. 

“Hali za watu ni mbaya kiafya na hata kimazingira, kwa sababu taka zinatupwa ovyo, kuomba kuoga kwa watu shilingi 500 kwa mtu mmoja hadi shilingi 1,000, na ukitaka kujisaidia pia ni ivyo hivyo na wengi wetu tumeishiwa fedha sababu nauli nayo kubwa shilingi 150,000 kufika kijijini hapa,” alisema.


CHANZO:HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake