HALI si shwari ndani ya migodi ya tanzanite Mererani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, baada ya mlinzi wa TanzaniteOne, Raphael Aswela (45), kulipuliwa kwa bomu la kutengenezwa nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Polisi mkoani Manyara, Aswela yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi Hospitali ya Rufaa ya KCMC huku akiwa amekatika mguu wa kulia, mkono wa kushoto, vidole vitatu vya mkono wa kulia na pia amejeruhiwa machoni.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika eneo la Kitalu B kinachomilikiwa na Sammy Mollel na kufadhiliwa na Philipo Mkenga ‘Jangu Master’.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Palmera Sumari alipoulizwa kwa njia ya simu, alikiri kuwepo kwa tukio hilo, lakini alisema hawezi kutoa taarifa mapema kuhusu tukio hilo kwa kuwa uchunguzi zaidi unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwatia mbaroni waliohusika na ulipuaji huo.
Kamanda Sumari alisema, hawezi kuthibitisha kama ulipuaji huo ni bomu la kutengeneza ama ni baruti za kawaida za migodi, hivyo aliomba muda ili atoe taarifa za uhakika zaidi.
Hata hivyo, habari kutoka Kituo cha Polisi Mererani zilieleza kuwa wachimbaji wawili wa mgodi huo wa Mollel na kufadhiliwa na Jangu Master, wameshakamatwa na wengine wanasakwa na Polisi.
Aidha, inaelezwa kuwa mchimbaji wa mgodi huo aliyetajwa kwa jina la Richard Mkenga, naye amejeruhiwa katika tukio hilo, lakini haieleweki amepelekwa katika hospitali gani.
Hata hivyo, kuhusu Aswela, mmoja wa wahudumu wa Hospitali ya KCMC aliyeomba kutotajwa jina lake, alisema mgonjwa huyo alipelekwa hapo na wafanyakazi wenzake wa TanzaniteOne huku akitokwa na damu nyingi na hali yake ni mbaya na ndio maana yuko katika chumba cha uangalizi maalumu.
‘’Huyu mlinzi amekatika mkono na mguu na amekatwa vidole na jeraha kubwa chini ya goti…hawezi kuwa katika hali nzuri kwa hali hiyo,” alieleza mhudumu huyo.
Habari kutoka katika eneo la tukio, Kitalu B, zilidai wamiliki na mfadhili wa mgodi huo wanatuhumiwa kufanya matukio hayo mara ya tatu sasa, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na Ofisi ya Madini iliyoko Arusha na hata Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wahusika wa mgodi huo.
Mchimbaji madini hayo ya tanzanite aliyejitambulisha kwa jina Olodi Mollel, alidai inasikitisha kuona maofisa wa Serikali wanashirikiana na wahalifu kuleta madhara katika migodi ya madini Mererani.
Kumekuwa na matukio ya kufanyiana hujuma katika uchimbaji wa madini ya tanzanite, ambayo yanapatikana Tanzania pekee, na mara nyingi wachimbaji wadogo wamekuwa wakikwaruzana na Kampuni ya TanzaniteOne katika shughuli zao.
Juhudi za kuwapata viongozi wa TanzaniteOne jana hazikuzaa matunda, ingawa baadhi ya wafanyakazi wake walieleza kuwa huenda wakatoa taarifa muda wowote kuanzia jana.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake